Huhitaji kuwa na elimu ya sekondari lau ya kidato cha kwanza, kubaini kwamba Azam FC inaandaliwa kuwa bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Unachoweza kujiuliza ni kuwa Bodi inayoendesha Ligi Kuu Bara (TPLB) inatupeleka wapi?
Katikati ya mashindano ya kuwania taji la Ligi Kuu Bara, michuano inayoshirikisha timu 16, Azam inapewa ruhusa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwenda Zambia kucheza bonanza na kuziacha timu nyingine zikipambana.
Tayari imetengenezewa viporo viwili kwani wikiendi iliyopita, kwenye moja ya michezo yake ingeivaa Stand United, lakini TFF imeipa baraka timu hiyo, eti kwa mwaliko wa Zesco ya Zambia.
Ndiyo, inakwenda kushiriki bonanza kama la pale Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam linaloweza kuandaliwa na taasisi yoyote ambako timu kama Kambarage ya Songea inaitwa kushiriki. Tumeona hivyo hasa wakati wa Sherehe za Pasaka.
Katika kuwania usukani wa Ligi Kuu Bara, Azam na Yanga zimeshindana sana. Leo timu hii ikishika usukani, haipiti wiki inashushwa na mpinzani wake anakalia kiti.
Kuna kipindi Azam ilikuwa ina kiporo cha mchezo mmoja, kikawa kinampa nafasi ya kushindana vema, lakini leo hii imekwenda Zambia, huku nyuma Yanga imepoteza mchezo mmoja tayari.
Hakuna ubishi tayari hapo ni faida (advantage) kwa Azam kwani itabaki na michezo yake 16 wakati Yanga na Simba zinazowania kiti hicho zitakuwa mbele katika michezo.
Si kwamba Azam wameondoka wote, bila shaka kuna watendaji wake waliobaki. Wanaofuatilia michezo ya Ligi Kuu na kuangalia kasi za wapinzani wao.
Unaweza kujenga imani ya ‘fitna’ za soka la Bongo ambalo wale wa karibu wanajua. Ni rahisi kwa sasa makamanda waliobaki wakawa na kibarua cha kuhakikisha Yanga na Simba hazifanyi vema ili Azam ikija inapeta kwa urahisi. Tayari Yanga imetunguliwa na Coastal. Imepigwa mbili mtungi kama imesimama.
Fitna ya Azam ilifahamika mapema kwamba imepata mwaliko huo. Yanga ikashtuka na ikaomba ruhusa iende Afrika Kusini. Ikakataliwa ilhali wanalambalamba wameruhusiwa.
Simba ikatangaza nayo inataka kwenda Kenya, nao wakala kibano na TFF ikawaambia acheni wivu, pigeni soka.
Katika akili ya kawaida unaweza ukajiuliza na kupata majibu ya haraka tu kwamba hapa kuna timu inaandaliwa mambo mazuri. Na ndiyo hayo tunayoweza kujadili hapa kwamba Azam inaandaliwa ubingwa.
Hii maana yake nini? Hapa TFF inaonesha udhaifu mkubwa kwa kuiruhusu Azam kuacha Ligi Kuu kwenda kushiriki bonanza nchini Zambia la timu nne.
Licha ya Simba na Yanga kutangaza nao wamepata mwaliko maalumu – Yanga kwenda Afrika Kusini na Simba ikataka kwenda Kenya – TFF imesema: “Hapana” kwa wababe hao wakongwe.
Mwenyekiti wa TPLB, Ahmad Yahaya, anatetea kuwa Azam ilikuwa na mwaliko huo tangu mwaka jana na kwamba Simba na Yanga zisiige, lakini katika hali ya ushindani wa ligi, unapata shaka.
Haji Manara, msemaji wa klabu ya Simba, anasema: “Timu yetu haitacheza mechi zijazo mpaka timu zote zishiriki. Hapa kuna wasiwasi wa kuachwa nyuma.”
Anasema kwamba wataendelea na michezo ya ligi ukiwamo wa Jumamosi iliyopita dhidi ya African Sports, lakini wataiandikia TFF juu ya kumaliza viporo vya Azam mapema kabla ya kuingia mechi za mwisho wa ligi.
Msimamo kama huo unafanana na wa Yanga ambako msemaji wao, Jerry Muro, anasema: “Imetushangaza sana sisi kunyimwa nafasi, wenzetu wanapewa. Bodi iliangalie hili, Azam ikirudi imalize viporo vyake na ndipo ligi iendelee.”