Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Licha ya Serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji katika maeneo mengi nchini bado lipo tatizo la miradi hiyo kushindwa kuwa endelevu na kuisababishia hasara Serikali.

Waziri wa Maji nchini Juma Aweso amebainisha hayo leo June 27,2023 jijini hapa, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi za Wakurugenzi ya Mfuko wa Maji wa Taifa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini.

Amesema ujenzi wa miradi ya maji hivi sasa siyo tatizo kwakuwa Serikali imekuwa ikiwezesha fedha nyingi katika maenneo mengi lakini tatizo lililopo hivi sasa ni kushindwa kuwa endelevu.

Kutokana na hayo ameitaka Bodi ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kuangalia namna ya miradi ya maji inavyoweza kujiendesha yenyewe katika maeneo ya vijijini na kumaliza kero ya maji.

Aweso pia ameiagiza Bodi ya Mfuko wa Maji wa Taifa kutafuta vyanzo vingine vya mapato badala ya kuendelea kutegemea fedha zinazotolewa na serikali.

“Serikali inatupatia fedha za mfuko wa Maji kila mwezi lakini Bodi hatupaswi kuendelea kutegemea chanzo kimoja kwani mahitaji bado mengi hivyo tutafute namna nyingine ya kupata fedha, mbona kuna taasisi zinapata fedha na sisi tutafute vyanzo vingine vya mapato”amesema Aweso

Naye Kaimu mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijimi (RUWASA) Bwai Biseko, amesema hadi kufikia Desemba 2022, jumla ya miradi 2,273 ya miundombinu ilikuwa imejengwa na kukamilika kupitia fedha za ndani na wadau wa Maendeleo.

“Miradi hiyo inanufaisha wanachi 11,641,230 katika vijiji 4,809. Katika kipindi hicho ujenzi wa mabwawa saba ulikamilika na jumla ya visima 947 vilichimbwa”amesema

Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi September 2022, RUWASA ilifanikiwa kuunda na kusajili CBWSOs 2,524 na zimeweza kuajiri watalaam 5,586 wa fani za ufundi, uhasibu na kada saidizi ili kuwa na uendelevu wa huduma.

Amesema,”Katika mwaka wa fedha 2023/2024, RUWASA imepanga kutekeleza jumla ya miradi ya maji vijijini 1,546 ikihusisha miradi ya ujenzi wa mabwawa ya kuhifadhi maji katika maeneo mbalimbali,”amesema