Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba inashika nafasi ya tatu mbele ya kinara Yanga na Azam, lakini taarifa za ndani ya klabu hiyo, zinasema kwamba haikustahili kuwa hapo hadi sasa.
Mmoja wa viongozi wa timu hiyo anasema kwamba itakuwa ni vigumu kwa Simba kutwaa taji la Ligi Kuu Bara kwani kuna tatizo kubwa la uongozi kushindwa kufuatilia mtiririko wa mambo.


Anasema kwamba kwa kikosi ilichonacho Simba kwa sasa ingekuwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini kutokana na hali hiyo itakuwa ngumu kwa Simba kutwaa ubingwa.
Bosi huyo aliyeomba jina lake lisitajwe kwa sasa anasema kwamba Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva  (pichani juu) hana budi kuvunja ‘Baraza lake la Mawaziri’ kwani wale anaosaidiana nao, “wamechoka.”


Amesema kwamba kama Avava hatavunja kamati mbalimbali za klabu hiyo, itabidi abebe lawama zote kwa timu kushindwa kutwaa ubingwa sambamba na kukosa kucheza mechi za kimataifa baadaye mwakani.
Anasema kuwa Aveva amekuwa akiwakumbatia watu ambao hawana faida yoyote katika timu zaidi ya kumdanganya kuwa timu inaweza kufanya vizuri kwa kuingiza kamati ya bufundi ambayo hutumia utamaduni kupata ushindi.


“Kama Aveva anataka Simba iwe timu bora zaidi basi inabidi atimue wajumbe wote na aunde upya maana watu wanaotakiwa  kuwa wajumbe wanaofaa anawajua na sio hao ambao wanatumia nafasi za kupata riziki Simba. Simba hakuna ugali, ni kujitolea,” anasema.
“Ajaribu kubadilisha wajumbe maana alionao wanamdanganya sana,” anasema Aveva ambaye hata hivyo, alionekana kushangazwa na taarifa hizo akisema, “Mbona tuko fresh. Tunafanya vema.”


Katika hatua nyingine, Simba iliweka mambo sawa kwa beki wake, Hassan Kessy ambaye awali alitoroka kambini baada ya kuona ‘longolongo kibao’ katika kile kilichoitwa kutimiziwa ahadi yake.
Mchezaji huyo alikuwa anaidai Simba fedha kadhaa baada ya kusajiliwa Desemba, mwaka jana akitokea Mtibwa Sugar inayotokea kwenye mashamba ya miwa yalioko Tarafa ya Turiani, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.


Akizungumza na JAMHURI, Athumani Tippo ambaye ni meneja wa Kessy, anasema walimaliza mzozo kati ya beki nhuyo na Uongozi wa Simba mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kupewa fedha ya nyumba na usafiri.
“Sasa tupo katika mchakato wa kutafuta nyumba nzuri ya kuishi mchezaji wangu, ila kuhusu zile fedha nyingine (milioni 5) wametuomba muda wa kumalizia na tumewakubalia,” anasema Tippo.


Anasema kwamba Kessy aliamua kuondoka kikosini Simba kutokana na madai hayo ambayo haikufahamika mara moja siku ya kulipwa.
Naye, Kessy alithibitisha kupokea  fedha hizo na kusema anashukuru Simba kumtimizia madai yake na kusema kuwa sasa anatalajia kujiunga na kikosi iko mapema wiki hii.  Kessy alijiondoa katika kikosi cha Simba akishinikiza kulipwa haki zake kwa mujibu wa mkataba ikiwemo Sh. Milioni tano, ikiwa ni sehemu ya dau la usajili na nyumba ya kuishi kama walivyokubaliana na uongozi wa Simba.