Kumeibuka mgogoro wa ardhi katika Kisiwa cha Juma Kisiwani, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza,
unahusu ekari 26 zinazomilikiwa na mfanyabiashara wa madini, Baraka Chilu; lakini mfanyabiashara wa samaki, Joseph Njiwapori, anadaiwa kulivamia eneo hilo.
Serikali ya Kijiji cha Juma Kisiwani imelifikisha suala hilo Polisi Wilaya ya Sengerema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Juma Kisiwani, Tibahikana Maharage, ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa Njiwapori ameingia isivyo halali katika eneo hilo.
“Hili eneo linamilikiwa na Baraka Chilu. Amepewa hati na mihitasari yote ya umilikishwaji ipo. Njiwapori amevamia,” amesema mwenyekiti huyo.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho (VEO), Deogratias Thomas, amesema Aprili 13 na 16, mwaka huu, alimwandikia Njiwapori barua kuhusu suala hilo lakini amekaidi mwito.
Ukaidi huo umemfanya awaandikie polisi barua, akimtaja Njiwapori kuwa anahatarisha amani eneo hilo ikiwa ni pamoja na ukataji wa miti alioufanya.
Chilu, amesema Njiwapori ameingia kwa mabavu katika eneo lake na kuweka kambi ya uvuvi.
Chilu ana hatimiliki ya eneo hilo yenye namba 1/SENG/KTR/404 iliyotolewa Februari 19, mwaka huu chini ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999. Amemilikishwa eneo hilo kwa miaka 99.
Ameomba vyombo vya dola kumchukulia hatua za kisheria Njiwapori.
Njiwapori ameulizwa kuhusu tuhuma za kuvamia eneo lisilo lake, amejibu kuwa kuna mazungumzo ya awali yalifanyika. Hakuweka wazi aina ya mazungumzo na aliyezungumza naye.
“Hilo suala nitalifanyia kazi baadaye,” amesema Njiwapori alipozungumza na JAMHURI kwa simu.
Amesema amepata taarifa za kuwekwa rumande wafanyakazi wake watano kutokana na mgogoro huo.
Miongoni mwa waliokamatwa ni msimamizi mkuu wa kambi hiyo, Rashid Mbona.
Ofisa mmoja wa Polisi Wilaya ya Sengerema amethibitisha kutiwa nguvuni wafanyakazi hao.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Juma Kisiwani wameeleza masikitiko yao juu ya uvamizi huo.
“Kama Njiwapori ana tabia ya kuvamia maeneo ya watu, tutaomba uitishwe mkutano wa kijiji tumjadili. Tumkatae aondoke,” amesema mkazi mmoja.