Noel Fungo (22) mkazi wa kijiji cha Ikondo jimbo la Lupembe wilayani Njombe,amehukumiwa kutumikia kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 9.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, John Makuri Imori, ameeleza hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Njombe wakati akitoa taarifa za mafanikio ya Jeshi la Polisi kwenye makosa mbalimbali kwa mwezi Julai.
“Katika mwezi Julai tumeweza kupata mafanikio mahakamani kwa maana ya kuwatia watuhumiwa hatiani,Noel Fungo ni mkazi wa kijiji cha Ikondo huyu alitiwa hatiani katika Mahakama ya Wilaya ya Njombe kwa kufungwa kifungo cha maisha kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka tisa”amesema Makuri.
Makuri ameongeza kuwa waliokuwa watuhumiwa wengine Yusuph Abraham mkazi wa kijiji cha Uganga wilayani Makete amefungwa miaka 30 kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wilayani humo,Otumary Wenderage mwenye umri wa miaka 38 amefungwa miaka 30 kwa kosa la kumbaka bibi kizee mwenye umri wa miaka 80 huku Christian Juma (31) akifungwa miaka 20 kwa kosa la shambulio la aibu kwa mtoto wa miaka 10.
Pia amesema Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya bangi kilo moja,mifuko 26 ya saruji,Mbuzi 15,Ng’ombe 9,mifuko 269 ya saruji na vifaa vingine pamoja na mali nyingine zilizokamtwa kutoka kwa wahalifu ikiwemo gari aina Toyota FunCargo yenye namba za usajili T 960 BMM,Pikipiki 2,Sabufa 2 na simu aina mbalimbali zipatazo 8.