Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Credit Suisse, Tidjane Thiam, ameukana uraia wake wa Ufaransa ili kutimiza masharti ya kugombea urais wa Ivory Coast katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Thiam, 62, ambaye alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha upinzani PDCI mwaka 2023, alitangaza kuwa amerejesha hati yake ya kusafiria ya Ufaransa na kubaki raia wa Ivory Coast pekee. Alisisitiza kuwa lengo lake ni kuleta mabadiliko na kuboresha maisha ya wananchi.
Thiam aliwahi kuwa waziri nchini Ivory Coast kabla ya kuhamia nje ya nchi baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1999. Alichukua nafasi za uongozi katika kampuni za kimataifa kabla ya kuongoza benki ya Credit Suisse mnamo 2015.
Wakati huo huo, Rais Alassane Ouattara, 83, ameashiria kuwa atagombea muhula wa nne, hatua inayotarajiwa kukumbwa na upinzani mkali.