Sisi sote tunatarajia vyombo vya habari na mchango wake wa Taifa letu. Kwa jumla vyombo vya habari hufanya kazi tatu. Huelimisha, huchochea maendeleo na huburudisha. Lakini pia vyombo vya habari hupunguza tatizo la ajira. Hutoa ajira.
Mwananchi wa kawaida hunufaika sana na vyombo vya habari. Anaelimika na anachochewa kimaendeleo, anaburudika, na anaweza kupata ajira.
Kwa upande wa kwetu Tanzania Taifa halinufaiki vya kutosha na uhuru mkubwa wa vyombo vya habari uliopo nchini. Viongozi hawafanyii kazi habari zinazotolewa na vyombo vya habari. Wanavipuuza.
Kabla hatujazungumzia kwa undani viongozi na Serikali kwa jumla inavyovipuuza vyombo vya habari, tuangalie historia ya vyombo vya habari katika nchi yetu angalau kwa kifupi.
Tanganyika (Tanzania Bara) ilianza na magazeti. Kwa miaka mingi wananchi wa Tanganyika na wa Afrika kwa ujumla hawakuyaamini magazeti. Kila kitu kilichoandikwa gazetini kilipuuzwa. Kilionekana ni uzushi. Watu waliposomewa jambo lolote kutoka gazetini walizoea kusema kwamba hayo ni mambo ya magazeti.
Magazeti Tanganyika yalianzia mwaka 1888 wakati wamisheni wa Kanisa la Kwanza la Anglikana nchini (Magila,Tanga) walipotoa gazeti la “Msimulizi.” Gazeti hili lilisimulia masuala ya elimu. Liliaminiwa na lilipendwa. Hizo zilikuwa enzi za utawala wa Mjerumani. Wakati wa utawala wa Mwingereza, Serikali ilianzisha gazeti la “Mamboleo” Mwaka 1923.
Gazeti la ‘Mamboleo’ liliwavutia zaidi washairi. Kulikuwa na ukurasa mzima wa mashairi. Wakatokea washairi maarufu walioendelea kuandika mashairi yao katika gazeti hilo, miongoni mwao ni Shaaban Robert, Abushiri Mbwana, na Mohamed Chipukizi.
Mambo mengine yaliyoandikwa katika gazeti la ‘Mambo Leo’ hata kama yalikuwa ya kweli yalisaidia kuwathibitishia wananchi kwamba magazeti ni uzushi mtupu. Kwa mfano, safari moja gazeti la “Mambo Leo” liliandika kwamba mti uliokuwa umeanguka miaka mingi nyuma ulikutwa umesimama!
Wakati wa Vita ya Pili ya Dunia ya mwaka 1939 hadi 1945, Serikali ilianzisha gazeti la “Habari za vita.” Wakati ule Tanganyika ilikuwa imepeleka askari wake 92,000 nje ya nchi kwenda kupigana upande wa Mwingereza Ethiopia, Somalia, Misri, Uyahudi, na Burma, kwa hiyo wananchi walifuatilia hali ya ndugu zao vitani kwa kusoma gazeti la “Habari za vita ” lililotolewa bure.
Gazeti la “Habari za Leo” lilichangia sana katika kuwafahamisha kwamba gazeti huandika uzushi mtupu. Kwa mfano, gazeti liliandika kwamba askari wa upande wa Mjerumani waliokufa vitani ni 100, litaandika kwamba waliokufa upande wa Muingereza ni wawili!
Katika mazingira hayo watu waliendelea kusema kwamba hayo ni mambo ya magazeti, ni uzushi. Baadaye mwaka 1950 Kanisa Katoliki lilianzisha Gazeti la “Kiongozi” lililokuwa gazeti la dini, liliaminiwa sana. Lilitolewa Kiwanda cha kupiga chapa cha Kipalapala, Tabora. Mhariri wake wa muda mrefu alikuwa Padre Kabeya, aliliendesha gazeti hilo kwa umakini wa hali ya juu.
Mwaka 1952 Dar es Salaam ilipata gazeti la kwanza la kila siku. Liliitwa “Mwangaza”. Gazeti hili liliwavutia sana wakazi wa Dar es Salaam kwa sababu liliandika mambo ya kweli yaliyokuwa yakitokea maeneo yao. Baada ya hapo yalianzishwa magazeti ya “Baragumu” na “Mwafrika”.
Gazeti la “Mwafrika” lilianzishwa wakati wa kudai harakati za uhuru zilizoongozwa na Chama cha TANU. Gazeti hilo lilipendwa na liliaminiwa sana na wananchi kwa sababu lilishiriki kikamilifu katika kudai uhuru wa Tanganyika. Kwa upande mwingine, Serikali ya Mwingereza Tanganyika iliona gazeti la “Mwafrika” kuwa ni la uzushi na uchochezi.
Ukafika mwaka 1958 kipindi cha mapambano makali ya kisiasa Tanganyika. Gazeti la “Mwafika” likathubutu kuandika kwamba “Mwingereza asiwadanganye wananchi kwamba yupo Tanganyika kwa lengo la kuwastaarabisha wakati yupo hapa kwa lengo la kuwanyonya.”
Wahariri wawili wa gazeti hilo, Rashid Baghdelleh wa Kilwa na Robert Makange wa Tanga, wakakamatwa. Wakaletwa Mahakama ya Kivukoni, wakahukumiwa kifungo cha miezi sita Gereza la Ukonga. Siku walipotoka gerezani walipokewa kishujaa katika mapokezi yaliyoongozwa na Chama cha TANU.
Kitendo cha Serikali ya Mwingereza kuwafunga wahariri wake kwa madai kwamba waliandika uzushi wakati walikuwa wameandika ukweli mtupu liliwapa mwanga. Wananchi walijifunza kwamba ukweli kuwa uzushi kwa yule anayeguswa na ukweli huo.
Desemba 9, 1961 Tanganyika ilipata uhuru. Chama cha TANU kilisherehekea siku hiyo kwa kutoa gazeti la “Uhuru”.
Mwaka 1967 Chama cha Taifa cha Wafanyakazi kilichoitwa NUTA (kifupi cha maneno ya Kiingereza National Union of Tanganyika Workers) kilianzisha gazeti la wafanyakazi lililoitwa “Mfanyakazi”.
Mwaka 1972 TANU ilianzisha gazeti la kila Jumapili lililoitwa “Mzalendo”. Basi kabla ya Tanzania kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 magazeti maarufu ya Kiswahili yalikuwa Kiongozi, Mfanyakazi, Uhuru na Mzalendo.
Magazeti hayo yote yalijitahidi kuandika ukweli mtupu katika kipindi hicho ambacho hakikuwa na ushindani mkubwa wa kisiasa, kilikuwa kipindi cha chama kimoja. Magazeti yalipoandika ukweli kuhusu kiongozi fulani, uongozi ulikuja juu. Kesho yake alidai kuwa mwandishi wa habari alikuwa amemnukuu vibaya.
Mwingereza enzi zake, mbali na kuanzisha gazeti la “Mambo Leo” mwaka 1923, alianzisha Kituo cha Redio mjini Dar es Salam Mwaka 1951. Kituo hicho cha redio kilianzishwa mtaa wa Kichwele (miaka hii Mtaa wa Uhuru) jirani kabisa na Kiwanda cha Bia, kiliitwa Sauti ya Dar es Salam kwa sababu redio ilisikika Dar es Salam tu.
Mwaka 1954 kituo cha Sauti ya Dar es Salaam kilihamishiwa Barabara ya Pugu (Barabara ya Nyerere) na kiliitwa Sauti ya Tanganyika kwa sababu redio ilisikika kote Tanganyika. Wananchi walinufaika na vipindi vya burudani kama michezo ya kuigiza, mashairi, na vichekesho pia kwa kupelekeana salamu zilizoandamana na muziki motomoto.
Baada ya kuingia mfumo wa vyama mwaka 1992, Tanzania haikupata vyama vingi tu. Pia ilipata vyombo vingi vya habari ikiwa ni pamoja na magazeti redio na runinga. Japokuwa hapa si mahali pake si vibaya tukizungumzia kwa kifupi Tanzania inavyonufaika na mfumo wa vyama vingi. Upinzani umesaidia kwa kiasi kikubwa chama tawala na Serikali yake kuendelea kuwa macho ili visinyang’anywe madaraka yake ya utawala.
Lakini Tanzania ingeweza kufanya vizuri zaidi kama ingetumia vizuri zaidi mfumo wa vyama vingi. Kilichotokea ni haki ya kuonekana waziwazi chama tawala na vyama vya upinzani. Kwa mfano, chama tawala kitatangaza kuwa kitanuia kutoa elimu bure. Chama cha upinzani kitainuka na kudai kuwa chama tawala kimeiba sera yake. Katika mazingira hayo hapana shaka vyama vya upinzani vimeficha sera zao mifukoni ikihofia kuwa sera hizo zitaibwa na chama tawala.
Vyama vya upinzani vinasubiri kutumia sera zake au mawazo yake mazuri vikishika madaraka ya utawala japo haijulikani lini. Kwa upande mwingine, Tanzania ina utaratibu mzuri wa kushirikisha vyama vya upinzani kwenye masuala ya Bajeti ya Serikali. Katika mkutano wa Bunge la Bajeti mawaziri halisi na mawazili vivuli (wa kambi ya upinzani) hutoa mawazo yao kuhusu utekelezaji wa shughuli za sekta mbalimbali za Taifa.
Haijulikani Serikali inatumia kwa kiasi gani mchango wa vyama vya upinzani, utakuta Serikali inaepuka kutumia mawazo mazuri ya vyama vya upinzani kwa kuhofia kwamba ikitumia mawazo hayo wapinzani wataaminiwa na wananchi na watapewa kura wakati wa uchaguzi. Ni ubinafsi tu unaodhoofisha maendeleo ya Taifa.
Sisi sote tunajua nchi zilizopata maendeleo makubwa duniani na zile zilizotumia vizuri mfumo wa vyama vingi, ukiweka kando nchi za kikomunisti. Tusije tukaendelea kujivunia mfumo wa vyama vingi ambao haunufaishi sana Taifa letu. Turudi upande wa vyombo vya habari unakuta kwamba uhuru wa vyombo vya habari ulioshamiri Tanzania haunufaishi sana Taifa letu mbali na kuwaelimisha, kuwaburudisha na kuwachochea wananchi kimaendeleo.
Tumebaki kuwa na sifa tu kwamba tuna uhuru mkubwa wa vyombo vya habari huku Serikali ikishindwa kutumia vizuri uhuru huo kwa maendeleo ya Taifa, kila mtu anajua kwamba Serikali inatumia mamilioni ya shilingi za umma kununua magazeti ya kila haina kwa ajiri ya mawaziri wake na maofisa wake mbalimbali.
Huwezi kukuta lundo kubwa la magazeti ofisi za Serikali. Ukweli ni kwamba ni viongozi wachache sana wa Serikali wanaofanyia kazi yanayoandikwa magazetini. Wengi wanaendelea kuyaangalia magazeti kama vyombo vya uzushi na uchochezi. Kuna magazeti ambayo yana safu maalum ya kuandika kero za wananchi. Lakini nani anajali!
Katika nchi zilizoendelea, kama Uingereza na Marekani, huwezi kukuta gazeti limeandika kashfa nzito inayomhusu waziri au kiongozi yeyote wa Serikali au Shirika la Umma, kesho ikawa kimya. Serikali itafuatilia mara moja kashfa hiyo kwa lengo la kujisafisha au kuchukua hatua kali dhidi ya mhusika.
Kwetu Tanzania mambo ni tofauti kabisa, waziri anaandikwa weee! mpaka magazeti yanachoka yenyewe Serikali iko kimya. Viongozi watawasiliana kwa simu na kuchekeshana kutokana na hayo yaliyoandikwa gazetini kana kwamba hayawaathiri wao wenyewe, Serikali na Taifa kwa ujumla.
Pengine hapa ni vyema tukizungumzia athari za Serikali za kupuuza magazeti na vyombo vya habari kwa ujumla. Kwanza, heshima ya mhusika inapungua mbele ya umma. Na kama kiongozi wa Serikali pia heshima ya Serikali inapungua.
Pili, kashfa ambayo inamhusu mtu mmoja isiposhugulikiwa huhusishwa na viongozi wengine. Watu huona kiongozi mhusika analindwa kwa sababu anachofanya hakimnufaishi peke yake. Wanasema wanakula naye.
Tatu, kwa kuwa kiongozi anayefanya maovu hachukuliwi hatua anaendelea kufanya maovu tena makubwa zaidi. Nne, magazeti hufika mahali yanachoka kufichua maovu, kwa hiyo maovu yanaongezeka. Tano, tusije tukasahau kwamba magazeti yetu yanasomwa na wageni na majirani zetu wanapoendelea kusoma kashfa ambazo hakuna anayeshugulikia na sisi tumesifika kwa utawala bora, bila ya shaka wanatushangaa, wanatucheka, na wanatudharau.
Sita, mbele ya wananchi na mbele ya wageni Serikali inaonekana ni dhaifu. Nani anaheshimu Serikali dhaifu? Saba, wananchi wanapoteza kabisa imani juu ya Serikali yao. Kila mtu anajua matokeo ya wananchi kupoteza imani juu ya Serikali yao. Wanajitenga na chama tawala na Serikali yake wanaungana na vyama va upinzani.
Chukua kwa mfano, ubabe wa Serikali iliyodumu mikoa ya Lindi na Mtwara kwa miaka miwili ambapo wananchi wameendelea kusumbuliwa na jeshi lao la ulinzi na wamezuiwa kufanya mikutano ya hadhara. Viongozi wa mikoa wakiwamo chama tawala waliendelea kulalamika kupitia vyombo vya habari. Lakini hakuna aliyejali.
Niliwahi kuandika katika gazeti hili kwamba kwa miaka mingi mikoa ya Lindi na Mtwara imekuwa ngome ya kutegemewa ya Chama Cha Mapinduzi. Nikaishauri Serikali itumie busara katika kushughulikia matatizo ya gesi kule kusini. Hata Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliwahi kuitaka Serikali iwasikilize wananchi wa kusini. Lakini nani alijali. Nilionya kwamba Serikali ikiendeleza ubabe wake kusini wananchi watakikimbia chama tawala. Nilichoandika ndicho kilichotokea.
Majuzi wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, wanachama wote wa CCM Kijiji cha Lihanga, Mtwara, wamejiunga na CUF. Anguko la CCM halisababishwi na vyama tawala na Serikali yake. Lakini dalili ya mvua ni mawingu. Hiyo mvua iliyonyesha majuzi Mtwara inaweza kuwa mvua ya rasharasha tu. Mvua zenyewe za masika zitanyesha wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na chaguzi zitakazofuata baada ya hapo.
Sisi sote ni mashahidi unapofika wakati wa uchaguzi tumezoea chama tawala kikijigamba kwamba Serikali yake ni sikivu na inashugulkia vyema kero za wananchi.
Hakuna asiyekubali kwamba Serikali imefanya kazi nzuri katika kushughulikia kero za wananchi. Lakini ingeweza kufanya vizuri zaidi kama isingepuuza vyombo vya habari. Serikali imeshindwa kutumia vizuri uhuru mkubwa wa vyombo vya habari uliopo nchini. Sasa ikabili athari zake.