Akifafanua madhumuni ya elimu kwa Taifa katika kuielezea sera ya Elimu ya Kujitegema, Rais Julius Kambarage Nyerere alitamka yafuatayo:
“Kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kazi kingine maarifa na mila za Taifa, na kuwaandaa vijana wawe tayari kuchukua nafasi zao katika kulitumikia na kuliendeleza Taifa.”
Umuhimu wa elimu kwa Taifa haupingiki. Lakini upo utata unajitokeza iwapo mhitimu habaini uhusiano wa moja kwa moja kati ya elimu aliyonayo na hali yake ya maisha.
Hata kama serikali na sekta binafsi zinawekeza kiasi cha kutosheleza mahitaji yote ya elimu nchini, hiyo pekee haiwezi kubadilisha mtazamo wa mwanafunzi anayehitimu elimu katika ngazi yoyote na asiione elimu yake kama nyenzo muhimu ya kuboresha maisha yake.
Ni suala ambalo halihusu elimu iliyopatikana tu, lakini linahusu pia ajira ambayo inaweza kutokana na elimu hiyo.
Mara kwa mara napata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa shule za msingi ambao huwauliza malengo yao ya kazi pale watakapokuwa watu wazima. Baadhi ya majibu ninayopata yanaashiria kutokuwapo kwa imani kuwa kutafuta elimu ni jambo muhimu kwao.
Mwanafunzi mmoja aliniambia kuwa yeye akiwa mtu mzima ataenda kusoma Kenya na baada ya hapo atafanya kazi ya kuuza mkaa.
Nilipotafakari sababu za mwanafunzi yule kukaa shule muda wote huo na baadaye kuwa mjasiriamali wa kuuza mkaa sikupata jibu la kuridhisha. Yeye mwenyewe hakuwa na jibu. Hata hivyo, naamini alinijibu kwa kutumia uzoefu wa maisha aliyoshuhudia kijijini, ambako muuza mkaa anaweza kuwa ana kipato kikubwa zaidi kuliko mwalimu anayemfundisha yeye darasani.
Na labda ameshuhudia mwalimu wake akihangaika kupambana na gharama za maisha wakati muuza mkaa akiwa na maisha ahueni zaidi. Yawezekana pia kushuhudia kuwa mwalimu huyo huyo ana madeni mengi tu, ikiwa ni pamoja na deni analodaiwa na muuza mkaa. Kwa mazingira kama haya si ajabu kuwa mtoto wa darasa la pili aamue kuuza mkaa atakapokuwa mtu mzima.
Na matukio ya namna hii, ya watoto kutohusisha elimu na maisha bora yanayoambatana na kipato cha kutosha, yapo mengi nchini.
Kijijini nimekutana na mwanafunzi ambaye amehitimu kidato cha nne na ambaye anafanya biashara ya kupika pombe za kienyeji akisubiri kupata nafasi ya kujiunga na jeshi.
Huyu hajafikia uamuzi wa kuacha kujiunga na jeshi ingawa kipato cha pombe kinamwingizia pesa nzuri. Angekuwa na mtaji wa kutosha biashara hiyo ingeweza kumwingizia zaidi ya shilingi laki moja kwa siku, pesa ambayo wasomi wengi wa ngazi ya juu hawawezi kuipata.
Msomi aliyeondoka kijijini kwenda kutafuta elimu akirudi kijijini na kukuta muuza mkaa na mpika pombe za kienyeji, mmoja kahitimu darasa la saba na mwingine kahitimu kidato cha nne, wote wakiwa na kipato zaidi yake, anaweza kuanza kuhoji sababu ya kutumia muda mrefu kusaka elimu.
Ni muhimu nisisitize kuwa, kuachilia mbali athari za kimazingira za biashara ya mkaa na athari nyingine zinazoweza kuhusishwa na biashara ya pombe, si nia yangu kujenga hoja kuwa hizi ni shughuli ambazo hazina maana. Ni shughuli ambazo zinakidhi mahitaji ya Watanzania waliyo wengi, hasa wale wanaoishi vijijini.
Yale madhumuni mapana kwa Taifa ya kusambaza elimu miongoni mwa raia wake bado yanabeba umuhimu ule ule wa enzi za Mwalimu Nyerere. Na ndiyo maana tumeshuhudia kwenye Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni kuwa vyama vyote vilivyoshiriki kwenye uchaguzi vilitoa ahadi mbalimbali za kuboresha elimu na kupambana na vikwazo dhidi ya elimu.
Vipaumbele kwenye elimu vinaweza kuwa vimebadilika, lakini umuhimu wa elimu kwa Taifa haujapunguka. Kwa sababu hiyo, pamoja na maswali anayoweza kujiuliza mwanafunzi mmoja mmoja kuhusu faida ya kukaa masomoni muda mrefu, elimu inabaki kuwa moja ya nguzo kuu za kuhakikishia Taifa lolote linajenga uwezo wa kusukuma mbele maendeleo.
Lakini ukweli unabaki kuwa uamuzi wa mwanafunzi mmoja mmoja unaweza kuathiri kwa kiasi fulani lengo la Taifa la kujenga kada ya wasomi katika nyanja mbalimbali za elimu. Na ndiyo maana upo umuhimu wa kupunguza vile vikwazo vinavyomsababisha mwanafunzi aone faida kubwa zaidi kwenye ujasiriamali wa mkaa kuliko kwenye kuongeza elimu yake.
Taifa la watu wasiokuwa na elimu siyo tu ni kikwazo kwa maendeleo yake, bali pia ni tishio kwa demokrasia na uhuru wa Taifa hilo.
Elimu ndogo kwa raia ni sawa na uwezo mdogo kwa raia wa kubaini, kuchambua, na kuhoji uamuzi wa serikali na viongozi ambao unaweza kugusa ustawi wa maisha yao na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Aidha, pamoja na kuwa elimu bora hutumika vibaya na imewezesha baadhi ya wasomi kupora rasilimali za nchi zao, Taifa la raia na viongozi walioelimika vizuri lina uwezo mkubwa zaidi wa kulinda rasilimali za Taifa hilo.
Mawakala wa wakoloni walifanikiwa kupora maeneo makubwa ya ardhi barani Afrika ambayo baadaye yaligeuzwa kuwa makoloni kutokana na mikataba ya udanganyifu iliyotiwa sahihi baina ya mawakala hao na watawala wa Kiafrika.
Watawala waliokuwa na uelewa mkubwa kidogo walipinga njama za wakoloni za kupora maeneo yao na baadhi yao walipigana vita dhidi ya wakoloni kulinda maeneo yao.