Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mkuu Shirika la ndege Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi amesema wameanzisha huduma ya kumtambua mteja ambae anafanya safari zake mara kwa mara kwa kutumia shirika hilo ambapo mteja huyo anaweza kukata tiketi ya daraja la uchumi na kupanda mpaka daraja la Biashara.
Aidha Matindi ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda lao lililopo katika Viwanja vya maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo ikiwemo ukataji wa tiketi na fursa zinazopatikana katika usafiri wa anga.
Matindi ameyasema hayo baada ya kutembelea katika banda lao, ambapo amesema zipo fursa nyingi wamekuwa wakizitoa kwa wateja wao ikiwemo huduma za ukataji wa tiketi na kulipa kidogo kidogo kwani huduma hiyo inamsaidia kupanga safari zake bila kuumia kwa kulipa gharama kubwa kwa wakati mmoja.
“Na sasa tumeanzisha huduma ya kumtambua mteja wetu ambae amekuwa anafanya safari zake mara kwa mara na mteja huyo anaweza kukata tiketi ya daraja la uchumi na kupanda mpaka daraja la Biashara. Yaani anakua anapata aina fulani za upendeleo kuchagua siti kupata huduma ya ziada ya mizigo lakini akiwa pia na pointi nyingi anaweza pia kupata tiketi ya bure.
“Hata hivyo nichukue fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara kutumia Ndege zetu katika kusafirisha biashara zao nje lakini pia shirika litawasaidia kuyafikia masoko mengi ya bidhaa zao kwa manufaa ya nchi lakini pia kwa manufaa yao binafsi,” ameongeza.
Akizungumzia ushiriki wao katika maonesho hayo, amesema kwa mwaka huu wamekuwa tofauti ambapo huduma zote zinazotolewa kwa wasafiri wa anga zimewekwa katika sehemu moja ambapo inamuwezesha mwananchi kuweza kujifunza lakini pia kuhudumiwa akiwa katika sehemu hiyo hiyo.