Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imeokoa wasafiri wanaotumia ndege nchini kwa kumaliza utaratibu wa kutoa huduma mbovu, ulioanzishwa na mashirika binafsi, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
ATCL imewafuta machozi Watanzania na wageni wanaotumia usafiri wa ndege nchini, kutokana na unyanyasaji mkubwa waliokuwa wakifanyiwa na Shirika la Fastjet kwa kiburi cha hali ya juu.
Fastjet waliodhani wametawala usafiri wa anga Tanzania milele, walifikia hatua msafiri anafika uwanja wa ndege anaambiwa amechelewa, wakati muda wa ndege kuondoka ukiwa bado kwa saa moja au zaidi na wakati mwingine analipa nauli kwa kutumia simu za mkononi baadaye anaambiwa fedha hazikufika na zinapotea jumla.
Wakati mwezi wa Desemba watu walikuwa wakipangishwa mstari katika ofisi za Fastjet kukata tiketi kwenda sehemu mbalimbali nchini katika Mtaa wa Samora, Dar es Salaam, mwezi huu ofisi za Fastjet kwa siku zinapokea wateja wasiozidi 20.
Katika kilichochukuliwa kuwa Fastjet ni wanyanyasaji wa hali ya juu katika usafiri wa anga, ukikata tiketi yao ndege ikikuacha au ukiwa na dharura fedha yote inapotea tofauti na utaratibu wa kimataifa wa biashara ya usafiri wa anga wakati mtu asipotokea hupigwa faini kidogo inayojulikama kama ‘no show’ charges.
Wakati Fastjet wakiendelea na utaratibu wa mteja kupoteza fedha yote aliyotoa akichelewa au kupata dharura, kwa ATCL wanafanya uungwana wa kuheshimu utaratibu wa kutoza faini ya ‘no show’, ambapo mteja asiposafiri anatozwa faini ya Sh 35,000 kisha tiketi yake inakuwa hai na kutumika tena.
Kwa suala la mizigo pia nalo ATCL imekata jeuri ya Fastjet ambayo kwa wafanyabiashara ya samaki Mwanza wanalaani kuwa Fastjet inawatoza Sh 22,500 kwa mtu aliyewahi kulipia begi au ndoo ya samaki saa 24 kabla ya safari na Sh 55,000 kwa ndoo au begi linalolipiwa saa ya kusafiri uwanjani, imeua biashara yao.
“Inakuwa kama unaadhibiwa kwa kusafiri. Tumeibwa mno fedha zetu na tunashukuru ujio wa ATCL,” alisema Salum Ali, aliyekuwa anasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza wiki iliyopita.
Taratibu mbovu ambazo bado zinatumiwa na Fastjet ni msafiri kutakiwa kukata tiketi mpya pale anaposhindwa kusafiri siku aliyotakiwa kusafiri, kutokana na sababu yoyote iwayo, kutotolewa kwa wakati taarifa za kuahirishwa safari za ndege na gharama za nauli kubadilika mara kwa mara ndani ya muda mfupi.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Injinia Ladislaus Matindi, ameieleza JAMHURI kuwa tiketi za shirika hilo zinabadilishika, lakini kwa tozo ndogo kama gharama ya kubadilishia na si kutoza nauli mpya wala kumtaka msafiri kuongeza pesa zaidi.
“Inategemea aina ya tiketi, kwa mfano daraja la juu (la biashara) kubadili tiketi ni bure kwa mara ya kwanza, lakini kama msafiri atahitaji kubadili tena atalipia gharama kidogo ya kubadilishia tiketi. Sisi tupo kwa lengo la kutoa huduma kwa Watanzania, huduma ambayo inamjali mnyonge na kupitia huduma hiyo nasi tunahesabika kuwa tunafanya biashara,” anasema Matindi.
Anasema ndege za ATCL zinatoa pia viburudisho kwa abiri wake ambavyo havitozwi pesa, tofauti na baadhi ya mashirika ya ndege.
Noel Yohana, aliyesafiri na ndege ya ATCL ya saa 10:00 jioni Desembba 20, 2016 kwenda Mwanza, anasema alichagua kusafiri na ATCL kutokana na unafuu wa nauli, na huduma nzuri zinazotolewa bure ndani ya ndege.
“Nilikata tiketi, nililipa Sh 305,000 kwenda Mwanza kwa ATCL, lakini siku hiyo hiyo kabla ya kukata tiketi ATCL nilianzia kampuni nyingine ya ndege (jina linahifadhiwa) nikaambiwa nauli ni Sh 354,000 ya kwenda Mwanza,” anasema Yohana.
Akizungumza na JAMHURI, Emmanuel Bashaija amesema “Mimi nasafiri kwenda Bukoba kwa nauli Ya Sh 325,000. Nashukuru kurejea kwa huduma za ATCL kwa sababu ndege nyingine bei zao ziko juu zaidi.”
Meneja Mkuu wa Shirika la Ndege la Fastjet, John Corse, anasema malalamiko ya baadhi ya wasafiri wanaotumia usafiri wa shirika hilo kutobadilishiwa tiketi zao dharura zinapotokea, wasafiri wanatakiwa kuzitambua na kuzikubali taratibu zinazotumiwa na shirika hilo katika kutoa huduma zake na si kulilinganisha na mashirika mengine.
“Taratibu za huduma zetu zote zipo katika tovuti yetu kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza. Mtu anapoamua kusafiri na ndege zetu maana yake amekubaliana na masharti yetu. Sisi hatubadilishi tiketi ya msafiri kwa sababu tunaamini tiketi ni mkataba tosha ambao unaonesha msafiri afike uwanjani masaa mawili kabla ya muda wa ndege kuondoka,” anasema Corse.
Akizungumzia suala la baadhi ya mashirika ya ndege kutotoa huduma ipasavyo kwa wateja wake, Msemaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), Ally Changwila, anasema Sheria ya Usafiri wa Anga ya Mwaka 2006 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2008 (Tanzania Civil Aviation Act 2008) inasema taarifa za kuahirishwa kwa safari ya ndege inatakiwa kutolewa siku mbili kabla.
“Sheria ipo wazi, kama shirika la ndege linapata dharura ya kuahirisha safari linatakiwa kutoa taarifa haraka na kama zitachelewa kuwafikia wateja wake, basi shirika husika linatakiwa kuhakikisha inapatikana ndege nyingine mbadala; la sivyo linawajibika kuwatafutia sehemu ya kupumzika iwapo wanatoka mbali, mfano hoteli, huku likifanya utaratibu wa kupata ndege nyingine.
“Kwa wale ambao wanatoka maeneo ya karibu na uwanja wa ndege, shirika husika linatakiwa kumrudishia gharama zote alizotumia kufika uwanjani huku likifanya taratibu za ndege nyingine,” anasema Changwila.
Kaimu Katibu wa Baraza la Watumiaji wa Usafiri wa Anga nchini, Debora Mligwa, anasema ATCL ni shirika ambalo halina migogoro na wateja wake tofauti na mashirika mengine ya ndege nchini.
Alipoulizwa ni shirika gani ambalo linaongoza kwa kulalamikiwa na watumiaji wa usafiri huo kwa miezi sita iliyopita, hakuweza kutoa jibu zaidi ya kusema;
“Hilo ni suala gumu, orodha ipo ila ninahitaji kukuamini sana kabla sijakupatia orodha hiyo maana ni masuala ya kibiashara na mashirika haya yapo katika ushindani. Kwa sasa siwezi na sidhani kama naweza kukupa maelezo zaidi juu ya suala hilo ila ninachoweza kukwambia kwa sasa ATCL hawana migogoro ikilinganishwa na mashirika mengine kwa siku za hivi karibuni,” anasema Mligwa.
Awali akizungumzia suala la utoaji wa huduma za mizigo na abiria (ground handling service) kuwa chini ya shirika la ndege nchini, Mkurugenzi wa ATCL Matindi anasema kwa sasa huduma hizo ziko chini ingawa ni gharama kubwa kuziendesha.
“Ground handling’ ni gharama kubwa sana. Tunajijenga taratibu baada ya kuanza upya. Wapo wanaosema ‘ground handling’ ikiendeshwa na ATCL tutakuwa na faida kubwa ila kwa uzoefu wangu hilo si suala rahisi. Kama shirika ukihitaji kufanya ‘ground handling’ ni laziama kwanza uwe na ndege nyingi na zenye safari nyingi za ndani na nje ya nchi kwa siku.
“Mashirika mengi ya ndege yanakuwa na ‘ground handling’ baada ya kujijenga vizuri tena baada ya kujihakikishia huduma bora za ndege zenyewe kitaifa na kimataifa. Tulikuwa na Dahaco lakini kulingana na mwenendo wa ATCL haikusaidia chochote. Kwa sasa tumelenga zaidi kuimarisha huduma ya usafiri. Hata hivyo, tumetangaza tenda kwa ajili ya kupata shirika litakalofanya ‘ground handling’ ambapo mashirika matano yameshajitokeza hadi sasa,” anasema Matindi.
Mwaka huu, Rais Magufuli amenunua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 zinazofanya safari sehemu mbalimbali nchini na kuongeza ufanisi wa shirika hilo. Ndege hizo zimeungana na ndege moja Dash 8 Q 300 iliyokuwapo yenye uwezo wa kubeba abiria 50.
Tanzania inapanga kununua ndege aina ya Boeing 787 Dash 8 Dreamliner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262, inayotarajiwa kuwasili nchini Juni 2018.
Ndege nyingine ambazo Tanzania itazinunua ni moja aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kuwasili Mwezi Juni 2017; ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018.
Hatua hizi za Rais Magufuli zinaifanya ATCL kuwa shirika la kiushindani katika biashara ya ndege, hali inayodhoofisha mashirika yaliyokuwa yanafanya udalali.
Kwa upande wa Shirika la Ndege la Precision Air, maafisa wao walipofuatwa kuzungumzia ubora wa huduma wanazotoa pale makao makuu Dar es Salaam, walisema Afisa Uhusiano yuko likizo hivyo hawana mtu wa kusema.