Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi amesema injini moja ya ndege ya kampuni hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya,ilipata hitilafu ya kupata joto na kusababisha moshi wa mafuta kuingia ndani ya ndege kupitia mfumo wa hewa.
Akitoa ufafanuzi Dar es Salaam,Matindi amesema hitilafu hiyo haikuwa na madhara na harufu hiyo iliyoingia ndani ya ndege ilidumu kwa dakika tano na kusababisha taharuki kwa abiria ambao hata hivyo, wahudumu wa ndege waliwatuliza.
Amesema tukuo hilo lilitokea Februari 24,mwaka huu, wakati ndege ya ATCL Airbus A220-300
yenye namba TC 106 iliyokuwa ikuruka kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya ikiwa na abiria 122 dakika 30 baada ya kuruka hitilafu hiyo ilitokea.
“Baada ya hitilafu hiyo kutokea marubani wa ndege hiyo walichukua hatua kwa kuzima injini hiyo moja na baada ya dakika tano harufu ya moshi huo ikakata na ndipo rubani kiongozi,Michael Lengaram akaamua kugeuza ndege na kuirudisha Dar es Salaam salama,”amesema Matindi.
Amesema wakati tukio linatokea ilikuwa ni dakika 30 zimepita tangu ndege hiyo iruke kutoka Dar es Salaam na ilikuwa imefika Hifadhi ya Taifa Mikumi,mkoani Morogoro.
Matindi alisema ndege hiyo ingeweza kuendelea na safari yake kwa kutumia injini moja, lakini rubani aliamua kuirudisha kwa usalama wa abiria na ndege hiyo.
Akizungumzia hitilafu hiyo na ukubwa wake, Mkuu wa Kitengo cha Usalama na Ubora wa kampuni hiyo,Emmanuel Tivai alisema tatizo lililotokea ni la kawaida na hushughulikiwa kwa kufuata taratibu zinazotambulika kitaifa na kimataifa.
“Kilichotokea ni hitilafu ya kawaida katika usafiri huu na huwa hatua zilizofanywa na wahudumu wa ndege wakiwemo marubani ndio sahihi na kama kuna uhitaji wa taarifa kama hiyo kutolewa kwa umma haizuiwi kufanya hivyo,”alisema Tivai.
Ameongeza kuwa baada ya marubani kuirudisha ndege salama, uongozi wa ATCL uliwatafutia ndege nyingine ambapo abiria 104 walisafiri na abiria 18 walibalilisha tarehe nyingine ya safari.