Na Andrew Chale, JamhuriMedia, Dar
WAZIRI wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amebainisha kuwa, Tanzania kupitia shirika lake la ndege (ATCL) linaenda kuwa na ndege zake mpya 16.
Prof. Mbarawa ameyasema hayo mapema jana Oktoba 2,2023, wakati wa kutangaza hafla ya mapokezi ya ndege mpya ya abiria aina ya Boeing B737-9MAX pamoja na uzinduzi wa ndege mbili aina ya CESSNA 172S itakayofanyika leo Oktoba 3,2023 majira ya kuanzia saa nne asubuhi katika kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar Es Salaam.
“Nitumie fursa hii kuutarifu umma wa Tanzania kuhusu ujio wa ndege
mpya ya abiria aina ya Boeing B737-9MAX pamoja na uzinduzi wa ndege
mbili za mafunzo aina ya Cessna 172S JNIA ambapo shamrashamra zinatarajiwa kuanza majira ya saa Nne asubuhi na watu wote wanakaribishwa.” amesema Prof. Mbarawa.
Ambapo amesema: “Mwaka 2016, Serikali ilichukua hatua za kuifufua ATCL kuanza kuinunulia ndege na kufanya mabadiliko ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi.
Hadi Septemba, 2023 ATCL imeshapokea ndege 12 mpya ambazo zimenunuliwa
na Serikali.
Ndege mbili kubwa aina ya B787-8 Dreamliner
ambazo zinauwezo wa kubeba abiria 262 kila moja, ndege nne za masafa yakati aina ya Airbus A220-300 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja, ndege tano za masafa mafupi aina ya D8 Q400 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na ndege kubwa ya mizigo aina ya B767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54.2.” Amesema Prof. Mbalawa.
Prof Mbarawa amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dkt, Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea
kuhahakikisha kuwa ATCL, inatoa huduma zenye kuhimili ushindani kwa kuanzisha safari za moja kwa moja kwenda kwenye
masoko ya kikanda na kimataifa na Julai, 2021 Serikali iliingia mikataba na Kampuni ya Boeing ya Marekani ya ununuzi wa ndege nne mpya zenye teknolojia ya kisasa.
“Ndege hizo ni ndege mbili za abiria za masafa ya kati aina ya B737-9MAX zenye uwezo wa kubeba abiria 181 kila moja, ndege
moja ya abiria ya masafa marefu aina ya B787-8 Dreamliner yenye uwezo
wa kubeba abiria 262 na ndege moja kubwa ya mizigo aina ya Boeing B767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54.
Ndege ya mizigo aina ya B767-300F
tayari ilishawasili na inaendelea kutoa huduma zake na ndege moja ya
masafa ya kati aina ya B737-9Max uundaji wake umekamilika na inatarajia
kuwasili nchini leo tarehe 03 Oktoba, 2023.
Aidha, Ndege mbili zinaendelea kuundwa ambapo zinatarajia kuwasili nchini mwezi Disemba, 2023 na mwezi Machi,
2024.” amesema Prof. Mbarawa.
Ambapo ameeleza kuwa,ndege ya abiria ya masafa ya kati aina ya B737-9MAX
inauwezo wa kubeba abiria 181 katika madaraja mawili ambapo daraja la
kawaida “economy class” ni abiria 165 na daraja la biashara (business class)
abiria 16, pia uwezo wa kubeba mzigo wa tani 6 na kuruka wastani wa masaa 8 bila kutua.” amesema Prof Mbalawa.
Prof Mbarawa amebainisha kuwa,kuwasili kwa ndege hiyo kutaifanya ATCL kuwa na ndege 13 mpya zilizonunuliwa kutoka na utekelezaji wa mpango mkakati wa Serikali
ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2016 na hivyo kuwa na ndege 14
zinazosimamiwa na ATCL katika uimarishaji wa wigo wa mtandao wa safari zake ndege kwa soko la ndani, kikanda na kimataifa.
Kwa sasa ATCL inahudumia vituo vya ndani vipatavyo 14 ambavyo ni Mwanza, Bukoba, Songea, Zanzibar, Katavi, Dar es Salaam, Iringa, Geita. Kigoma, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, na Tabora.
Pia, ATCL inahudumia vituo vya Kikanda na kimataifa ambavyo ni Entebbe-Uganda,
Nairobi-Kenya, Bujumbura-Burundi, Hahaya-Comoro, LubumbashiDRC, Ndola,Lusaka-Zambia,Harare-Zimbabwe.
Pia Johannesburg- Afrika Kusini, Mumbai-India, na Guangzhoa – China na Dubai.
Ujio B737-9MAX kutaiwezesha ATCL kuongeza vituo vya Pemba, Tanga, Mafia, Nachingwea na Musoma kwa mtandao wa safari za ndani. Pia itaongeza miruko ya safari za usiku kwa viwanja vya ndege ambavyo vina taa pamoja na kuanzisha safari za usiku katika viwanja vya ndege vya Dodoma na Songea ambavyo miiradi ya ufungaji wa taa za kuongozea taa imekamilika.”
Kwa upande wa mitandao wa safari nje,ATCL itaendelea kuongeza miruko ya kwenda Mumbai, India na Guangzhou, China huku ikianzisha safari mpya za Kinshasa, Goma,Dubai, Muscat, na Lagos.
Prof Mbarawa amesena sambamba na uimarishaji wa ATCL tangu mwaka 2016 Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa ndege zinazonunuliwa zinakuwa na wataalamu wa ndani wa kuzihudumia ili kupunguza gharama za kutumia wataalam wa nje hususani Marubani na wahandisi ndege.
Ambapo hatua hizo ni pamoja na kukijengea uwezo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kukijengea majengo, ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia, ununuzi wa ndege za mafunzo, na kuweka
miundombinu wezeshi kwa ajili kutoa Kozi za muda mrefu za Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege (Degree and Diploma); Kozi za kutoa mafunzo ya wahudumu wa Ndani ya Ndege (Cabin Crew) na Uendeshaji wa Safari za Ndeg pamoja na Ndaki ya Chuo cha Urubani (Flight Crew).
“Hadi sasa chuo kinatoa mafunzo ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege, Uendeshaji
wa Safari za Ndege pamoja na Uhudumu wa Ndani ya Ndege kwa Ithibati za TCAA.
Vilevile, Chuo kinatoa mafunzo ya Air Fares and Ticketing, Airport Operations Fundamentals, Airline Marketing pamoja na Airline Customer Service kwa Ithibati ya IATA.
Prof Mbarawa amesema,Mwaka 2021 Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliiwezesha NIT kuingia mkataba wa ununuzi wa. dege mbili za mafunzo ya Urubani aina ya Cessna 172 Skyhawk zinazotumia injini moja kila ndege toka Kampuni ya Textron Aviation Inc ya
Marekani.
Ndege hizo ziliwasili nchini mwezi Januari, 2023 zikiwa zjmevunjwa ambapo kwa sasa zimekamilika kuundwa na zipo tayari
kuzinduliwa kwa ajili ya kuanza kutoa rasmi mafunzo ya Urubani. Ndege hizo
kila moja inauwezo wa kubeba watu wanne (4) ikijumuisha rubani, na zinatumia mfumo wa kisasa wa uendeshaji (glass cockpit) ambao unamuwezesha rubani kuratibu taarifa kiurahisi na hivyo kuongeza umakini
na usalama wakati wa urushaji ndege.
Ndege hizo zitatumiwa na NIT kutoa mafunzo ya Urubani kwa daraja la awali (PPL) ambayo yatachukua miezi 6 kwa ada ya TZS 21,000,000 na daraja la biashara (CPL) ambayo yatachukua miezi 12 kwa ada ya TZS 53,800,000/=) na kufanya jumla ya ada kwa mafunzo yote kuwa TZS 74,800,000 ambayo ni ndogo ukilinganishwa na gharama za kusoma mafunzo haya nje ya nchi ambayo kwa wastani hugharimu TZS 300,000,000/=.” Amesema Prof Mbarawa,
Na kuongeza: Kwa kuwa ndege moja inaweza kutumika kufundishia wastani wa wanafunzi watano (5), Chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 10 kwa mkupuo mmoja.
Katika kuongeza ufanisi wa mafunzo ya urubani mwezi Juni, 2023 Serikali
ya Awamu ya Sita imewezesha NIT kuingia mkataba na ununuzi wa ndege moja ya mafunzo ya injini mbili aina ya Beechcraft Baron G58 toka Kampuni ya Textron Aviation Inc. ya Marekani. Ndege hiyo inatarajia kuwasili katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025. Kuwasili kwa ndege hii kutawezesha wahitimu wa kozi ya CPL kufanya mafunzo ya Multi-Engine Class Rating na Multi-Engine Instrument Rating hivyo kukidhi vigezo vya kuingia kwenye ajira.