KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL), imeingia makubaliano ya kupeleka marubani wake kufundisha na kusimamia ndege mpya za Airbus A220 za Kampuni ya Ndege ya Ibom nchini Nigeria.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema hayo jana Dar es Salaam na kuongeza kuwa
ATCL imetoa marubani wake waandamizi wawili ambao watakuwa na jukumu la kuwafundisha kwa vitendo marubani na walimu wa marubani wa Ibom Air kwa muda wa miezi sita.
“Marubani wa ATCL watakuwa na jukumu la kufundisha na kusimamia mafunzo kwa vitendo hadi watakapojiridhisha marubani wanafunzi na walimu wao wamefikia viwango vinavyo
takiwa kurusha ndege hizo,” alisema.
Aidha, Kampuni ya Ibom Air itailipa ATCL gharama za mafunzo hayo kwa mujibu wa mkataba kwa kipindi chote cha makubaliano.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya ATCL kuonesha uzoefu wa muda mrefu wa kumiliki ndege za Airbus A220-300 na pia kuridhishwa na kiwango cha umahiri wa marubani wa ATCL.
Mafunzo hayo yanalenga kujenga uwezo kwa marubani wa Ibom Air watakaorusha ndege za Airbus A220, ambazo ATCL ina uzoefu wa miaka mingi wa kumiliki ukilinganisha na Ibom Air ambao ndio wanaanza kutumia ndege za aina hiyo.
ATCL ina zaidi ya marubani 100, inamiliki ndege aina ya Boeing B787-8, B737 MAX 9, B767-300F, Airbus A220-300 pamoja na Dehaviland Q400 na Q300.