Mwanzoni mwa mwezi Desemba Shirika lijulikanalo kama Christ for All Nations (Kristo kwa Mataifa Yote) lenye makao yake makuu jijini Orlando, Florida nchini Marekani lilitangaza kuwa Mchungaji Reinhard Bonnke amefariki dunia. 

Mchungaji Bonnke atakumbukwa kwa kazi yake kubwa ya kueneza neno la Mungu na kufanya maombezi ya kuponya watu na kuwasaidia katika shida zao mbalimbali kote barani Afrika.

Alikuwa ni mchungaji ambaye kazi yake iliwagusa wengi kwa sababu, kwa imani yao, wengi waliokwenda kwake wakiwa na shida mbalimbali waliona zimetatuliwa. Hivyo akajizolea uaminifu na umaarufu miongoni mwa watu wengi.

Si tu kwa walio na shida za moja kwa moja kama vile magonjwa ndio waliona zaidi kazi zake, bali hata wale ambao walikuwa na shida za kiimani nao walipata kimbilio kwake, kwa sababu mahubiri yake yaliwafanya wengi wajione kuwa wanaungana na Muumba wao kiimani.

Mchungaji Bonnke alifariki dunia Desemba 7, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 79. Bonnke alikuwa anamiliki nyumba Rivira Beach na Boynton Beach, Florida. Hata hivyo, shirika hilo ambalo yeye ndiye alilianzisha, halikusema kifo chake kimetokana na nini.

Ingawa Mchungaji Bonnke alifanya kazi ya kuhubiri na kuombea watu duninai kote lakini kazi zake zilijidhihirisha zaidi barani Afrika ambako mikutano yake ilikuwa ikivunja rekodi kwa kuhudhuriwa na watu wengi mno. 

Huko ndiko ambako uwezo wake wa kuwavuta watu kiimani ulipoonekana sana, kiasi cha jina lake likawa ni moja kati ya watu maarufu ambao watu wengi walikuwa wanawafahamu.

Wakati huo Bonnke alisema lengo lake kubwa la kuifanya kazi hiyo ni kuhaikisha kuwa anawaleta watu wote kwa Kristo.

“Yeye (Kristo) anazungumzia watu wote, hazungumzii asilimia fulani ya watu,” ilikuwa ni moja ya kauli maarufu za Bonnke wakati akimzungumzia Kristo katika mahojiano aliyoyafanya mwaka 2014. “Nitalenga shabaha kuelekea kwenye mwezi ili nipate faida kubwa.”

Rekodi zinaonyesha kuwa mkutano wake uliowahi kukusanya watu wengi ulifanyika katika miaka ya mwanzo ya 1990 jijini Lagos, nchini Nigeria. Makadirio ya shirika lake linaonyesha kuwa mkutano huo ulihudhuriwa na watu milioni 1.6. Baadhi ya watu wanapingana na idadi hiyo lakini kila mmoja anakubali kuwa mkutano huo ulikuwa na watu wengi ajabu!

Ni jambo la bahati mbaya kwamba kutokana na msongamano wa watu, watu walikanyagana na kusababisha vifo vya watu 17. Bonnke mwenyewe alisema baadaye kuwa ujumbe wake una maana ya kipekee kwa Waafrika.

Habari yake kubwa ambayo ilivuta hisia za watu wengi ilimhusu mtu mmoja aliyeitwa Daniel Ekechukwu, anayetajwa kuwa ni Lazaro wa kizazi cha sasa. Baada ya ajali ya gari mke wa mtu huyo aliuchkua mwili wa mume wake ambaye inaaminika kuwa alikuwa amefariki dunia na kuupeleka katika kanisa ambalo Bonnke alikuwa anahubiri. Wakati wa ibada, Bonnke anasema alishuhudia Ekechukwu akifufuka katika wafu.

Wakati watu wakishangaa kwa kauli hiyo, Bonnke mwenyewe akasisitiza kwa kusema kuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa yeye kushuhudia watu wakifufuka. “Kuna matukio mengine ambayo watu waliinuka kutoka katika mauti,” alisema na kuongeza:

“Haya ni mambo halisi lakini kuna baadhi ya watu wanaonekana kutoamini, sawa, Mungu awasamehe.”

Mmoja wa wachungaji wa Bonnke walioulizwa baadaye kuhusiana na suala hilo alisema hata yeye haelewi kwa undani ukweli kuhusu mtu kufufuka. Mchungaji huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa hata habari kuhusu maelfu ya watu kuponywa magonjwa yao na mchungaji huyo, wakiwamo wagonjwa wa ukimwi, saratani na wale waliopooza, nalo ni suala linalotia shaka. Alibainisha kuwa anavyoelewa yeye hakuna nguvu zozote za ajabu ambazo Bonnke anazo isipokuwa uwezo wake wa kufanya miujiza ndilo jambo linalowavuta watu wengi kwake

Maisha ya Bonnke

Bonnke alizaliwa Aprili 19, 1940, Konigsberg nchini Urusi. Alikuwa ni mtoto wa pili katika familia iliyokuwa na watoto sita ambao waliongozwa na mama yao hadi Denmark wakati walipokimbia ili kujisalimisha wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Baba yake alikuwa ni askari katika jeshi la Ujerumani kabla hajaacha kazi hiyo na kuwa mchungaji. Hata hivyo, aliwakataza watoto wake kufuata kile alichokifanya yeye – kuingia katika masuala ya kueneza neno la Mungu.

Akisimulia maisha yake, Bonnke anasema alikuwa na umri wa miaka kumi tu wakati alipoisikia sauti ya Mungu ikimuita kwamba aende kuhubiri barani Afrika. Pia anasema alikuwa bado kijana mdogo tu pale alipoanza kunena kwa lugha, kwanza kuhubiri katika kona ya mtaa aliokuwa anaishi kabla ya kuanza kuwabadili watu katika imani.

Alianza kufanya kazi kama mmisionari nchini Lesotho mwaka 1967 na akaanzisha shirika lake la Christ for All Nations miaka saba baadaye.

Jinsi miaka ilivyozidi kusonga na watu wanaomfuata kuongezeka, Bonnke akageuka kuwa mtu mzuri sana kwenye kuchangisha fedha. Kwa kutumia kipaji na uwezo wake, aliweza kukusanya mamilioni ya dola za Marekani, hivyo kuweza kuandaa mikutano mingi sehemu mbalimbali duniani.

Katika mahubiri yake hakuwa mtu wa kutoa ujumbe wa kuwatisha watu au kuwakemea. Kila mara alikuwa akiongea kwa sauti ya chini, wakati mwingine inayokaribia kuwa mnong’ono, akitoa ujumbe ule ule, kuwataka watu waache kumfuata shetani na kumgeukia Mungu.

Katika kila mkutano wake, mwishoni aliwaita watu ambao walikuwa tayari kumpokea Mungu kusogea mbele kwenye jukwaa na hilo liliitikiwa kwa watu wengi waliokuwa wakitetemeka, kulia, kucheza na kupiga mayowe kujitokeza huku wakisifu umuhimu wa uamuzi wao.

Kwa mujibu wa Bonnke na shirika lake, takriban watu milioni 79 walifanya uamuzi kama huo katika miaka yote ambayo Bonnke alifanya mahubiri maeneo mbalimbali duniani. Baadaye, aliamua kutumia njia mpya ya kuhubiri kwa kufanya hivyo kupitia televisheni.

Mahubiri ya Bonnke yalijikita katika falsafa ya mtu kuzawadiwa pale anapofanya uamuzi wa kumfuata Mungu. Bonnke aliwaambia wafuasi wake na watu wengine waliomsikiliza kuwa uamuzi wa kuacha kumfuata shetani na kumgeukia Mungu unaambatana na zawadi ya afya njema na utajiri.

Imani yake hiyo ni sawa na imani ya wahubiri wengine wawili, Benny Hinn na Kenneth Copeland. Wote watatu waliongoza mashirika ambayo yaliwafanya wawe matajiri wakubwa, ingawa mara zote Bonnke alikuwa hataki kujibu maswali kuhusiana na maisha yake binafsi.

Maisha binafsi

Pamoja na kumiliki jumba la kifahari lenye thamani ya dola milioni tatu za Marekani huko Ritz-Carlton, Bonnke na mke wake Anni, walinunua eneo jingine lenye ukubwa wa futi za mraba 5,900 kwa thamani ya dola milioni 1.45 za Marekani mapema mwaka huu, kwa mujibu wa taarifa ya Jimbo la Palm Beach. Mara zote Bonnke alisisitiza kuwa alijifunza kutojiona mwenye hatia kutokana na raha anazozipata.

“Baraka ni baraka. Nimelazimika kujifunza mambo mengi kwa miaka mingi na ninamshukuru Mungu kwa alichonipatia,” Bonnke aliwahi kusema.

Ingawa Bonnke alibakia kuwa kiongozi wa juu katika shirika lake, lakini mwaka 2010 Mchungaji Daniel Kolenda alichaguliwa kuwa rais wa shirika hilo na kuwa mmoja wa wahubiri waliofanya kazi kubwa sana, hasa safari za kuhubiri maeneo mbalimbali duniani.

Pamoja na mke wake, Bonnke ameacha pia watoto watatu wakubwa; Kai-Uwe, Gabriele na Susanne na wajukuu wanane.

Maajabu Mwanza

Kama tulivyoona, Mchunagji Kolenda alichukua nafasi ya urais kwenye Shirika la Christ for All Nations mwaka 2010 na kuwa nguzo muhimu katika kazi za kuhubiri, hasa barani Afrika ambako Bonnke na shirika lake tayari walikuwa wameshajijengea umaarufu.

Katika maeneo ambayo Kolenda na timu yake walitembelea mara kwa mara ni Tanzania. Na hapa nchini maeneo ambayo walikuwa wanakwenda mara kwa mara walipozuru ni Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam.

Juni 2016, Kolenda na timu yake walikuwa wanafanya mahubiri jijini Mwanza. Katika andiko aliloliweka Juni 25, 2016, Kolenda anaandika maajabu ambayo aliyaona siku hiyo.

Anaandika kuwa asubuhi ya siku hiyo mganga wa jadi alileta ndumba na vibuyu vya mababu zake ili vichomwe moto. 

Kabla ya kuchoma moto vitu hivyo, mchungaji wa eneo hilo alifanya maombi na wakati wa maombi mganga huyo alianza kuonyesha dalili za kuwa na mapepo. Baada ya kuona hivyo, maombi yaliongezwa na kufanikiwa kuyaondoa kabisa mapepo hayo. Mtu huyo baadaye aliamua kumfuata Mungu.

Kolenda anasema hivyo ndivyo siku ilivyoanza na jambo la kushangaza ni kuwa katika mahubiri ya jioni, vifaa vingi sana vya uganga vililetwa na watu wengi ili vichomwe moto baada ya watu hao kuamua kuachana na nia zao za maisha ya kumwabudu shetani na kuamua kumgeukia Mungu.

Kolenda anasema kuwa hayo yalikuwa maajabu, kwani jinsi mahubiri yalivyokuwa yanaendelea na ndivyo jinsi ambavyo watu wengi walimiminika wakiwa na vifaa vyao vya uchawi ili viharibiwe.

Anaongeza kuwa asubuhi ya siku hiyo baada ya Peter Vandenberg kumaliza mahubiri, yeye Kolenda hakuwa na nguvu za kutoa ujumbe kutokana na uchovu. Lakini watu walikuwa na njaa sana na hali ilikuwa kana kwamba walikuwa wanajaribu kuzuia bwawa kubwa la maji lisipasuke. Aliamua kuweka kipaza sauti chini na nguvu ya Mungu ikaanza kusambaa na kuwawezesha kuwabatiza watu wengi ajabu.

Katika mahubiri ya usiku maajabu yakaendelea. Watu wengi wakatolewa mapepo na wakaanza kunena kwa lugha mbalimbali, lakini tukio kubwa lilimhusisha msichana ambaye mwili wake ulikuwa na majipu yaliyodumu kwa miaka mitatu lakini aliponywa kwa maombezi siku hiyo.

Pia siku hiyo usiku mwanamke mmoja akatoa ushuhuda akisema kuwa alikuwa kilema lakini akapata uwezo wa kutembea tena. Lakini Kolenda alipomuuliza maswali, ilibainika pia kuwa mwanamke huyo alikuwa pia bubu na hakuweza kuzungumza. 

Kolenda alifanya maombi kwa ajili yake palepale jukwaani na mwanamke huyo akaruhusiwa kurejea nyumbani. Siku iliyofuata, mwanamke huyo alifika tena kwenye mkutano akiwa anaweza kuzungumza mwenyewe kwa mara ya kwanza!

Pia alikuwepo mwanamke mwenye uvimbe mkubwa tumboni ambao ulikuwa unamfanya ashindwe kutembea vizuri na kumsababishia maumivu makali. Baada ya kufanyiwa maombi, uvimbe huo uliondoka na maumivu yakaisha!

Koleda akakumbusha kuwa miaka 20 iliyopita walikuwa Mwanza na walikutana na mwanamke aliyekuwa anaugua ukimwi akiwa katika hali mbaya sana. Reinhard Bonnke akamfanyia maombi na kuulaani ugonjwa huo. Mara moja mwanamke huyo akaona nguvu ya Mungu ikishuka mwilini mwake na aliporudi kwa madaktari siku chache baadaye akaambiwa kuwa hana maambukizi ya HIV.

Kolenda anasema miaka 20 baadaye, mwanamke huyo aliwatembelea jioni kwenye mkutano wao na kutoa ushuhuda wa kile kilichomtokea baada ya kuombewa na Bonnke miaka 20 iliyopita.

Kolenda anasema wapo watu ambao wanabisha kuwa hakuna miujiza na kuwa kinachowatokea watu wanapoombewa kinatokana na mihemko na matumizi ya nguvu za ajabu. 

Lakini anasema tukio hilo limethibitisha kuwa miujiza inatokea kweli, maana kama mwanamke huyo asingekuwa ameponywa asingeweza kuishi na ukimwi kwa miaka 20 katika kipindi ambacho dawa za kufubaza virusi vya ukimwi zilikuwa hazijaanza kutolewa.