Stanslaus Mlungu

Stanslaus Mlungu (78), aliyekuwa mfanyakazi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na kustaafu kazi Desemba 31, 1991 kutokana na matatizo ya kiafya, amelalamika kwamba ameibwa fedha zake za pensheni na watumishi wa Mfuko wa Pensheni wa PPF mwaka 1992.
Mlungu amesema baada ya kustaafu kazi akiwa na nafasi ya Mtunza Stoo (Storekeeper) katika kituo cha Sumbawanga kwa sababu za kiafya, amefuatilia mafao yake Makao Makuu ya PPF, Jijini Dar es Salaam bila mafanikio yoyote akiambulia ahadi za njoo kesho, wiki ijayo na usumbufu mwingine.
Amesema mara ya mwisho aliambiwa kwamba hundi yake ya malipo ya mkupuo namba 535902 ikiwa na Sh 168,866.75 iliyoandaliwa Aprili 16, 1992 kwa jina la Stanslaus Andrea Mlungu, inaoneka ilikuwa ya wazi na kupita benki siku hiyo hiyo na fedha hizo kuchukuliwa na mnufaika ambaye si yeye.
Kumbukumbu za malipo zinaonesha aliyelipwa pensheni ni Juma Mohammed na si Mlungu na kwamba hiyo ilikuwa mbinu ya baadhi ya wafanyakazi wa mfuko wa PPF kumwibia mafao yake.


Amesema kutokana na wizi huo aliogundua baada ya kumwomba mfanyakazi mmoja amwoneshe faili lake na kumweleza wazi kuwa anasumbuliwa bila sababu kwani waliochukua fedha hizo ni wafanyakazi wa mfuko huo.
“Baada ya kugundua wameniibia mafao yangu mwaka 2003 niliwaomba wanilipe haki yangu sawa na maagizo yaliyotolewa na wanasheria wa Serikali kupitia barua yangu ya Juni 1, mwaka jana, yenye kumbukumbu namba SAKM/WFM/MADAI/016/02 lakini wakaendelea kukaidi.
Niliwaeleza kwamba wanilipe kwa kufuata sheria namba 14 ya mwaka 1978, kifungu cha 44 ambacho kiko mahsusi kwa ajili ya kumwadhibu aliyechelewesha malipo ya mstaafu bila sababu za msingi bado wamekuwa wakinizungusha hadi sasa,” amesema Mlungu.


Katika kikao cha kujadili malalamiko ya Mlungu kuhusiana mkokotoo wa mafao yake kwa njia ya riba ya kudunduliza (Compound Interest) kilichofanyika Mei 27, mwaka jana chini ya Eligius Mwankenja kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, mlalamikaji ametaka PPF wamlipe mafao kwa njia hiyo kuanzia mwaka 1991 hadi atakapolipwa.
Madai yake mengine ni kulipwa gharama za usumbufu kwa upande wa chakula jumla ya Sh 24,180,000 kuanzia mwaka 1991 ikiwa ni Sh 155,000 matumizi yake kwa mwezi na gharama za malazi Sh 4,680,000 kwa miaka 13 na jumla ya madai yake yote ikiwa Sh 28,860,000 pia kurejeshwa kwenye malipo ya pensheni ya kila mwezi.


Hata hivyo, PPF walieleza kuwa hawahusiki na ucheleweshaji wa malipo ya Mlungu na kwamba waliridhia alipwe kiasi cha Sh milioni moja, lakini Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii iliagiza kiasi hicho kiongezwe na kuwa Sh milinioni 1.5, jambo ambalo halitoi haki upande wake.
Mlungu amesisitiza kuwa PPF ndiyo waliohusika na fedha hizo walizoamua kumlipa mtu mwingine wanayemfahamu wao kwa makusudi yao na hawezi kukwepa kuhusika na kumsababishia usumbufu wa muda mrefu huku akishindwa hata kulipa kodi ya pango la nyumba na sasa anaishi kwa kulala kwenye barazani.
Amesema kutokana na ukokotoaji wa kutumia riba ya kudunduliza kwa mujibu wa sheria namba 14 ya mwaka 1978 kwa kutumia asilimia 12 tangu mwaka 1991 alipostaafu hadi sasa, lakini kinachofanyika ni ujanja wa kujumlisha michango yake ya kila mwezi jambo analitafsiri kama dhuluma.
“Angalia wanachoita kukokotoa wanapiga hesabu zao kwa asilimia 5, 6, 8,10 na 12; huu ni ujanja mtupu! Kwa nini hawa PPF wamekuwa wasumbufu namna hii? Wameiba haki zangu na kunizungusha kwa muda mrefu sana wakati madai yangu yako wazi namna hii,” ameeleza.
Pamoja na kutokubaliana na kiwango kidogo cha mafao yake anachodai kushinikizwa na PPF, Mlungu amefikisha malalamiko yake sehemu mbalimbali ikiwamo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango lakini hakuna ufumbuzi wa madai yake hadi sasa.


Baada kushindikana ufumbuzi wa madai yake, alimwandikia barua Rais John Magufuli akieleza kucheleweshwa kwa utatuzi wa malalamiko yake na uongozi wa PPF kuhusu mkokotoo wa riba ya kudunduliza kwa zaidi ya miaka 14 sasa.
Amemwomba Rais Magufuli kuingilia kati suala hilo, kwani tangu mwaka 2003 alipoanza kufuatilia mafao yake na malimbikizo baada ya kustaafu na kubaini kuwa alilipwa mtu mwingine, amekuwa akizungushwa na maofisa wa PPF licha ya kwamba walikubali kuhusika na kosa hilo na pia kuandaa malipo yake pamoja na riba.


Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alielekeza kuwa alipwe kwa mujibu wa Sheria namba 44 ya mwaka 1978 ambayo ndiyo inayopaswa kutumika katika ukokotoaji lakini mfuko huo umekaidi.
“Mimi ni mzee wa miaka 77 sasa, tangu nije hapa kufuatilia madai yangu kutoka Sumbawanga mwaka 2003 hadi sasa, nimekuwa nalala nje nikisaidiwa na wasamaria wema; napangishiwa chumba na kodi ikiisha nafukuzwa nalala nje, sina chakula zaidi ya kuombaomba kwa watu kama mwendawazimu, naona aibu sana kuishi katika hali hii miaka hii yote nikiwa na akili timamu nikiteseka kwa ajili ya uzembe wa mtu mmoja.


Zaidi ya hayo, nimeingia kwenye madeni ili niweze kujikimu, naumwa mifupa, uvimbe mkubwa mkononi na sina pesa ya matibabu ni mateso matupu. Gharama zinakuwa kubwa pale wao wanapochelewa kunilipa ili niondoke, na hilo sio kosa langu mimi,” inaeleza sehemu ya barua yake hiyo yenye kumbukumbu namba SAK/WFM/MADAI/016/03 ya Septemba 9 mwaka jana.
Pamoja na madai yake hayo aliyoyaeleza katika sehemu ya barua yake kwa Rais akimwomba amsaidie apate haki yake ambayo ameendelea kuisotea kwa muda mrefu bila mafanikio yoyote. Septemba 23 mwaka jana, Wizara ya Fedha na Mipango ilimwandikia barua akitakiwa kuwasilisha katika Mfuko wa Pensheni wa PPF taarifa zake za kibenki kwa ajili ya kurejeshwa kwenye payroll ili aweze kulipwa pensheni yake ya kila mwezi kwa mujibu wa sheria.


Pia iliagiza alipwe malimbikizo yake yote ya mafao na pensheni anayostahili ambayo yalikokotolewa na kukubaliwa katika vikao vya pamoja yanayofikia Sh 6,488,399 na kwamba kiasi hicho cha mafao kilikubaliwa na pande zote PPF na Mlungu ambacho kilikokotolewa hadi Juni, mwaka jana.
“Madai yako yanayohusu riba katika malimbikizo ya mafao na pensheni pamoja na suala la madai ya kulipwa usumbufu wa Sh milioni 28 tutaomba lisubiri kwanza maamuzi. Utajulishwa hatima ya madai haya mengine mara baada ya Wizara ya Fedha na Mipango kupokea ushauri wake kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” imeeleza sehemu ya barua hiyo ya Wizara ya Fedha na Mipango yenye kumbukumbu namba CAN. 406/415/01 ya Septemba 23, mwaka jana iliyosainiwa na Eligius Mwankenja.


Pamoja na uamuzi huo uliotolewa yeye anachopingana na PPF ni kutumia sheria ya mwaka 2002 ambayo haikufuta haki za wale waliokuwa wanatawaliwa na sheria namba 14 ya mwaka 1978 ambayo yeye ni mhusika.
Amesema bado anaamini kuwa yuko sahihi kwa tafsri ya kulipwa malimbikizo ya pensheni kuanzia mwaka 1991 hadi sasa kwa mkokotoo wa kudunduliza ingawa sheria hiyo inataja kiwango cha asilimia 5 ya riba ya limbikizo lakini lazima iwepo tathmini ya riba na fedha kati ya mwaka 1991 hadi sasa.
Kwa mujibu wa sheria hiyo kwa kuzingatia kifungu cha 44, malimbikizo ya Sh 6,411,588.20 ndiyo yanayopaswa kukokotolewa kwa riba limbikizo kuanzia mwaka 1991 kwani bado PPF wameendelea kuhodhi fedha hizo.
Meneja Mkuu wa Pensheni wa PPF, John Mwalisu, amelieleza JAMHURI kuwa Mlungu alilipwa mafao yake ya mkupuo Machi 1990 lakini bado aliendelea na kazi hadi mwaka 1991 alipostaafu kazi kwa sababu za kiafya.
“Tulimlipa lump sum (kwa mkupuo) na pensheni zake za kila mwezi kuanzia Aprili 1990 na Machi 1990 alichukua nusu ya malipo yake hayo ya mkupuo kwa barua yake mwenyewe na mwaka 1992 tulimaliza kumlipa.


Ugomvi uliibuka mwaka 2003 baada ya tangazo la Serikali la kutaka watumishi wote wa Serikali walipwe pensheni zao na pia warudishwe kwenye payroll na yeye alikuwa miongoni mwa watu waliotakiwa kuingizwa kwenye utaratibu huo.
Tuna mafaili matano makubwa ya mzee Mlungu yenye kumbukumbu zake na SSRA walisema arudishwe kwenye malipo ya pensheni ya kila mwezi na tumefanya hivyo lakini ameshindwa kutupa ushirikiano wake kwa kutupa akaunti yake ya benki ili tumpatie fedha zake,” amesema Mwalisu.
Amesema walifanya vikao na wadau wote akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuelewa vizuri suala hilo lakini amekuwa akigeuka na kuanzisha madai yake upya. Hata hivyo, pamoja na compound interest fedha zake hazifiki hata milioni nne na hizo haziko kisheria.
Akionesha faili kubwa lililokuwa na nyaraka mbalimbali za Mlungu, amesema Februari 27, 2003 aliomba kulipwa pensheni ya kila mwezi na alianza kupatiwa matibabu mwaka 1975 na maombi yake ya kulipwa sh milioni 68 bila utaratibu hiyo haikubaliki.


Hata hivyo, ameongeza kuwa kifungu namba 44 anachotaka kitumike katika kukokotoa madai yake kilifutwa na SSRA na badala yake asilimia 5 ndiyo iliyokubaliwa na Mwanasheria Mkuu, lakini pamoja na kumwandalia mafao yake hajaripoti kusaini hundi yake.
Mwalisu amesema barua ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Novemba 5, 2010 yenye kumbukumbu namba J/P/100/5/20 iliyohusu riba ya kudunduliza, iliagiza itumike asilimia 5 baada ya kikao kilichowahusisha wadau wote.
Pia katika barua Wizara ya Fedha ya Septemba 23, 2016 yenye kumbukumbu namba CAN.406/415/01 uamuzi uliotolewa ni kwamba alipwe pensheni yake ya kila mwezi kwa mujibu wa sheria.
Amesema ilielekezwa kuwa alipwe mafao yake yote ya pensheni anayostahili yanayofikia sh 6,488,399 kiasi kilichokubaliwa kwa pande zote akiwemo mdai na PPF.


Mlungu amekanusha kwamba hakustaafu na kulipwa mafao yake kwa mkupuo na pensheni ya kila mwezi kama anavyodai Mwalisu na hadi sasa hakuna alicholipwa.
Kuhusu kuibwa kwa pensheni yake amesema wafanyakazi wa PPF walichukua malipo yake na anaelezwa kuwa wahusika hao wako nje ya nchi.
Afisa uhusiano wa SSRA, Sarah Kipande, amesema malalamiko ya mwanachama huyo yanapaswa kuwasilishwa katika mamlaka hiyo na iwapo aliibwa mafao yake kwa kulipwa mtu mwingine ni kosa kisheria.