Askofu Mkuu wa York, Stephen Cottrell anakabiliwa na wito wa kujiuzulu kwa kushindwa kushughulikia kesi ya unyanyasaji wa kingono, siku chache kabla ya kuchukua mamlaka ya muda ya Kanisa la England.
Uchunguzi wa BBC unaonyesha, akiwa Askofu wa Chelmsford, Cottrell alimwacha kasisi David Tudor kusalia katika dayosisi hiyo licha ya kujua kuwa alikuwa amezuiwa na Kanisa kuwa peke yake na watoto na alilipa fidia kwa mwathiriwa wa unyanyasaji wa kingono.
Msemaji wa Cottrell anasema alikuwa katika “hali mbaya” na hakuwa na uwezo wa kisheria wa kumfukuza kasisi huyo. Tudor alipigwa marufuku miezi miwili tu iliyopita baada ya kukiri unyanyasaji wa kingono yanayohusiana na wasichana wawili.
Hata hivyo, Askofu wa Newcastle, Mchungaji Helen-Ann Hartley anasema Cottrell angeweza kufanya zaidi na anapaswa kujiuzulu kama askofu mkuu.
Mwanamke ambaye alilipwa fidia ya pauni 10,000 na Tudor kwa madai ya kumnyanyasa kingono alipokuwa mtoto anasema kushindwa kwa Cottrell kuchukua hatua alipoambiwa kunamaanisha “ondoke Kanisani.”
Wito wa kumtaka Askofu Mkuu Cottrell ajiuzulu unakuja wakati wa msukosuko katika Kanisa la Engaland kufuatia ripoti ya kusikitisha ya wakili John Smyth kuhusu jinsi lilivyoficha unyanyasaji mkubwa wa kingono .