Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro , Jacob Ole Mameo  amewataka wanawake wa Umoja wa Jumuiya ya Kikristu Tanzania (CCT) kutumia nguvu waliyonayo kukemea wanaobeza jitihada zinazofanywa na baadhi ya wanawake walio katika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa dini na serikali.

Askofu Mameo ametoa wito huo mkoani Morogoro wakati akifungua Kongamano la Wanawake CCT la maombi lenye ujumbe ‘haki huinua taifa’.

Mameo ambaye ni Mwenyekiti wa CCT Morogoro amesema haki ni msingi kuu katika kukuza demokrasia duniani.

Amesema mahala penye vurugu na migogoro haki itakuwa imekanyangwa ama kukandamizwa.

Askofu Mameo amesema licha ya haki huinua taifa bado kwa upande wa wanawake hawapigiani chapuo na hiyo kushindwa kupendana wenyewe kwa wenyewe.

“Nitolee mfano mwanamke akasimama kwenye dayosisi hii kugombea uaskofu sidhani wanawake watampa kura, wanawake mpo wengi mnayo haki ya kulisemea Taifa kuhusu kusimamia haki,”amesema Askofu Mameo.

Askofu Mameo amelisifu Bara la Afrika kwa kukuza demokrasia katika upande wa haki sawa kwa wanawake na limeweza kutoa marais katika nchi tatu tofauti tofauti na  mabara mengine duniani yalidai ni vinara wa demokrasia.

Bara la Afrika limetoa maris wanawake watatu katika nchi ya Liberia ,Malawi na sasa Tanzania.

Kwa upande Mwenyekiti wa Wanawake Taifa CCT, Nailah Mayala amesema takribani wanawake 300 kutoka makanisa wanachama 12 Tanzania  wamekutana mjini Morogoro wakiwa  na lengo la kuliombea taifa na kujadili masuala mbalimbali  yanayowahusu wanawake.