ASKARI wanyamapori wa vijiji (VGS)37,wamehitimu mafunzo maalum ya kozi namba 18/2022 katika chuo cha mafunzo ya Uhifadhi Maliasili kwa Jamii Likuyusekamaganga wilaya ya Namtumbo mkoni Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mafunzo hayo,mkuu wa chuo hicho Jane Nyau alisema,askari hao wamepata mafunzo maalum ya mbinu za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ikiwa ni utekelezaji wa mkakati huo.
Amesema,mafunzo hayo yametolewa kwa muda wa wiki mbili chini ya ufadhili wa Mamlaka ya usimamizi Wanyamapori Tanzania(Tawa)na wahitimu hao wametoka katika wilaya na mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Nyau amesema,askari hao wamejifunza mbinu ambazo ni rahisi kuzitumia katika mazingira yao ya kawaida ambazo hazitumii gharama kubwa kiuendeshaji na zinawapatia faida nyingine mbadala.
Ametaja baadhi ya faida hizo ni kutumia mizinga ya nyuki ambayo mbali na kudhibiti wanyamapori hasa Tembo,lakini wananchi watanufaika kwenye kilimo kwani nyuki hao huhusika katika uchavushaji wa maua na hivyo kuongeza mazao kwa wakulima,wananchi kupata chakula ikiwamo asali na nta.
Alisema,matarajio ya chuo kwamba askari hao watakaporejea kwenye maeneo yao watakwenda kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na binadamu kwa kushiriki moja kwa moja kuwadhibiti na kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu walizofundishwa ili waweze kuzitumia kutatua changamoto hizo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mamlaka ya udhibiti wa wanyamapori Tanzania(Tawa)Kamishina msaidizi Said Mshana alisema, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Tawa imepanga kuchimba mabwawa 50 ya maji katika Hifadhi mbalimbali za Taifa.
Amesema,mpango wa kuchimba mabwawa hayo ni mkakati wa kudhibiti na kupunguza mtawanyiko wa wanyamapori wakali na waharibifu kwenda nje ya maeneo yao.
Amesema mkakati mwingine ni kuongeza doria za udhibiti wanyamapori pori wakali na waharibifu,ambapo jumla ya doria 64,724 zimefanyika katika kipindi cha Julai hadi Juni 2022 na kujenga vituo 16 vya kudumu vya askari wa kudhibiti matukio ya wanyamapori katika wilaya 16 hapa nchini.
Mshana amesema, hatua hizo na nyingine zilizopangwa kutekelezwa naTawa zitasaidia kupunguza changamoto ya mara kwa mara inayotokea ya wanyama hao kutoka kwenye hifadhi kwenda kwenye makazi ya watu na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao mashambani.
Kwa mujibu wa Mshana,matukio ya migongano kati ya wanyamapori na wananchi yanayoongezeka kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na binadamu kuendesha shughuli zao kwenye mapito na mtawanyiko,na hivyo kupelekea ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kamishina Mshana,amewakumbusha wananchi wanaokaa jirani na maeneo ya hifadhi,kutofanya shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo hayo,ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Mkuu wa wilaya ya Nantumbo Dkt Julius Ningu,ameipongeza Tawa kwa kuchukua hatua madhubuti katika kudhibiti matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ambao wanatishia maisha na mali za wananchi.
Amesema,hatua hizo pamoja na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mkakati wa Kitaifa wa kusimamia utatuzi wa migogoro baina ya watu na wanyamapori wa mwaka 2020-2024.
Amesema,mkakati huo unaohusisha wadau mbalimbali ikiwamo taasisi za uhifadhi,NGO’s na Halmashauri za wilaya utawezesha kupunguza migogoro na muingiliano kati ya wanyapori na binadamu.
Amewapongeza wahitimu kwa uvumilivu walioonyesha katika kipindi chote cha mafunzo na kueleza kuwa,mafunzo waliyoyapata yamewajengea utimamu wa mwili na kuwapatia mbinu za udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.
Katika risala yao iliyosomwa na Nassoro Ndengwike wahitimu hao walisema, katika kipindi cha mafunzo wamefundishwa mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu,uhifadhi wa maliasili zilizopo katika hifadhi za Taifa,sheria za uhifadhi,fidia na vifuta jasho.