JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI
Takriban watu 56 walikamatwa katika Hoteli ya St George katika eneo la Irene, jijini Pretoria, baada ya polisi kufanikiwa kumuokoa Waziri wa Ulinzi, Thandi Modise (pichani), naibu wake, Thabang Makwetla na Waziri katika Ofisi ya Rais, Mondli Gungubele.
Tukio hilo lilitokea Alhamisi jioni baada ya kikundi cha askari wa zamani wa Chama cha ANC kudaiwa kuwateka viongozi hao na kuwazuia hotelini humo kwa muda.
Walikuwa wanadai walipwe rand milioni 4.2 kwa kila mmoja.
Mawaziri hao walikwenda kwenye hoteli hiyo kwa ajili ya kukutana na chama cha askari wa zamani waliopigania uhuru (LSWV), kinachoundwa na askari wa vikundi kadhaa waliopigana dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Vikundi hivyo ni pamoja na Umkhonto weSizwe (MK), the Azanian People’s Liberation Army (Apla) na Azanian National Liberation Army (Azanla).
Kabla ya tukio hilo, wanachama wa kundi hilo waliandamana nje ya jengo la Luthuli, yalipo makao makuu ya ANC na kuwalazimisha watu kukimbia kutoka katika jengo hilo.
Msemaji wa SAPS, Brigedia Vish Naidoo, alisema polisi walipata taarifa kuhusiana na kutekwa kwa mawaziri hao Alhamisi alasiri.
“Baada ya juhudi za kufanya majadiliano na watekaji kushindwa, polisi waliamua kutumia utaalamu wao kukabiliana na hali hiyo. Hivyo walifanikiwa kuwaokoa mawaziri hao. Hakuna risasi zilizopigwa katika tukio hilo,” alisema Naidoo.
Aliongeza kuwa watu 56 walikamatwa katika tukio hilo na kuna uwezekano mkubwa wakafikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka matatu ya utekaji nyara.
Katika taarifa iliyotolewa kwa njia ya video, Gungubele alisema: “Tulijikuta katika hali ambayo binafsi sikutarajia tukiwa tumeshikiliwa kinyume cha sheria. Tulidhani kuwa tunahudhuria kikao kujadili matatizo ya askari hao.
“Hatukukubaliana jinsi kikao hicho kinavyopaswa kuendeshwa. Ilifika wakati nadhani tulikubali kutokubaliana na kuamua kuahirisha kikao lakini wakati tunataka kutoka wakafunga milango,” anabainisha.
Anasema ilikuwa katika hatua hiyo ndipo alipobaini kuwa wametekwa lakini baadaye wakaokolewa na polisi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la News24, kikosi maalumu (STF) kiliongoza harakati za kuwakomboa mawaziri hao. Kikosi hicho ni cha askari polisi maalumu ambao huvalia sare za jeshi na wamepewa mafunzo ya kukabiliana na ugaidi.
Bado haijafahamika iwapo wanachama hao wa LSWV walitoa vitisho kwa mawaziri hao wakati wakiwashikilia.
Kwa kawaida ANC hufanya vikao vyake katika hoteli hiyo ambayo hulindwa na polisi wakati wa vikao hivyo.
Hata hivyo, msemaji wa LSWV, Lwazi Mzobe, aliiambia Newsroom Africa kuwa Modise hakushikiliwa kinyume cha hiari yake.
Kundi hilo linaidai serikali imeshindwa kuwahudumia wapigania uhuru na wanadai fidia ya rand milioni 4 kwa kila mwanachama.