Wanajeshi wapatao 75 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watapandishwa kizimbani leo, kwa kukimbia mapigano baada ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kusonga mbele katika jimbo la mashariki la Kivu Kusini.

Taarifa iliyotolewa Jumapili na ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi ilisema kuwa askari hao pia wanashitakiwa kwa vurugu dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na mauaji na uporaji.

Wanajeshi 75 wanaokabiliwa na kesi walikamatwa kwa kukimbia mapigano baada ya kushikiliwa kwa mji wa Nyabibwe. Wanatuhumiwa kwa ubakaji, mauaji, uporaji na uasi, ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi imelieleza shirika la habari la Reuters.

Umoja wa Mataifa umeripoti ukiukaji mkubwa ikiwemo unyongaji, ubakaji wa magenge na utumwa wa kingono kufuatia msako mkubwa wa M23 mwishoni mwa mwezi Januari ambao ulipelekea kutekwa kwa mji mkubwa wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa iligundua kwamba wapiganaji wa M23 na askari wa serikali pamoja na wanamgambo wanaounga mkono serikali wote wanahusika. Kongo bado haijatoa tamko kuhusu ripoti hiyo kuhusiana na vikosi vyake lakini imeutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza ukiukajiinaodai unafanywa na M23 na Rwanda.

Rwanda, ambayo inakanusha kuunga mkono kundi la M23, imekataa jukumu lolote. Waasi wa M23 hawajajibu maombi ya kutoa maoni yake. Licha ya tangazo la upande mmoja la usitishaji mapigano, waasi hao wameendelea kusonga mbele kuelekea mji mkuu wa Kivu Kusini, Bukavu.