Askari wahifadhi wa TANAPA 97 wamehitimu mafunzo ya aina tatu tofauti katika chuo cha Uhifadhi Maliasili Jamii cha Likuyu Sekamaganga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mafunzo hayo kwenye hafla ya ufungaji mafunzo hayo iliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho,Naibu Kamishina wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda wa Kusini Asteria Ndaga alisema kati ya wahitimu,askari Uhifadhi 52 wamehitimu mafunzo ya awali ya ajira mpya.
Kamishina Ndaga amewataja maafisa Uhifadhi saba na Askari Uhifadhi mmoja wamehitimu mafunzo ya mabadiliko ya utendaji kazi kutoka mfumo wa kiraia na Kwenda kwenye mfumo wa kijeshi na maafisa Uhifadhi Daraja la pili wapatao 37 wamehitimu mafunzo ya awali ya Uongozi.
Hata hivyo Ndaga amesema mafunzo hayo yalifunguliwa katika vipindi vitatu tofauti yakijumuisha wanawake saba na wanaume 90 ambapo kati yao 44 ni maafisa uhifadhi na 53 ni Askari Uhifadhi na kwamba mafunzo yalifundishwa kwa njia ya nadharia na vitendo.
Amezitaja mada mbalimbali zilizofundishwa kuwa ni uzalendo,maadili, kuzuia na kupambana na rushwa,elimu ya uhifadhi na utalii,uraia,uchunguzi,utoaji Ushahidi mahakamani,namna ya kuandaa hati za mashitaka,sheria za ulinzi,utunzaji wa vielelezo, mafunzo ya uongozi na mifumo mbalimbali inayotumika katika uhifadhi.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika ufungaji wa mafunzo hayo Naibu Kamishina wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Herman Batiho amewapongeza wahitimu wote kwa kuhitimu mafunzo hayo muhimu ambayo amesema yamewajengea uwezo wa usimamizi wa rasilimali za wanyamapori na misitu ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa.
“Ni matumaini yangu mafunzo haya yamewajengea uzalendo,uadilifu,ujasiri,utayari,kujiamini Pamoja na kuwapa mbinu na ari kubwa katika kulinda maliasili za Taifa’’,alisisitiza Kamishina Batiho.
Hata hivyo aliwataka wahitimu kuhakikisha mafunzo hayo wanayafanya kwa vitendo katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku kwenye vituo vyao vya kazi na kusisitiza kuwa mbinu walizojifunza kwenye mafunzo hayo zikawe chachu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za uhifadhi hususan kukabiliana na majangili.
Naye Kamishina Msaidizi Mwandamizi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere Witness Shoo amewaasa wahitimu kuhakikisha wanafanya kazi kwa uaminifu kwa sababu serikali tayari imewapa ajira ambayo ni dhamana kwao.
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo Afisa Uhifadhi TANAPA Mwandamizi Ombeni Gingi akizungumza kwa niaba ya wenzake ameahidi kutumia mafunzo hayo katika kusimamia rasilimali za Taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga Namtumbo kilianzishwa mwaka 1995 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma