Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Vuruguru kubwa zimeibuka katika kijjji cha Jangwani,Mto wa Mbu Wilaya ya Monduli mkoani Arusha na kusababisha mtu mmoja kufariki kwa kudaiwa kupigwa risasi na askari wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na wengine saba kujeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Mout Meru.

Akizungumzia tukio hilo mmoja ya wananchi wa kijiji hicho,Samsoni Saria amesema tukio hilo limetokea jana kati ya saa tatu asubuhi na saa 11 jioni katika kijiji cha Jangwani na eneo la Kirurumo wilayani humo.

Amesema kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa mipaka kati ya kijiji cha Jangwani ni eneo la Hifadhi la Ziwa Manyara.

Amesema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya asubuhi baada ya wananchi wanaojishughulisha na uvuvi kuonekana katika ziwa hilo wakivua samaki na mitumbwi, ndipo askari wa TANAPA wakiwa na boti ya doria waliwavamia na baadhi yao kuwakamata na kuwafunga pingu na wengine kuzamishwa kwenye maji.

Amesema kuwa kutokana na tukio hilo liliamsha hasira kwa wananchi wa kijiji hicho baada ya kuwepo taarifa ya vijana waliokuwa wakivua ziwani kufa na kwenda kufanya uharibifu wa mali mbalimbali kwenye ofisi za TANAPA zilizopo Kirurumo Mto wa Mbu,na kuwataka askari wa TANAPA wawaonyeshe wenzao wawili ambao hawaonekani.

Hata hivyo askari hao kwa kushirikiana na Polisi walifyatua mabomu ya machozi ambapo Mkuu wa Wilaya ya Monduli,Joshua Nasari alifika eneo la tukio Kirurumo na kuwasihi wananchi kuacha vurugu hizo.

“Nawaomba mtulie wakati malalamiko yenu yakitafutiwa ufumbuzi na pia kuwasaidia wananchi waliojeruhiwa baada ya kutokea vurugu kwani hadi sasa mtu mmoja amepoteza maisha na wengine wamejeruhiwa niwasihi wananchi watulie wakati serikali inashughulikia suala hili ” amesema.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Kirurumo,Dkt. Melisa Saeli amesema wamepokea majeruhu saba wakiwa na majeraha miguuni,tumboni ,befani na kichwani na watano wamewapa rufaa kwenda Hospital ya Rufaa Mt. Meru,mkoani Arusha.

Naye Kamishna wa Uhifadhi Tanapa, William Mwakilema akiongea amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hatua zaidi za uchunguzi zinafanywa na Jeshi la Polisi ambao watatoa taarifa zaidi juu ya tukio hilo.

“Ni kweli kuna changamoto imetokea ila tumekaa kikao na kukubaliana kwamba jeshi la Polisi wanafanya uchunguzi na ndio watatoa ufafanuzi wa tukio hilo,” amesema.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP-Justine Masejo amekiri kutokea kwa tukio hilo mnano Mei 22, 2023 majira ya saa 5:40 asubuhi huko katika Kitongoji cha Magomeni kijiji cha Jangwani eneo la Mto wa Mbu Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha.

Amesema kuwa askari wa hifadhi ya Manyara wakiwa katika doria ya kawaida eneo la ziwa Manyara waliwakamata wavuvi watatu waliokuwa wakivua samaki katika maeneo yaliyozuiliwa kwa uhifadhi.

Walijitokeza wavuvi wengine na kuzusha vurugu iliyopelekea askari hao wa uhifadhi kushindwa kuwachukua watuhumiwa hao na kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi.

Amesema kuwa umati wa watu hao walikwenda hadi kwenye ofisi ya kijiji cha Jangwani na kufanya uharibifu mkubwa katika ofisi hiyo ya Serikali kwa kuvunja madirisha pamoja na kuchana bendera ya Taifa na kuondoka nayo kwa madai kuwa wavuvi wenzao wamezamishwa kwenye maji wakati wanakamatwa na Askari wa uhifadhi.

Kamanda amesema kuwa baada ya uharibifu huo, kundi hilo liliamua kuelekea ofisi na makazi ya askari wa TANAPA yaliyopo Mto wa Mbu.

“Watu hao wakiwa wanaelekea kuvamia ofisi na makazi ya TANAPA njiani walifanya uharibifu mkubwa wa magari kwa kutumia marungu na mawe pamoja na kupanga mawe barabarani kuzuia watumiaji wengine wa barabara wasiendelee na shughuli zao.

“Licha ya juhudi za kuwazuia kuingia katika ofisi na makazi hayo ya TANAPA watu hao waliendelea kupambana na askari wa uhifadhi na ndipo Jeshi la Polisi waliongeza nguvu kuokoa kuzuia madhara zaidi kwa binadamu na mali za watu binafsi na za Serikali.

“Kutokana na ghasia hizo mtu mmoja alipoteza maisha na watu saba walijeruhiwa na wamelazwa hospitali wakiendelea na matibabu na watu 12 wanashikiliwa na jeshi la polisi kuhusiana na tukio hilo,” amesema.

Amesema kuwa upelelezi wa shauri hili unaendelea kubaini walioanzisha na kushiriki katika vurugu hizo pamoja na kuchunguza madai ya wananchi kuwa kuna wavuvi wamezamishwa katika maji. Uchunguzi ukibaini ukweli kulingana na ushahidi watu hao watafikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha tunaendelea kutoa onyo kali kwa baadhi ya watu ambao wanatabia ya kupambana na vyombo vya dola ambao kimsingi wamepewa dhamana ya kulinda maisha ya watu, mali zao pamoja usalama wa nchi kwani inaweza kusababisha madhara makubwa.

“Endapo kuna changamoto yoyote zipo taratibu nzuri za kufuata kuliko kufanya vurugu na kujichukukulia sheria mikononi kwa kupambana na vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria ya kulinda maisha ya watu, mali zao na rasilimali za Taifa,” amesema kamanda.