Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro
Askari kutoka Ukanda wa Mashariki Mwa Afrika wametakiwa kujiweka imara katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka, ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo wakati akifunga rasmi zoezi la utayari FTX USALAMA PAMOJA 2024 lililofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura amesema kuwa kufanyika kwa zoezi hilo la utayari kutachochea kuongeza hali na morali kwa askari katika kukabiliana na makosa mbalimbali ya uhalifu.
Akizungumzia umuhimu wa zoezi hilo IGP Wambura amesema kuwa, litawezesha kupima utayari wa askari, kuongeza maarifa Pamoja na kuimarisha uhusiano na mashirikiano.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika ambaye pia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Burundi Meja Jenerali Fredric Budomo amesema kuwa kufanyika kwa zoezi la utayari nchini Tanzania ni miongoni mwa mafanikio makubwa hasa katika eneo la kuongeza maarifa katika kuukabili uhalifu wa kimataifa.
Pia Mhe. Sillo amesisitiza suala la mashirikiano hasa katika eneo la kubadilishana taarifa za uhalifu na wahalifu jambo ambalo litasaidia kuzifanya nchi wanachama kuendelea kuwa salama.
Tukio hilo la ufungaji wa zoezi la utayari FTX2024 pia limehudhuriwa naMkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Camillus Wambura pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Burundi Meja Jenerali Fredric Budomo ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAPCCO, IGP wa Rwanda Kamishna Jenerali Felix Namuhoranye, Naibu Inspekta Jenerali wa Kenya Kutor Mathew Kipruto Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Sudani Kusini Luten Jenerali Jackson Elia Haiaka na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Uganda Abaasi Byakagaba.