Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
UTAFITI uliofanywa na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) umebainisha kuwa asilimia 50 ya mkaa mbadala unaotumiwa katika maeneo mbalimbali hauna ubora.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Mtambo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema takwimu hiyo imetokana na tafiti waliyofanya katika mikoa 12 ikiwa na lengo la kuwabaini wanaotumia mkaa mbadala kupitia mradi wa kukuza matumizi ya nishati.
Amesema kutokana na utafiti huo Mkoa wa Dar es Salaam umeonekana kuongoza kuwa na watumiaji wengi wa Mkaa Mbadala.
“Tulibaini kuwa watengenezaji wengi kufanya shughuli hiyo bila kupata mafunzo ya kitaalamu. Pia tukabaini changamoto za malighafi ya utengenezaji wa mkaa mbadala ambapo imeonekana watengenezaji wengi wanatumia mabaki ya mkaa yanayotokana na kuni ambayo yanatoa mkaa wenye ubora ambao tunaupiga vita.
“Mradi huu ulianza mwaka 2022 kwa kuwabaini watengenezaji wa mkaa mbadala katika mikoa 12 ambapo tulikusanya takribani watumiaji 59, katika kuangalia ubora wa mkaa na sampuli zaidi ya 43 ambazo ni zaidi asilimia 50 tukazikuta hazina ubora. Kutokana na hali hiyo tumetoa mafunzo kwa watengenezaji zaidi ya 30 kwenye mikoa 11 tuliyoifanyia utafiti na tunaendelea kuwaita watengenezaji wengine waje kupata mafunzo Tirdo,” amesema Profesa Mtambo.
Amesema mbali na hilo utafiti pia umeonyesha wanaopaswa kutumia mkaa mbadala hasa taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 ambazo ni 127 zilizofanyiwa utafiti asilimia 52 bado wanatumia kuni hivyo changamoto bado ipo.
Profesa Mtambo amewakaribisha watengenezaji wa mkaa na watumiaji kufika katika ofisi hiyo kwa ajili ya utengenezaji wa nishati hiyo kupitia mradi hio ambao unaendelea.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (REPOA), Dkt. Donald Mmari amesema kama taasisi waliona wafanye utafiti ambapo walianza kwakuangalia kuhusu utumiaji wa mkaa na faida zake kiafya.
“Sisi REPOA pia tumeshiriki katika mradi huo na moja ya jambo ambalo tumelibaini ni uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni nchini. Mwaka 2015 upotevu wa misitu hekta 372,000 lakini miaka saba baada yaani ilipofika mwaka 2022 upotevu umefika hekta takribani 400,000 tukaona hiyo ni mbaya sana,watu wanakata miti inaleta madhara ikiwemo hewa ya ukaa lakini pia kuongezeka kwa ukame na majanga,” amesema Dkt. Mmari.