Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Shujaa Cancer Foundation kwa kushirikiana na ubalozi wa Sweden nchini pamoja na Wizara ya Afya kwa pamoja wameungana kuadhimisha mwezi wa uhamasishwaji wa saratani ya matiti.

Maadhimisho hayo yalilenga kusisitiza umuhimu wa kugundua mapema, elimu, na msaada wa jamii katika vita dhidi ya saratani ya matiti.

Sherehe za maadhimisho hayo zilifanyika hapo jana katika eneo la michezo viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya maadhimisho hayo mkurugenzi mkuu wa asasi ya shujaa Cancer Foundation Bi:Gloria Kida ameeleza kuwa maadhimisho hayo imekuwa ni sehemu ya muendelezo kwa wao kuadhimisha mwezi wa saratani ya matiti kwa kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya mambo ya saratani ambayo yamekuwa yakitokea katika jamii.

“Kwa huu mwezi wa kumi ni mwezi ambao tunautumia kujaribu kuelimisha jamii kuhusiana na habari ya uchunguzi wa saratani ya matiti. Na kwakuwa asasi yetu inashughulika pia na masuala ya saratani ya matiti kila unapofika mwezi ambao tuna wale mashujaa ambao tunashughulika nao kwa huwa tunajaribu kuhamasisha juu ya saratani. Sisi kama asasi tulikaa tukashauriana njia gani rahisi ya kuwakutanisha watu wa rika zote kwani saratani ya matiti haiwakumbi wanawake peke yao isipokuwa kila mtu.”amesema.

Mbali na mkurugenzi huyo wizara ya afya kupitia muwakilishi wake katika kongamano hilo ambae ni mkurugenzi msaidizi wa magonjwa yasiyoambukizwa katika wizara ya afya Dkt: Omary Ubuguyu akiwasilisha salamu zake kutoka wizara ya afya amesema kuwa wao kama serikali wanatambua juhudi zinazofanywa na asasi hiyo ya shujaa katika kuhakikisha wanapambana na changamoto ya tatizo la saratani.

“Sisi kama serikali tunatambua jitihada za wazi zinazofanywa na asasi hii ya shujaa na ni hatua muhimu sana za kuunga mkono juhudi za serikali kwenye kupambana na matatizi ya saratani. Tanzania kwa sasa tunaathirika kwa kiasi kikubwa na changamoto ya saratani hivyo katika jamii yetu kuna umuhimu mkubwa wa kutambua uwepo wa saratani hizi na namna bora ya kukabiliana nazo.” Alisema.

Kongamano hilo pia limewezeshwa kwa ukaribu na ubalozi wa Sweden nchini Tanzania ambapo ubalozi huo umeahidi kujitolea kushughulikia changamoto ya kimataifa ya saratani ya matiti kwa kutoa misaada ya kibinadamu na mikakati ya muda mrefu ikiwa lengo lake ni kuhakikisha kila mwanamke, popote alipo, anapata huduma ya kugundua mapema tatizo hilo na kupata matibabu.

Maelezo hayo yaliwasilishwa na muwakilishi wa ubalozi wa Sweden katika kongamano hilo Bwn: Mikael Stahl ambae ni mkuu wa siasa, biashara na mawasiliano katika ubalozi wa Sweden.

“Leo tumekuja pamoja si kwaajili ya mazoezi tu, bali kwa ajili ya kuongeza uelewa kuhusu saratani ya kawaida zaidi kwa wanawake duniani. Saratani ya matiti inaua zaidi ya watu 600,000 kila mwaka na asilimia 62 ya vifo hivi hutokea katika nchi zinazoendelea. Kupitia kugundua mapema, nafasi za kupona huongezeka kwa kiasi kikubwa na ndio maana matukio kama haya ni muhimu kwaajili ya kuongeza umuhimu na kuhamasisha uchunguzi wa mapema na kuokoa maisha.”

“Sweden, kwa kushirikiana na mashirika ya ndani kama shujaa cancer foundation na mengine ya kimataifa, imejitolea kushughuliikia changamoto ya kimataifa ya saratani ya matiti kwa kutoa misaada ya kibinadamu na mikakati ya muda mrefu ikiwa na lengo la kuhakikisha kila mwanamke, popote alipo anapata huduma ya kugundua mapema na matibabu.” Alisema.

Maadhimisho hayo pia yalihusisha waathirika mbalimbali wa saratani ambao walikumbana na ugonjwa huo na kupona tatizo ambao wanatizamwa kama mashujaa wa saratani ya ugonjwa wa matiti.