Wiki hii Kampuni ya Jamhuri Media Limited inaandika historia ya kipekee. Juni 28, 2011 kwa ushirikiano wa waandishi wa habari wanne, tulisajili kampuni ya Jamhuri Media Limited. Oktoba 5, 2011 tulipata usajili wa Gazeti Jamhuri. Desemba 6, tukachapisha nakala ya kwanza ya Gazeti Jamhuri. Ni wazi basi, kuwa wiki hii tunahitimisha mwaka mmoja na nusu wa kampuni kusajiliwa, lakini pia tunatimiza mwaka mmoja wa kuendesha Gazeti Jamhuri.

Kutokana na tukio hili, nimejikuta nawiwa kukushukuru wewe msomaji wa gazeti hili, kuwashukuru wafanyakazi wa Gazeti Jamhuri, Wakurugenzi na ndugu na jamaa ambao kwa njia moja au nyingine wamechangia kwa kiasi kikubwa gazeti hili kufikia hapa lilipo. Najikuta kwa kila hali nikilazimika sasa kuwataja wote walioshiriki katika kuhakikisha gazeti hili linaingia mitaani.


Hawa nitawataja wale tu, waliopo kwenye chumba cha habari. Wa kwanza ni Manyerere Jackton. Huyu ni Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti Jamhuri. Manyerere tumefanya wote kazi katika kampuni tatu, kabla ya yeye na mimi kukubaliana kuanzisha Gazeti Jamhuri. Kabla ya hapo tulifanya kazi wote Majira, Tanzania Daima na hatimaye Habari Corporation, yeye akiwa Mhariri wa Mtanzania na mimi nikiwa Mhariri Mtendaji pale.


Mwingine ni Manyilizu Magembe. Huyu anafanya kazi katika idara ya fedha. Tulipata kufanya kazi wote Habari Corporation pia. Wengine ni Christopher Gamaina (Mhariri wa Habari), Anderson Mbeyela (Afisa Usambazaji), Magdalena Paul (Mwandishi), Suzana Rose Senga (Mtaalam wa Kompyuta). Siwasahau pia wafuatao:- Esther Mbusi, Sarah Mossi na Zuberi Mohamed, ambao tulianza nao kazi, lakini kiungwana wao waliamua kutafuta malisho ya kijani zaidi sehemu nyingine. Hawa wote nawashukuru sana. Wamekuwa nguzo kwa gazeti hili kusimama na kufikia hatua ya leo.


Wakati nikiwashukuru hawa, napaswa sasa kuwashukuru Wakurugenzi wengine wawili wa Jamhuri Media Limited. Hawa si wengine, bali ni Absalom Kibanda na Neville Meena. Tulishirikiana nao kwa kiasi kikubwa wakati tunafanya vikao vya kuanzisha kampuni kwa muda usiopungua miezi sita kuanzia Januari 2011. Ingawa kiuendeshaji tumebaki wakurugenzi wawili sasa; Manyerere Jackton na Deodatus Balile, tunauthamini mchango mkubwa wa mawazo na fedha kidogo walizochangia hawa wenzetu katika hatua hizi za awali.


Sitanii, haijawahi kuwa rahisi. Ndani ya mwaka mmoja nimesikia maneno mengi juu ya umiliki wa kampuni na gazeti hili, na wala leo sitatumia fursa hii kuyajibu, ila walau kwa nia ya kuonesha ugumu wa kuanzisha kampuni na hatimaye gazeti nisimulie kidogo hatua tulizopitia. Tulikuwa tunafanya vikao katika baa ya Calabash pale Mwenge Dar es Salaam kila Jumamosi saa 4 asubuhi.


Gharama ya kusajili kampuni na gazeti haikuzidi shilingi milioni 2. Kiasi hiki cha fedha si kikubwa, lakini kwa wakati huo kiasi hiki kilikuwa kikubwa. Yapo mengi ya kukumbuka, lakini nakumbuka siku tuliyopaswa kuchonga mhuri wa kampuni zilihitajika Sh 45,000 hatukuwa nazo. Kibanda ilibidi akakope fedha hizi na kwenda kulipia.


Siku nyingine, kabla ya kukamilisha usajili wa kampuni tukiwa pale Mlimani City, tulikabana koo kuchangishana shilingi 400,000. Ilibidi posho tulizokuwa tumepata kutoka safarini tukabane kwa nguvu kuweza kuchangishana kiasi hiki.

 

Napenda kukufahamisha mpendwa msomaji kuwa wakati huo hatukuwa na mishahara na hivyo hali ilikuwa ngumu kweli. Ni kweli katika mazingira hayo tunao marafiki tuliowaeleza nia yetu ya kuanzisha gazeti. Nachukufa fursa hii kuwashukuru wote kwa michango yao ya hali na mali na hasa rafiki yetu mmoja aliyeko mkoani Iringa, aliyetuwezesha kupata fedha za kuweka kwenye akaunti na hatimaye tukaweza kusajili gazeti hili. Nafahamu wengi waliotusaidia katika hatua hii walituasa kuwa wasingependa kutajwa majina yao, na hivyo siwezi kuvunja makubaliano haya.


Sitanii, lakini pia nimesikia maneno yenye kunisikitisha kwa kiwango kikubwa. Wapo watu tuliowaendea, tukawaomba msaada, wakatuahidi ila bahati mbaya hadi leo mwaka mmoja tunaendesha gazeti, hawakupata kutimiza ahadi yao ya kutusaidia. Hata hivyo, hawa wamekuwa mabingwa wa kuutangazia umma kupitia mitandao ya jamii kuwa ama walitusaidia au wanaendelea kutusaidia. Inakera mno. Hata hivyo, imetubidi kukubaliana na busara za wahenge kuwa “simba akiishauawa, wanaojipaka damu ni wengi.”


Wanajipaka damu si kwa sababu wajichafue, bali makusudi wahesabiwe katika kundi la mashujaa kuwa wameshiriki kumuua simba, hivyo wao si waoga nao ni mashujaa sawa na wauaji wa simba. Kero yangu katika hili, ni tabia inayozidi kukua hapa nchini.

 

Tabia hii si nyingine, bali ni maelezo kuwa kwa mwandishi wa habari akijikusanya (hata kwa kuomba sawa na walivyofanya watu wa taaluma nyingine) na kuanzisha gazeti, redio au televisheni, basi amehongwa. Hata hivyo, kwa tasnia au taaluma nyingine kama madaktari wakihitimu masomo na kujenga hospitali binafsi, basi huyo ni halali, hakuhongwa.

 

Muuza duka akifungua kibanda, basi hiyo ni halali. Fundi wa gereji akifungua carwash, basi hiyo ni halali. Mwalimu chuo kikuu anapofungua shule binafsi ya msingi au sekondari, hiyo ni halali, lakini mwandishi akianzisha gazeti, basi amehongwa. Ebo!


Sitanii, napenda kuwasihi Watanzania tujaribu kuwa na mtazamo chanya. Tuwape moyo Watanzanai wenzetu, wanaothubutu kujitoa mhanga kufungua kampuni na kuendesha magazeti, redio au televisheni. Biashara hii ni ngumu kweli. Zipo kampuni kubwa hapa nchini, ambazo wamiliki wake walianza kwa kuuza kalamu na karatasi za chooni (toilet papers), lakini leo zina heshima ya pekee.

 

Orodha ya wafanyakazi niliyoitaja hapo juu, walau tunao watu 10 waliopata ajira ya moja kwa moja katika gazeti hili (idadi itaongezeka si muda) na hivyo tumechangia katika kukuza ajira nchini.


Ukiacha hao, tukizungumzia ajira tunazotengeneza nchini kupitia mawakala (agents), wauza magazeti mkononi na kwenye mbao (vendors), ni wazi tunatoa ajira kwa watu wasiopungua 250 hapa nchini. Naamini tulistahili kupongezwa badala ya kukejeliwa na baadhi ya watu wenye mitazamo ya kisiasa. Ombi hili, linanifanya nirejee kauli yangu niliyoitoa mwaka jana. Tunaomba wasomaji na wananchi kwa ujumla mtuhukumu kwa kazi yetu na si kwa hisia.


Baada ya kuyasema hayo, nirejee kuwashukuru wasomaji wetu. Tuliwaahidi siku ya kwanza kabisa wakati tunaanzisha gazeti hili, kuwa tumelianzisha kwa nia ya kutumikia jamii. Tuliahidi kujikita katika maeneo ya msingi ya uandishi wa habari ambayo ni kuburudisha, kuhabarisha na kuelimisha. Nafurahi kusema kazi hii tumeifanya vizuri mno.


Tunashukuru wasomaji wetu kwa heshima kubwa mliyotupatia kutokana na kazi ya mikono yetu. Kufikia hatua ya kuuza nakala 20,000 ndani ya mwaka mmoja, hakika haliwezi kuwa jambo la mchezo. Nimeshiriki kuanzisha magazeti mengi hapa nchini; yakiwamo Mwananchi, Mwanaspoti, Tanzania Daima, Sayari na nimepata kusimamia magazeti kama Rai, Mtanzania, Bingwa, Dimba na The African. Najua ilivyo kazi ngumu kuuza idadi hii ya nakala. Waliopo kwenye tasnia ya habari, wanalijua hili.


Sitanii, mkondo na mwelekeo wa gazeti letu ni kukua zaidi. Tulisema na hapa tunarudia, kuwa tutawafikishia wananchi habari zilizofanyiwa uchunguzi wa kina, zisizomuonea mtu na wala zisizokuwa majungu. Tunafurahi kusema kifua mbele kuwa kazi hii tumeifanya kwa kiwango ambacho hata waliokuwa wanatutilia shaka, leo ni watetezi wetu kuwa kweli tunaitumikia jamii. Naahidhi kuwa kazi hii tutaindeleza kwa nguvu ya kipekee kutokana na ushirikiano mnaotupa wasomaji. Nasema, asanteni sana na Mungu awabariki.


Tunayo mawazo ya kukua zaidi. Tunafikiri kuingia katika uwanda mpana wa vyombo vya habari, ikiwamo magazeti mengi zaidi, redio, uchapishaji, televisheni na mtandao. Mipango hii yenye nia njema tunaamini kuwa tutaitekeleza na hatimaye Jamhuri Media Limited kuwa kampuni kubwa kitaifa na kimataifa. Nasema tumedhamiria, tumethubutu na tuungeni mkono. Mungu ibariki Jamhuri Media Limited, Mungu ibaridi Tanzania.