Wiki iliyopita, yaani Desemba 6, 2018 Gazeti la JAMHURI limetimiza miaka saba sokoni. Sasa tumeanza mwaka wa nane. Katika kipindi chote hicho cha miaka saba hatujawahi kushindwa kwenda sokoni. Tumechapisha kwa ukamilifu matoleo yote 52 kila mwaka na ya ziada tulipopata matoleo maalumu. Ndiyo maana toleo la leo ni la 376. Katika maoni yetu ya Desemba 6, 2011 tulipotoa nakala ya kwanza tulitoa ahadi.

Tuliahidi kuwa Gazeti la JAMHURI litakuwa gazeti huru, lisilokuwa na upendeleo wala kufungamana na upande wowote. Tuliahidi kufanya habari za uchunguzi na kutoa uwanja sawa kwa vyanzo vya habari, jamii, watuhumiwa na vyama vya siasa. Ila tulieleza bayana kuwa siasa si mkondo tutakaoupa kipaumbele katika habari zetu.

Tulisema bayana kuwa tunaamini jamii inayo matatizo mengi ya msingi ikiwamo rushwa, uonevu, matumizi mabaya ya madaraka, wizi wa mali za umma, matatizo ya kijamii kama dawa za kulevya, mifumo ya uendeshaji wa taasisi za umma kama tulivyoimulika Bandari ya Dar es Salaam miaka ya 2013-2015 na sasa ina ufanisi wa kupigiwa mfano.

Tangu tumeanza kuchapisha Gazeti la JAMHURI, tunasimama kifua mbele na kuonyesha kazi tulizozifanya mbele ya jamii kwa kufichua wakwepa kodi, wauza dawa za kulevya, waharibu uhifadhi na maliasili kule Loliondo na kwingineko, ukwapuaji wa fedha za umma kama E-passport, flow meters bandarini na makontena kupotea, TBL na mpango wa kodi, Kampuni ya Lake Oil iliyopigwa faini ya Sh bilioni nane ikazilipa baada ya sisi kuchapisha habari na mengine mengi.

Si kwa bahati mbaya kuwa gazeti letu halijajikita mno katika habari za kisiasa. Tunafahamu kuwa tunaishi kwenye jamii iliyo na haja ya kufanya siasa, lakini tunawashukuru wasomaji wetu kwa kutuelewa kwani matukio mengi ya kisiasa tumekuwa hatuyaandiki si kwa bahati mbaya, bali mkondo tuliouchagua wa kuandika Habari za Uchunguzi na Habari zenye Masilahi kwa Jamii (IJ/PIJ).

Tunapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wasomaji wetu na watangazji kwa kutuunga mkono katika kutoa huduma hii ya msingi katika jamii. Habari ni haki ya binadamu ya msingi. Hii ni haki wezeshi, kwa maana kwamba habari sahihi zinawezesha haki nyingine kupatikana. Tunaamini waliokuwa wakituuliza maswali ya umiliki, vyanzo vya fedha na uwezekano wa kuwapo sokoni kwa miaka hata miwili, sasa jibu wanalo.

Tunafahamu kuna changamoto nyingi katika tasnia ya habari, kwani uwezo wa wasomaji kununua magazeti umepungua, uwezo wa watangazaji kutoa matangazo umepungua, lakini kwa kuwa tuliahidi kuitumikia jamii na kuhakikisha tunachangia kujenga Tanzania imara isiyo na rushwa, yenye miundombinu imara, mifumo inayofanya kazi na maendeleo, tunajibana na kuhakikisha huduma hii haisitishwi.

Ni kwa msingi huo huo, tunaamini Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli katika eneo la ujenzi wa miundombinu kama reli ya Standard Gauge, umeme wa Stiegler’s Gorge, ununuzi wa ndege na ujenzi wa barabara, hatuoni aibu kusema serikali inajenga msingi imara utakaoiwezesha nchi yetu kufuta umaskini siku za usoni. Hata hivyo, tunaiomba serikali iangalie uwezekano wa kuongeza mzunguko wa fedha kidogo angalau wananchi wapumue.

Tunawashukuru wasomaji wetu, viongozi wa kiserikali, vyama vya siasa, jamii, viongozi wa dini na taasisi zisizo za kiserikali ikiwamo Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) ambao wametupatia maarifa yanayozaa matunda katika utendaji wetu.

Tunawashukuru wafanyakazi wote wa Jamhuri Media Limited kwa kuweka nguvu na akili yao katika kuzalisha Gazeti la JAMHURI, maana bila ninyi tusingeweza. Tunaomba mwendelee kutuunga mkono na tuendelee kushirikiana. Mungu ibariki JAMHURI, Mungu ibariki Tanzania.