Desemba 6, 2017 itabaki kuwa siku muhimu katika kumbukumbu za kazi nilizopata kuzifanya. Hii ni siku ambayo Serikali, kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ilitangaza ‘kuumaliza’ mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo.
Naikumbuka siku hii, si kwa sababu ya kumalizwa kwa mgogoro, bali kwa sababu Serikali imethubutu kutenda kile ambacho Serikali mbili au tatu zilizopita zilifeli.
Wala sitoikumbuka siku hii kama ya ushindi. Anayejua vema chanzo cha mgogoro wa Loliondo hawezi kuamini kuwa mgogoro umemalizwa! Lakini atapongeza hatua nzuri na ya kijasiri ya Serikali katika kuhakikisha kuwa jambo hili linafikia tamati.
Kwa miaka mingi nimeripoti habari za Loliondo. Nimekomalia suala la Loliondo kiasi cha baadhi ya watu kuhoji nini hasa ninachokitafuta. Bila shaka majibu wameshayapata sasa. Uamuzi wa Serikali wa kuunda chombo maalumu kulilinda eneo hili kiuhifadhi ndio msimamo wangu wa miaka yote. Nina kila sababu ya kuipongeza Serikali kwa kuheshimu maoni ya wahifadhi badala ya wanasiasa. Serikali imefanya jambo la kukumbukwa na kizazi cha sasa na kizazi kijacho kwa sababu imethubutu.
Kwenye mapambano haya tupo wengi. Kumekuwapo wapambanaji waadilifu na makini ambao kwa kipindi chote walitia pamba masikioni. Hawakuruhusu kukatishwa tamaa licha ya maneno ya hovyo juu yao.
Imekuwa kawaida ya baadhi yetu mtu anapokomalia jambo akaambiwa, ama amenunuliwa, au anatumiwa! Msimamo alioutoa Waziri Mkuu Majaliwa umesaidia kuthibitisha kuwa maneno mengi mabaya yaliyosemwa juu ya walioitetea Loliondo yalikuwa ya husda, fitna na uongo. Sidhani kama sasa yupo wa kusema Serikali nayo ‘imehongwa’ kuutetea uhifadhi!
Lakini jambo moja kubwa nimejifunza katika mgogoro huu. Nalo si jingine, bali ni suala la kusimama imara kutetea kile unachokiamini. Tena basi, kuamini kwenyewe kusiwe kwa hisia-hisia tu, bali kuwe ni kuamini kunakotokana na facts na data.
Waziri Mkuu alipotoa msimamo kuhusu Loliondo alizisifu NGOs kama wadau muhimu wa maendeleo katika eneo hilo na maeneo mengine nchini.
Lakini kwa waliomwona wakati akizungumza, wanasema ile ‘body language’ yake ilitosha kuwafanya wataalamu wa mawasiliano kujua alikuwa akimaanisha nini. Alitumia lugha laini kuwasilisha ujumbe mzito. Haikushangaza baadhi ya waliohudhuria hadi leo hawajajua kama kuna eneo linatengwa na kulindwa kisheria!
Mimi sina ugomvi na NGOs. Waziri Mkuu anajua mambo mengi sana kuliko sisi wengine. Tunayo Serikali ambayo watu wengi wanaamini inavitumia vyema vyombo vyake vya ulinzi na usalama kupata ukweli wa mambo. Naamini kwa dhati kabisa kuwa Waziri Mkuu kwa kuvitumia vyombo hivyo mahsusi, anaelewa mengi ya kuzihusu NGOs. Juzi juzi kumesajiriwa NGO nyingine Loliondo. Hii kazi yake ni ‘kulinda ardhi ya Wamaasai’! Siyo ardhi ya wafugaji au wakulima, hapana. Kulinda ardhi ya Wamaasai! Wanaojua ardhi ya Wamaasai wanaelewa kifuatacho! Haya mambo tunaweza kuyaona mazuri na mepesi, lakini sidhani kama mwisho wake ni mwema. Ni suala la muda tutajua kama Msajili wa NGOs amefanya jambo la maana au la hatari. Kuruhusu mambo ya aina hii kunafungua mwanya kwa makabila mengine nayo kuanza kufikirifikiri namna hiyo. Hii NGO inaweza kuja na msukumo mwingine hatari kwa Loliondo. Tusubiri.
Uzoefu wangu Loliondo unanishawishi nimwombe Waziri Mkuu na viongozi wengine wakuu wa nchi yetu wasibweteke na kuamini kuwa hatua iliyotangazwa ndiyo mwisho wa kelele Loliondo. Wasiamini hivyo. Mgogoro wa Loliondo utaendelea kuwapo kwa sababu ni mgogoro wa kimaslahi. Ni mgogoro wa kiuchumi.
Masonara wa mgogoro wa Loliondo bado wapo. Tena wapo hadi serikalini. Nimhakikishie Waziri Mkuu kwamba hata Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ametulia pengine kwa sababu ya woga au heshima kwake Waziri Mkuu.
Nitaomba mniwie radhi, lakini ukweli ni kuwa Gambo hajawahi kuwa upande wa wanaolinda maslahi mapana ya Serikali kwenye mgogoro wa Loliondo. Mbunge wa Ngorongoro, William ole Nasha na Gambo lao ni moja. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Methew Siloma yumo kwenye kundi hili. Maanda Ngoitiko, Tina Timan na wengine- wote ni genge moja.
Tena basi, nitumie fursa hii, kwa heshima kabisa nimwombe Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala, awe makini na kina Gambo na Nasha. Watakapomshauri achanganye na zake. Mwanzoni aliwasikiliza, lakini naona ameanza kuujua ukweli. Amsaheme Profesa Alexander Songorwa, kwa sababu msimamo wake, kama mmoja wa wahifadhi mahiri nchini ndiyo matokeo haya yaliyotangazwa na Waziri Mkuu.
Nimhakikishie Waziri Mkuu kuwa watu hao niliwawataja, na wengine, wataendelea kufanya vikao vya wazi na vya siri. Watapita vijijini kuhamasisha vuguvugu jipya. Haitashangaza tukiona mabango na maandamano. Ninavyoandika, wapo walioanza kazi hiyo.
Sisi tunaofuatilia Loliondo tunajua kwanini baadhi ya watu walikomaa kuanzishwe WMA licha ya kutambua kuwa haiwezi kuanzishwa katika ardhi isiyo ya kijiji. Tunajua walijiandaa vipi kufaidika kwenye WMA. Tunajua walio nyuma ya uanzishwaji wake. Hawa hawa wamekaa kimya ilhali wakitambua kuna kijiji kimempa mwekezaji kutoka Afrika Kusini ekari 25,000 (elfu ishirini na tano) ili afanye utalii wa picha. Wanajua ukomo ukubwa wa ardhi inayopaswa kutolewa na kijiji. Nchi hii yenye vijiji takribani 15,000 kila kimoja kikiamua kuingia mkataba na mwekezaji mgeni kitabaki kitu gani?
Wageni hawa wanakilipa kijiji dola 100,000 pekee kwa mwaka (Sh milioni 220 hivi) na nyingine 12,500! Mkataba wa miaka 15. Serikali haipati chochote! Wao wanapata nini? Ni siri yao na watetezi wao. Naamini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa kuwa yuko kwenye timu ya wizara za kisekta kuhusu Loliondo, atahoji na kupewa majibu ya aina hii ya uwekezaji. Ajiandae kupambana na vikwazo kwa sababu watetezi wa mwekezaji huyu ni kina Gambo na ni hao hao wanaompigia debe ili afunguliwe uwanja wa ndege uliofungwa kwa sababu za kiusalama. Unakuwa na uwanja wa ndege karibu na jiwe la mpaka wa nchi na nchi hapo unatarajia nini?
Mgogoro wa Loliondo utaendelea kufukuta kwa sababu kuna maelfu ya ng’ombe wanaingizwa nchini kutoka Kenya. Kenya hakuna kipande cha ardhi ya umma! Wanajua Tanzania ni kama haina mwenyewe. Mifugo kutoka Kenya ikizuiwa maana yake kuna Watanzania na Wakenya wanakosa pesa. Hawa hawatakaa kimya. Hawatakubali kwa urahisi kuweka alama mifugo yao. Wataipinga Serikali.
Vijiji vya Njoroi na Soitsambu katika Kata ya Soitsambu vinavyopakana na Kenya ni lango la uingizaji mifugo na wahamiaji haramu. Hakuna Kituo cha Polisi wala Uhamiaji. Wapenda migogoro hawatakubali kuona huduma hizo zikiwekwa hapo maana wanajua kwa kuziweka, uchumi wao utakuwa umevurugwa.
Wapo wanaodhani kuwa tunatetea uwepo wa Loliondo kwa sababu ya mwekezaji OBC. Hii ni sababu ndogo sana katika hoja pana zaidi ambayo ni uhifadhi. OBC hapa si kwao. Wao ni wageni. Wameikuta Tanzania na wataiacha. Wamekuja na kuna siku wataondoka. Tutakuwa hatuna busara kuamini kuwa tuna haki ya kuivuruga Loliondo kwa sababu ya kuwakomoa OBC. Wanaompinga mwekezaji huyu wanampinga kwa makosa gani?
Mwalimu Nyerere, katika kitabu chake cha Tujisahihishe anasema haya: “Mtu ambaye kapewa nafasi ya kuweza kuona anapofanya mambo kama kipofu hukatisha tamaa zaidi kuliko kama angekuwa ni kipofu kweli… Kipofu akinivamia na kuniumiza, nikikasirika kwa sababu ya maumivu aliyonitia ni jambo la kibinadamu, lakini nikijitoboa macho ili na mimi nimvamie na kumwumiza haitakuwa nimefanya jambo la busara.”
Naam, hatuwezi kuwachukia OBC kwa kuiharibu Loliondo. Leo kuna visima vingi sana vimechimbwa na wawekezaji, lakini NGOs na viongozi maharamia wamewashawishi wananchi kuvihujumu. Fikiria, kisima kimegharimu Sh milioni 50 kinaharibiwa na kuwafanya kina mama maskini watembee umbali mrefu mno kusaka maji. Hapa anakomolewa nani? Hii ni dhambi. Haya yapo Oloipir na katika vijiji vingi.
Kuna genge la wachochezi wasiokuwa na huruma. Wako radhi kuhamasisha wananchi waharibu miundombinu ya huduma za kijamii zilizowekwa na wawekezaji ili kuonyesha kuwa hawana manufaa nao. Hawa wanajulikana na hawatakaa kimya.
Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha dhamira ya dhati katika suala la uhifadhi. Ni wajibu wetu kuendelea kuiunga mkono na kuwasema wote wenye nia ovu ya kufifisha juhudi hizo.
Jambo muhimu ni kumwomba Waziri Mkuu asiamini kabisa kuwa mgogoro wa Loliondo umeisha. Alimradi manabii wa migogoro wakiwa bado wapo, kinachotakiwa ni kuwa makini nao. Serikali isilale. Ifuatilie hatua kwa hatua na ikiwezekana baadhi ya mambo yadhibitiwe kabla ya kukomaa. Serikali itachafuliwa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa. Itatukanwa. Itaandamwa. Itapewa majina yote mabaya. Isiyumbe. Muhimu ni kuwa imeamua kutenda jambo jema kwa wana Loliondo, Watanzania na wahifadhi wote duniani. Imeamua kuilinda Ikolojia ya Serengeti kwa sababu bila kufanya hivyo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti itakufa.
Namshukuru Mungu kuona kuwa jambo nililokuwa sehemu ndogo tu katika kulipigania, limetimia. Uhifadhi umeshinda. Angalizo kwa Serikali: Isijiaminishe kuwa mgogoro Loliondo umeisha. Kazi ndiyo kwanza imeanza.