Na Deodatus Balile, Zanzibar

Wiki iliyopita imekuwa wiki ya furaha kwa tasnia ya habari. Ni wiki ya furaha baada ya Alhamisi iliyopita Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, kutangaza kuyafungulia na kuyapa leseni magazeti manne; Mwanahalisi, Tanzania Daima, Mawio na Mseto. Magazeti haya yamefungiwa kati ya mwaka 2016 na 2018. Tanzania Daima leseni yake ilifutwa kabisa.

Aprili 6, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza vyombo vya habari vifunguliwe. Kwa bahati mbaya, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbas, mwandishi mwenzetu, akaitafsiri vibaya kauli na maelekezo ya Rais Samia, akasema ameelekeza zifunguliwe TV za Mtandaoni.

Sitanii, kuanzia hapo kilio kikawa kikubwa. Nikumbushe tu kuwa Juni 28, 2021 nilishindwa kwenda kumzika aliyekuwa mkurugenzi mwenzengu kwenye Kampuni ya Jamhuri Media Limited, Mkinga Mkinga na kulazimika kuhudhuria mkutano kati ya wahariri na Rais Samia. 

Niliwasilisha hoja 14 ikiwamo hii ya kuomba magazeti yafunguliwe. Tena kwa kupiga magoti mbele ya Rais Samia.

Rais Samia alisema magazeti ambayo yameishamaliza adhabu yafunguliwe na sheria ziangaliwe upya kuhakikisha zinakuwa wazi. 

Tangu wakati huo, tumefanya vikao zaidi ya 30. Tulianza na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa. Tuliwasilisha hoja zetu, akasema anazifanyia kazi.

Septemba 13, 2021 Rais Samia akahamisha Idara ya Habari kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwenda Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Wizara hii sasa ikawa inaitwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Akateuliwa Dk. Ashatu Kijaji, tukaanza naye mazungumzo. Ilifikia hatua Desemba, mwaka 2021 tuliamini magazeti yanafunguliwa kabla ya mwaka mpya.

Sitanii, Desemba 28, 2021 aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, akachafua hali ya hewa. Akasema nchi itauzwa kwa mikopo. Vuguvugu likawa kubwa hadi akajiuzulu. Januari 8, 2022 Rais Samia akafanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Nape Nnauye akateuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Mazungumzo yakaanza upya.

Ikumbukwe awali Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lilikuwa limewasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria kwa Waziri Dk. Kijaji. Hii ilikuwa ni Novemba 16, 2021. Msomaji unaweza kuona mlolongo ulivyokuwa mrefu. Hata hivyo, ifahamike kuwa katika mapambano haya Jukwaa la Wahariri halikuwa peke yake. Lipo Baraza la Habari Tanzania (MCT) na wadau wengine.

MCT walifungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki, ambapo Gazeti la Mawio lilishinda kesi mwaka 2017. Kwa bahati mbaya, Dk. Abbas mara zote alikuwa akitukejeli. Akidai serikali imekata rufaa, ilhali hakuna kitu kama hicho. Nilifika mahala pa kujiuliza iwapo huyu amesahau kama aliwahi kuwa mwandishi mwenzetu. Anyway, tunamtakia kila la heri katika utumishi wake uliotukuka.

Niruhusu niseme kidogo juu ya Waziri Nape. Nimeulizwa maswali mengi juu ya Nape. Baadhi wanasema ndiye aliyesimamia kutungwa kwa Sheria ya Huduma za Habari (MSA) ya mwaka 2016. Wakasema kwake itakuwa vigumu kuibadili sheria hii. Nimekuwa nikiwafafanulia wenye mawazo haya kuwa inawezekana wanamwonea Nape.

Nape nilifanya naye kazi mwaka 2016. Nafahamu shida aliyokuwa anaipata juu ya sheria hii. Nilifanya naye kazi Machi, 2017 baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuvamia Clouds Radio/TV. Nilimwona Nape alivyovipenda vyombo vya habari. Nimefanya naye kazi katika suala hili la magazeti, ambapo siku anayarejeshea leseni amesema: “Ukiwa njiani ukakutana na jiwe, unarudi nyuma kidogo, unapisha, kisha unaendelea na safari.” Ameongeza kuwa mazingira ya wakati huo na sasa ni tofauti kabisa.

Sitanii, yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Waziri Nape ameagiza ufanyike mkutano wa wadau, iundwe kamati ya wadau na serikali, kisha wote hawa wakutane na kujadili hizi sheria zinazolalamikiwa na kufikia mwafaka. Binafsi naona hii ni fursa. Tunao umoja wetu wa Haki ya Kupata Habari (CORI) unaounganisha mashirika 11. Huu ni wakati mwafaka wa kushirikiana kumaliza tatizo lililopo mbele yetu.

Jambo moja niliseme; Rais Samia kwa kuyafungulia haya magazeti amerejesha heshima ya Tanzania katika jamii ya kimataifa. Nina uhakika katika orodha ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (World Press Freedom Index) mwaka huu Tanzania itatoka katika nafasi ya 184 iliyopo sasa na kurejesa kwenye nafasi angalau ya 72 au juu zaidi, iliyoifikia wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.

Sitanii, vyombo vya habari si mshindani wa chama chochote katika siasa au uchumi kwa nchi. Jukumu letu la msingi ni kufikishia wananchi taarifa na taarifa za wananchi kuzifikisha serikalini. Kazi hii tunapaswa kuifanya kwa weledi, bila upendeleo, wala uonevu. Tunalenga kufika huko na mazingira anayoyajenga Rais Samia yanatia matumaini makubwa mno. Mungu ibariki Tanzania.