DAR ES SALAAM
Na Abbas Mwalimu
Mimi ni mmoja wa Watanzania waliofuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ya Mei 11, 2022.
Hakika ilikuwa hotuba iliyojaa hekima, busara na ukomavu wa kisiasa.
Mbowe ameonyesha kiu yake ya kutaka vyama vishindane kwa hoja na si matusi.
Hotuba yake imeonyesha wazi kuwa kuna haja kwa vyama vya siasa nchini licha ya tofauti zao za kiitikadi, kushirikiana kuijenga Tanzania kwa kujikita katika siasa za ‘masuala’ (politics of issues).
Lakini zaidi hotuba ya Mbowe inaonyesha kuwa kila chama kinategemea uwepo wa kingine katika kuibua hoja na kuendekeza masuala mbalimbali.
Kipekee hotuba yake imebainisha umuhimu wa vyama kuendesha siasa za kistaarabu zinazozingatia tamaduni zetu kama Watanzania na kuheshimiana.
Jambo moja muhimu ambalo Mbowe ameliahidi kwa Chadema ni kuijenga kama taasisi imara.
Katika hotuba yake, amesema:
“Tutajenga Chadema kama chama na taasisi imara yenye kutoa matumaini kwa ajili ya watu wote.”
Kutokana na hoja hii ya msingi, nami nina mambo napenda kushauri.
Kabla ya kujenga taasisi imara nadhani kuna haja kwa Chadema kufanya utafiti wa kina kubaini vyanzo vya migogoro ya mara kwa mara ndani ya chama. Hili ni muhimu hata kabla mchakato wa kujenga taasisi imara haujaanza.
Kwa nini? Kwa sababu leo watu wanafurahia akina Halima Mdee kufukuzwa, lakini wamekataa kujiuliza kuwa je, migogoro haitatokea tena? Na ikitokea inaweza kudhibitiwa vipi na mfumo ndani ya chama kwa ‘Diplomasia Zuishi’ (Preventive Diplomacy)?
Ni muhimu Chadema kufahamu kuwa migogoro huwa na vyanzo ambavyo si rahisi kuvigundua kwa haraka ingawa kile kinachofahamika kwa wengi hudhaniwa ndicho chanzo kumbe si kweli.
Kitaalamu ni kwamba migogoro mingi ina sababu zilizojificha sana. Rejea Profesa Mading Francis Deng na William I. Zartman (2011) na Combs (2011) katika kitabu ‘The Way of Conflict: Elemental Wisdom for Resolving Disputes and Transcending Differences’.
Migogoro mingi ni kama mwamba wa barafu uliopo baharini. Kile unachokiona juu ni sehemu tu ya mwamba mkubwa usioonekana. Rejea Hall (1952) katika Iceberg Model/Theory of Conflict.
Mgogoro katika sura ya mwamba uliopo baharini hutazamwa katika sura mbili. Sembdner (2011:28):
Sehemu ya kwanza ni ile ya juu ya mwamba ambayo inaonekana kwa macho na sehemu ya pili ni ile sehemu ya chini ya mwamba ambayo ipo baharini na haionekani kwa macho yetu.
Kwa waliowahi kutazama filamu ya Titanic jinsi meli ilivyogonga ule mwamba wa barafu na kukatika, watakubaliana nami namna hii ilivyo.
Kwa kawaida sehemu ya juu ya mwamba inawakilisha vitu kama muziki, lugha, hotuba, mavazi, chakula na kadhalika. Sehemu hii inaonekana kwa watazamaji.
Sehemu ya pili ambayo huwa haionekani kwa mtazamaji/watazamaji huwakilisha imani, itikadi, dini, falsafa, motisha, uvumilivu dhidi ya mabadiliko, tabia za mawasiliano, saikolojia ya maisha, utayari, katiba, uongozi na kadhalika.
Ingawa vitu hivi havionekani, vinahitajika kuvifahamu ili kutambua sehemu ya mgogoro isiyoonekana kwa kuwa hivi ndivyo vianzilishi vikuu au vichochezi vikubwa vya migogoro katika jamii kama ilivyoelezwa kwenye ‘iceberg model’ (Rothlauf, 2009:25).
Kwa kusisitiza, Schrumpf (1997:68) alieleza:
“Hidden interests are often layered. The first layer may be fears or beliefs founded in prejudice and stereotypes. This layer often offers little to bring the disputants together because the fears and beliefs are rarely shared. Under this layer are the real interests, which are based on the psychological needs foe belonging, power, freedom, and fun.”
Kutokana na ukweli huo, binafsi ninaamini kuna haja kwa Chadema kufanya utafiti wa kina kubaini vyanzo vya migogoro hatimaye kuijenga Chadema kama taasisi imara.
Katika kusisitiza umuhimu wa kufanya utafiti wa kina, ninaainisha baadhi ya rejea zilizobainisha vyanzo vya migogoro ndani ya vyama vya siasa katika nchi mbalimbali Afrika kama ifuatavyo. Nitaacha sababu hizi katika lugha halisi ili kila mmoja auone uhalisia wake:
Akindele (2011), Aleyomi (2013), Alli (2015), Chukwuma na Ali (2014), Chukwumerije (2009), Jinadu (2015), Momodu na Matudi (2013), Okoosi-Simbine (2005) na Olaniyan (2009) wote kwa ujumla wametaja vyanzo hivyo kuwa ni ‘paucity of ideology, absence of internal democracy, incumbency factor, goal incompatibility, godfatherism, politics of self-interest etc’.
Ukitazama hivyo vyanzo vinajikita katika maeneo makuu mawili ambayo ni kukosekana kwa itikadi sahihi na demokrasia ndani ya chama.
Rubin na wenzake (1994) waliainisha vyanzo vya migogoro ya ndani ya vyama vya siasa kuwa ni upendeleo kwa baadhi ya wanachama na kuwatenga wengine, kukosekana kwa mgawanyo sawa wa rasilimali ambapo kiongozi mkuu hupata mgawo mkubwa kuliko wengine, na nguvu ya mamlaka kuegemea upande mmoja wa juu tu.
Kukosekana kwa mgawanyo mzuri wa rasilimali na mamlaka kuegemea upande wa juu tu husababisha ‘tatizo la kiuongozi’ kama walivyobainisha Shale na Matlosa (2008) katika andiko lao ‘Managing Intra-Party and Inter-Party Conflict in Lesotho’ waliposema:
‘No single party in Lesotho seems immune from conflict related to leadership. But in some parties these conflicts tend to be covert, while in others, they are more overt and in public domain,’ (Shale na Matlosa, 2008:27).
Shale na Matlosa (2008:13) vilevile waliainisha vyanzo vya migogoro ya ndani ya vyama vya siasa kama walivyoainisha Rudin na wenzake (1994) lakini wao wakiongezea suala la kukosekana kwa mikutano ya mara kwa mara kwa mujibu wa katiba za vyama mahali ambapo mapato na matumizi ya vyama, uendeshwaji wa vyama, malengo na matarajio hujadiliwa kwa pamoja na kwa uwazi.
Kukosekana kwa mikutano au mikutano kutokuwa na ajenda muhimu kunanyima nafasi kwa wanachama kujua nini kinaendelea katika chama hivyo kuleta mgogoro.
Kukosekana kwa uwazi katika mapato na matumizi ya vyama vya siasa kunakotokana na udhaifu katika uendeshaji wa vyama vya siasa Afrika kunachangia pia kutokea kwa migogoro kama walivyoonyesha hofu yao IDEA (2007:85):
‘It is difficult, almost impossible, to advocate prudence in the management of public finances of political parties or require a certain level of financial accountability and transparency in the manner in which political parties are managed is not adequately understood.”
IDEA (2007) waliongezea hofu yao juu ya kukosekana kwa ajenda za msingi kwa baadhi ya vyama vya siasa Afrika ambapo husababisha kutokea migogoro ya ndani. IDEA walieleza:
“…African political parties are yet to own the political agendas and programmes,” (IDEA ,2007:9).
Kukosa ajenda za msingi kwa vyama vya siasa husababisha kutokea kwa migogoro ya ndani ya vyama hasa panapotokea baadhi ya wanachama kuhitaji uwepo wa ajenda maalumu ambayo/ambazo chama kitazibeba kama msingi wa kujitofautisha na vyama vingine na kuandaa sera mbadala ya kuiuza kwa wananchi.
Rejea, ‘Political Parties in Africa: Challenges for Sustained Multiparty Democracy. International Institute for Democracy and Electoral Assistance 2007’.
Mbali na sababu hizo zilizoainishwa hapo juu, Okoli (2001:3) aliongezea vyanzo vingine vya migogoro ya ndani ya vyama vya siasa, kuwa ni tofauti baina ya mtu na mtu, kugongana kwa masilahi, kutokufungamana kwa itikadi au mtazamo.
Nao Okonkwo na Unaji (2004) katika andiko lao ‘Intra-Party Conflict and Prospects of Democratic Consolidation in Nigeria’, walieleza vyanzo vya migogoro ya ndani ya vyama vya siasa, wakiainisha vyanzo vya migogoro kwa kuangalia namna baadhi ya wanasiasa wanavyogombea nafasi ya madaraka (Hobbesian character), tabia za ndani za chama ambazo hutokana na udhaifu katika muundo, mfumo na utendaji kazi wa taasisi yaani chama, nidhamu hafifu na utii, na kukosekana kwa sera au itikadi ya chama.
Mbali na hayo Okonkwo na Unaji (2016) waliainisha tabia ya ‘uungu-mtu’ (godfatherism) na cabalism kuwa nazo huchangia kuwepo migogoro.
Sambamba na hilo, Okonkwo na Unaji (2016) pia waliongezea sababu nyingine kuwa ni malengo, matamanio na matarajio ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa hukinzana na malengo ya wanachama na kuzaa makundi na mtifuano wa ndani ya chama.
Kwa upande wa Mbah (2011:9) anaamini kuwa migogoro inatokana na baadhi ya wanasiasa kutaka kutumia nafasi walizo nazo katika vyama kujikusanyia nguvu ya kisiasa ili kujiongezea nafasi ya kuwa na nguvu ya kiuchumi.
Kwa maana nyingine, siasa kwao ni nyenzo ya kujipatia nguvu ya kiuchumi. Hali hii huzua migogoro ndani ya vyama vya siasa.
Kwa maoni yangu ni kwamba licha ya kwamba vyanzo hivi vya migogoro vimeainishwa kutokana na tafiti zilizofanywa Nigeria, Lesotho na Afrika kwa ujumla lakini kwa namna moja au nyingine naamini miongoni mwa vyanzo hivi vinaweza kuwa visababishi vya migogoro ya ndani ya vyama vya siasa nchini Tanzania kikiwamo Chadema, kwa sababu vyanzo hivi Afrika hufanana.
Hivyo kwa ushauri wangu naamini kuna umuhimu kwa Chadema kutilia maanani tafiti na kuzifanyia kazi ili kuepusha kutokea kwa migogoro hapo baadaye.
Historia inaonyesha kuwa karibu vyama vyote vya upinzani nchini vimewahi kukumbwa na migogoro ya ndani kama ilivyowahi kuainishwa na Nyirabu (2002):
“In Tanzania for example, almost all… parties have experienced internal crises which have left the parties weak and fragmented.”
Hivyo naamini hoja si Chadema kujenga taasisi imara tu bali kuanza kufanya utafiti wa kina kubaini migogoro ya mara kwa mara inasababishwa na nini na kuitafutia suluhisho la kudumu ili isijirejee.
Mwandishi wa makala hii, Abbas Mwalimu, ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na diplomasia anayepatikana kwa simu 0719 258 484