Mpendwa msomaji, niwie radhi wiki hii nalazimika kuandika SITANII ndefu kidogo, na SITANII ya leo itakuwa na vionjo tofauti na zilizotangulia. Nitangaze maslahi pia, kuwa katika hili ninayo maslahi nitakayoyaeleza punde, lakini nitangulie kusema nampongeza na kumshukuru Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Sitanii, Agosti 16, 2016 nilikuwa Dodoma. Ilikuwa saa 6:00 mchana, nikapokea simu ya Mheshimiwa Lukuvi. Akaniambia, “Sasa tukutane Bukoba tarehe 18, tukasikilize malalamiko yenu ya ardhi, nakwenda Bukoba.” Moyo wangu ulipiga paa! Nikajiuliza nifanyeje. Nikatize ziara ya Dodoma nipitilize hadi Bukoba au nirejee Dar es Salaam usiku huo kwa ajili ya kuchukua nyaraka zinazohusiana na mgogoro huo kisha nitafute usafiri wa Dar es Salaam- Bukoba?

Nilikuwa na Mkurugenzi mwezangu katika Kampuni ya Jamhuri Media Limited, Manyerere Jackton. Tulishauriana na kukubaliana nirejee Dar es Salaam nichukue vielelezo (yeye aliviita vitendea kazi), kisha nianze safari ya Bukoba. Nilikwenda ofisi za Kampuni ya basi ya Shabiby, bahati nzuri nikapata basi la saa 10 jioni.

Nilipanda basi hilo, tukafika Dar es Salaam saa 6:30 usiku. Gari nililoagiza lije Ubungo kunipokea, dereva Sylivester Kabendera akaniambia limeharibikia Buguruni. Nilianza kuona majaribu mengi katika safari hiyo. Nilichukua teksi hadi Buguruni. Nilimwamsha fundi mmoja wa umeme wa magari, alipofika akasema pampu inaelekea ina tatizo, hivyo akatuunganishia “mchuzi juu”.

Sitanii, hadi nafika nyumbani muda ulikuwa yapata saa 8:00 usiku, kwa maana kwamba ni alfajiri ya Agosti 17, 2016. Nililala saa 1:30, hivyo ilipofika saa 9:30 nikaamka. Nikaoga, nikapakia mizigo na vitendea kazi. Nilimwamsha Kabendera tukachukua gari na kwenda Uwanja wa Ndege. Saa 12 asubuhi safari ya Dar es Salaam – Mwanza ilianza na saa 1:17 tayari tulikuwa Mwanza.

Mwanza nilikwenda ofisi za Auric airline nikapata tiketi ya Bukoba, ambapo tuliondoka saa 2:30 na baada ya dakika 45 kwa maana ya saa 3:15, tulifika Bukoba. Niliwasiliana na Josephat Kaijage, na maafisa kadhaa kuangalia tumejipangaje kuwasilisha hoja yetu ya kupinga uporaji wa ardhi ya kijiji chetu cha Nyanga eneo la Nyamyalilo tukipata nafasi mbele ya Waziri Lukuvi.

Sitanii, nikiri kwamba kwa muda mrefu na kwa kushirikiana na wanakijiji tuliwasilisha malalamiko yetu kwa Waziri Lukuvi kueleza jinsi mwekezaji George Rogers maarufu Malisizo, alivyopora ardhi ya wananchi wanyonge na kwa kutumia wanasheria akawa anatumia uwezo wa kifedha alionao kutisha na kupiga wananchi.

 

Historia ya mgogoro kwa ufupi

Mwaka 2005, Rogers aliwasiliana na uongozi wa Kata ya Nyanga akiomba eneo la kujenga kiwanda cha kusindika nyama. Uongozi ulimpatia ekari tano eneo la Nyamyalilo, huko Nyanga, kwa mujibu muhtasari uliopo. Kwa bahati mbaya, wananchi hawakushirikishwa katika uamuzi huu wa kugawa ardhi ya kijiji iliyokuwa sehemu yake inamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia.

Kama hiyo haitoshi, Rogers alianza kuvamia maeneo ya watu wenye kumiliki ardhi Nyamyalilo huko Nyanga, tena kwa jeuri ya ajabu. Mwanzoni, watu wengi walichukulia uvamizi wake na wanaompiga kama masuala ya kisiasa. Mimi ni mmoja wa watu ambao awali tuliamua kutoingilia suala hili maana liliingizwa katika itikadi za kisiasa, kwani kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 na mwaka 2015 lilikuwa kombe la kisiasa.

Sitanii, ukiacha karata za kisiasa kati ya mwaka 2010 na 2015 mbali na kupoka maeneo ya wananchi zaidi ya 160, Rogers aliwafungulia kesi wananchi 40, aliodai wamemvamia (wakati yeye aliwakuta) akawadai fidia ya Sh bilioni 1.66. Kwa wananchi wa kawaida hili lilikuwa tishio kubwa. Mara kadhaa walinipigia simu kuomba ushauri.

Baadhi walinieleza kuwa wana mpango wa kuhama kijiji kumkimbia Rogers aliyekuwa akiwatisha kwa vifungu vya sheria kila kukicha. Nilitumia maneno ya Biblia kwao kuwaambia kwamba “MSIOGOPE.” Tuliendelea kukusanya ushahidi na kuuwasilisha serikalini na katika vyombo mbalimbali kuthibitisha kuwa Rogers siye anayeporwa, bali yeye anawapora wananchi.

 

Mkutano wa Agosti 18, 2016

Waziri Lukuvi ilipofika saa 5:00 asubuhi siku ya Agosti 18, 2016 alifika na msafara ukiongozana na Mkuu wa Mkoa mpya wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu) Salim Mustafa Kijuu, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo, na wakuu wa wilaya za mkoa wa Kagera na viongozi wengine.

Baada ya utambulisho, Lukuvi alisema amefika Bukoba kusikiliza kero za ardhi na hivyo wananchi wawasilishe kero zao azipatie ufumbuzi. Alianza na kero ya mama mmoja aliyekuwa ameporwa kiwanja na watendaji wa halmashari na wakawa wanamzungusha miaka mingi bila kumpatia ufumbuzi.

Sitanii, Lukuvi aliagiza mama huyo apewe kiwanja ndani ya mwezi huu na akampa namba yake ya simu ya mkononi kuwa iwapo asingepewa kiwanja, amjulishe naye ashughulike na maafisa ardhi wanaomzungusha. Taarifa nilizonazo, Agosti 19, 2016, yaani siku moja baadaye mama huyo alipewa kiwanja.

Alipomaliza shauri la mama huyo, Waziri Lukuvi akasema: “Ehee, na wewe Balile umekuja kufanya nini Bukoba? Unalo la kueleza?” Nilisimama na kumshukuru, ila nikamwambia yupo mtu tuliyemwandaa kulizungumzia tatizo letu, Mzee Kaijage na mimi nitajazia mapengo. Akaridhia. Mzee Kaijage alisimulia historia ya mgogoro wa ardhi Nyanga eneo la Nyamyalilo dhidi ya mwekezaji George Rogers ulivyoanza, alivyotesa wananchi, vitisho anavyowapatia na tambo alizonazo kuwa Serikali iko mikononi mwake.

Mzee Kaijage alipomaliza kueleza, niliongeza ufafanuzi kwa kueleza kuwa ilipofika Februari mwaka huu, Rogers ameongeza upana wa eneo alilotaka kupora, akavamia mashamba ya wananchi likiwamo langu lenye miti niliyoipanda mwaka 1993 na kwa jeuri ya aina yake, anatwambia kuwa anachukua hiyo ardhi kisha angetulipa fidia ya Sh 300 kwa kila mita ya mraba.

Si hilo tu, tulipomhoji miti yetu iliyokomaa kiasi kile hatima yake ikoje, Rogers akasema angetupatia ruhusa ya kukata miti iwapo itakomaa kisha tuondoke. Kati ya mambo niliyoongeza ni kumtaka Rogers atoe ufafanuzi juu ya uhalali wa ukubwa wa eneo alilodai kumiliki.

Kata ya Nyanga ina mitaa mitano; Ihyolo, Nyarubanja, Kyakailabwa, Rubumba na Kyamyosi. Nilisema kwa takwimu kuwa ukubwa wa eneo lote hilo la mitaa mitano linalounda Kata ya Nyanga, ni ekari 1863. Mwekezaji ameghushi nyaraka, anaonesha katika mtaa mmoja tu wa Ihyolo, ambapo lipo eneo analovamia makaratasi yake yanaonesha anamiliki ekari 2016.

Sitanii, nilieleza kuwa hii ilikuwa ajabu kuliko ajabu zote kwani labda kama anamiliki baadhi ya viwanja angani na kwamba iwapo madai yake yana ukweli, basi anamiliki kata nzima ikiwamo mashamba yetu, nyumba zetu na shule zote mbili; ya msingi na sekondari.

Baada ya maelezo hayo, Waziri Lukuvi alihoji iwapo Rogers alikuwapo kwenye mkutano huo au mwakilishi wake. Kwa mbwembwe, Rogers alijitokeza akiwa mkononi ameshika ufunguo wa gari aina ya Prado akiuchezesha. Waziri alimtaka aeleze alivyopata ardhi. Kwa mbwembe huku akichomekea Kiingereza, alisema alipewa ardhi hiyo kihalali na hata Diwani wa sasa wa Kata ya Nyanga, Deusdedith Mutakyahwa, alikuwa mwajiriwa wake.

Alianza kueleza mambo mengi, yaliyofanya wananchi waanze kumzomea, na Waziri Lukuvi akawataka wananchi wakae kimya. Waziri Lukuvi kila alichomhoji Rogers alisema hana, alipoulizwa yeye kutokuwa na hivyo vielelezo ni kosa la nani, akasema: “Serikali ndiyo inayopaswa kulaumiwa kwani ilikuwa na jukumu la kubadili sheria haikufanya hivyo, na hivyo haikunipa hayo unayosema.”

Mwisho kabla hajatoa msimamo, Lukuvi alimuuliza Rogers: “Wewe ni raia wa Tanzania?” Akasema: “Mimi ni British.” Baada ya kauli hiyo, Waziri Lukuvi akatoa msimamo uliorejeshea wananchi haki iliyotaka kupotea, kama ifuatavyo:-

 

Kauli ya Lukuvi

Kila mwezi barua ilikuwa inakuja. Mimi sikujua nilifikiri niii…, kumbe ni ardhi ya mjini. Sasa nataka nikumbushe Mheshimiwa RC na viongozi. Nataka niwasomeshe darasa nyie mliopo hapa, ili wawekezaji kama hawa wakija mjue wanapaswa kufuata utaratibu gani.

Kwanza, umilikishaji, kwa maelezo ya mwekezaji na maelezo ya mlalamikaji, umilikishaji wa kiwanja Na 1 hiki Kitalu B, alichokisema, Nyanga, haukufuata utaratibu za uwekezaji. Hiyo ndiyo ‘opinion’ yangu. Kwa hiyo umilikishaji huu, nakwambia wewe hapo usoni, mimi kama Waziri ardhi mwenye dhamana nchi hii, umilikishwaji ulio nao wewe ni batili (makofi na wananchi kushangilia).

Na sababu zangu ni hizi, maana mimi huwa sina, sina kona. Nakwambia nakuangalia usoni. Sababu za ubatili wa umiliki wako ni hizi zifuatazo. Kwanza kampuni iliyomilikishwa ardhi ni kampuni ya kigeni, na kwa mujibu wa kifungu cha 19(2) cha Sheria ya Ardhi kinasema Kampuni ambayo hisa zake nyingi zinamilikiwa na wageni, ni kampuni ya kigeni.

Kwa hiyo kwa sababu kampuni yako ni ya kigeni na kwa Sheria ya Ardhi Kifungu cha 19(2) inaruhusu kampuni ya kigeni kupewa ardhi moja kwa moja kupitia Kituo cha Uwekezaji, yaani TIC, kwa hiyo wewe, na mimi nimeishatoatoa sana… Ulipaswa uwe na hati isiyoandikwa kwa jina lako Rogers and Family au nani, ulipaswa uwe na leseni na licence au hati iliyoandikwa TIC kwa sababu wewe ni mgeni tunakupangisha tu, chini ya dhamana ya TIC. Huna.

Na ili upate hiyo, fungu la 20(1) linasisitiza ili ardhi iweze kutolewa kwa Mwekezaji, Mheshimiwa RC hili ni darasa, raia wa kigeni ni lazima iwe ni ardhi ya uwekezaji, na kwa madhumuni ya uwekezaji. Haiwezi kuwa, na haitatokea chini ya Awamu ya Tano (makofi), kwamba mgeni atapita kila mahali kwenye kona ya nchi hii, atakusanyakusanya ardhi, halafu atachukua hati. Nchi hii haiwezi kutoa hati za namna hii, kweli.

Vinginevyo tunaweza tukakuta wenye pesa wote wageni wamekuja kuinunua Tanzania na tunaishi kwenye ardhi yao. Haiwezekani (makofi). Kwa hiyo sisi kama Serikali ndiyo tunaopanga, kwamba ardhi hii imeiva kwa ajili ya uwekezaji RC, ardhi hii imeiva ni ya uwekezaji, inatangazwa kwenye gazeti la Serikali. Halafu, mgeni ndiyo anakuja kuikuta.

Siyo yeye atoke kule Ulaya… kwanza hawa vibali vya ‘migration’ haviwaruhusu wageni kurandaranda mitaani (makofi). Nyie mnaruhusu namna hii? (Sauti ya Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kagera ikasema hapana). ‘Usi-take advantage’ kwamba wewe ni Mhaya unarandaranda tu na nyie hamjui uraia wake. Huyu ni Mwingereza (kicheko).

Kwa hiyo mgeni yeyote wa nchi hii haruhusiwi, kwa sheria, kurandaranda mitaani huko anakusanya eka moja moja na kuwanunua anavyotaka, kwanza hata kibali cha kuishi nchini hakimpi fursa ya namna hiyo. Kama ni mwekezaji atapata ardhi zilizotengwa na mamlaka ya Serikali na baada ya hapo utaratibu utafuatwa.

Kwa hiyo, ili ardhi iwe ni ya uwekezaji kwa mujibu wa fungu la 20 (2) inapaswa iwe imeainishwa na imetangazwa kama ardhi ya uwekezaji. La pili, mpaka leo, ofisini kwangu hakuna kumbukumbu zinazoonesha kwamba ardhi aliyomilikishwa huyu ‘foreigner’, huyu Bwana Rogers, iliishawahi kutangazwa kama ardhi ya uwekezaji.

Na haipo kwenye kumbukumbu za Mkoa wa Kagera, kwamba ni ardhi ya Uwekezaji. Lakini, hata kama ingekuwa ardhi hii imetangazwa kama ardhi ya uwekezaji, umilikishaji wa ardhi hii kwa mtu, kampuni au taasisi, ulipaswa kupitia katika Kamati ya Taifa ya Umilikishaji wa Ardhi, ambayo TIC ni mjumbe.

Sasa mimi ndiye ninayeratibu vikao vyote vya wawekezaji vya kugawa ardhi pale wizarani kwangu. Hajawahi kuomba na hajawahi kupitishwa na Kamati ya Ardhi kwa Mwekezaji katika Tanzania hii. Mgeni yeyote, lazima apitie kwenye Kamati ya Taifa ya Ugawaji Ardhi, na nyie mabwana ardhi mnajua, huu ndiyo utaratibu.

Kwa hiyo kumbukumbu za kwamba ardhi hii iliishawahi kutolewa kwa mwekezaji anaitwa Bwana Rogers, haipo. Kwa kuwa ardhi ya Kiwanja Na 1B Nyanga haukuwahi kuainishwa na kutangazwa kama ardhi ya uwekezaji, haikupashwa kumilikishwa kwa kampuni  ya kigeni, moja kwa moja kupitia kwa Kamishna au TIC kwa njia ya ‘derivative right’ (haki ya kumiliki kwa nakala) bila kupita katika Kamati ya Taifa ya Ugawaji wa Ardhi.

Lakini umilikishwaji wa ardhi hiyo kwa kampuni ya kigeni, kama itakuwa imetolewa tofauti na taratibu nilizotaja hapo juu, utakuwa umetolewa kinyume na sheria ya ardhi, hivyo miliki hiyo ni batili tangu ilipotolewa (makofi na kicheko). Na nyaraka zilizotolewa kuthibitisha miliki hiyo, ni batili tangu zilipoandaliwa. Lakini kama itaonekana vinginevyo, mamlaka nyingine za kisheria zipo.

Hivyo, kama ‘ruling’ (uamuzi) yangu mimi Bwana RC, kama Waziri ninayesimamia ardhi katika Serikali hii, na kwa ushauri niliopewa na wanasheria wangu wote na mabwana ardhi, ni kwamba hakuna miliki iliyotolewa kisheria katika Kiwanja Na 1, Kitalu B Nyanga, iwapo yupo anayehitaji kumilikishwa sasa, ni lazima ufuate masharti niliyoyataja. Unaweza kumilikishwa hata kesho, lakini fuata hiyo ‘process’.

Na kwa sababu hiyo, siyo kwamba tu eneo hili. Hukuwa na haki ya kumilikishwa Kitalu Na 1B, hukuwa na haki ya kumilikishwa viwanja ambavyo havikusemwa hapa. Wewe unamiliki vile vile ekari 60, zilizopo Bugorola, lakini pia unamiliki eneo lingine una plot kama 9 eneo la Block A Kibuye, vyote hivi ni batili (makofi/kicheko/kushangilia).

Kwa hiyo, uamuzi wangu, na nashangaa kwa nini jana umeanza kuwalipa fidia baada ya kusikia mimi nakuja. Kwa nini? Na wewe nilikufanyia uungwana, nilimwambia msaidizi wangu akupigie simu ukiwa Nairobi uje, kwa sababu sisi Serikali yetu haifanyi kazi kwa majungu. Tunafanya waziwazi na nilitaka nikuone usoni hivi, na Mwanasheria wako tukazungumza naye, nikashangaa ukasema umetenga milioni 130 za fidia.

Lakini tangu umeanza shamba lile, hela ambazo umeweza ‘kuraise’ (kukopa) kupitia benki ni milioni 50 tu. Kwa nini jana tu umepata milioni 130? Mikopo yako yote nimeiona. Ulichoweza ‘kuraise’ wewe una mkopo mmoja wa Sh milioni 50. ‘For all these years’ (kwa miaka yote hiyo) hujaendeleza, jana ghafla, umepata milioni 130 za kulipa watu, amri ya korti, lakini ninachosema ni kwamba, mimi nasema, siingilii uhuru wa Mahakama, lakini muamala huu uliokupa ardhi ndani ya Tanzania ulikuwa batili tangu ulipotolewa.

‘That is my ruling’ (huo ndiyo uamuzi wangu). Kwa hiyo namuagiza Kamishna wangu sasa wa Kanda ambaye yuko hapa [Joseph] Shewiyo, katika wiki moja awe ‘amerectify’ (amebatilisha) ardhi ile irudi ‘back to square one status quo’ (kama ilivyokuwa mwanzo) (makofi).

Bwana Shewiyo umenisikia? Katika wiki moja hii, lazima ardhi hii irudi ilivyokuwa. Na nyaraka zote zilizopo sizitambui ni batili kuanzia siku zilipotolewa. Na kama mwekezaji Rogers, unataka kumiliki unakaribishwa, lakini ‘please’ (tafadhali) fuata utaratibu huu. ‘Usi-take advantage’ kwa sababu umezaliwa huku, ni Mwingereza, alafu unaingiaingia.

Na nyie wanasheria mnaosaidia kampuni kama hizi, tafadhalini someni sheria vizuri na muwe wazalendo. Haiwezekani Waswahili wenzetu, wanasheria wenzetu mnakubali kupindisha sheria na kuwanyonga Watanzania maskini kwa maelfu kwa sababu ya kupata kamisheni nyepesi. Haiwezi kuwa (makofi).

Sasa kuna njia nyingi, kama huridhiki, lakini uamuzi wangu mimi kwa taarifa yako hii ofa yako nimeishaifuta. Na nyaraka zote zinazohusiana na ardhi nchi hii na kwa sababu nilikuwa na nyaraka zako zote hizi, hii kesi imekuja kwangu muda mrefu. Nina nyaraka zako zote za ofa, za ‘title’ iko hapa, za msajili, kila mahali. Kila mahali ulikopita nyaraka ninazo hapa.

Lakini kwa sababu nyaraka zote hizi zilianzishiwa na hati ambayo haikutolewa kisheria, kwa hiyo mimi naondoa ile ofa yangu, maana yake haikutolewa kisheria, kwa hiyo natamka kwamba [z]ile ofa zote ulizozipata katika eneo lote ni batili.

Bwana ardhi wa Manispaa, si upo? Haya sasa msaidie huyu, namna ya ‘kurectify’ hiyo ardhi kuanzia leo. Kesho kabla sijaondoka nione makaratasi. Haya.

 

Kilichofuata

Baada ya kauli hiyo nzito iliyorejesha imani ya wananchi kwa Serikali na amani katika Kata ya Nyanga, maeneo ya Bugorola, Kibuye na mengine kama Kashai, baadhi ya wananchi walipigwa butwaa wakijiuliza Waziri Lukuvi amepataje taarifa zote hizo, na baadhi wakaishia kushangilia.

Sitanii, kwa kufahamu George Rogers alivyo mkorofi, nikawasha tena kipaza sauti na kuomba kwa pamoja Waziri Lukuvi na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali (mstaafu) Salim Mustafa Kijuu, watusaidie kulinda usalama wetu kwani Rogers amejiwekea utaratibu wa kupiga yeyote anayekwaza au kuchelewesha masilahi yake.

Nilitoa mfano ambao Rogers alimpiga Mzee Josephat Kaijage ambaye ni Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Nyanga kutokana na Mzee huyo kukataa kuporwa ardhi na Rogers kwa njia zisizo halali na nikahitimisha kuwa baada ya maelezo hayo angetuletea usumbufu mkubwa na wanakijiji.

Waziri Lukuvi baada ya kusikia kauli hiyo, aligeuka akamwangalia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Augastine Leone Ollomi, kisha akamgeukia Mkuu wa Uhamiaji, Abdalla Towo, akamuuliza watu wa aina hiyo wana utaratibu gani ambapo wageni wanahangaisha wazawa.

Towo alipiga saluti, na dakika moja tu baada ya hapo akamwendea Rogers na kumweka chini ya ulinzi. Askari walimkabili na kumnyang’anya bastola mbele za watu, kisha wakaongozana naye kwenda polisi. Baadaye taarifa nilizopata, ni kuwa TIC wamemfutia Rogers hati ya uwekezaji, hivyo akapoteza sifa za kuendelea kuwa nchini na akatakiwa kuondoka ndani ya saa 24 kurejea kwao nchini Uingereza.

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa Rogers alikuwa raia wa Tanzania mzaliwa wa Kibeta, baadaye kwa maelezo aliyotoa Waziri Lukuvi katika mkutano wa hadhara, ‘alijilipua’ nchini Uingereza kwa kuukana uraia wa Tanzania akawa anaishi huko.

Haifahamiki nini kimemfanya atamani kurejea Tanzania, hata baada ya kuwa ameoa raia wa Uganda, ambaye naye aliukana uraia wa nchi hiyo na kupata uraia wa Uingereza.

Katika mkutano huo, Waziri Lukuvi alitolea uamuzi malalamiko ya wanachi zaidi ya 50, ambayo yote yalihusu kudhulumiwa viwanja, nyumba au maeneo ya wazi kuvamiwa, huku wengine wakizibiwa barabara za kuingia nyumbani kwao.

Josephat Kaijage, ameiambia JAMHURI: “Tanzania ingekuwa na mawaziri wanaofanya kazi kwa uwazi kama Mheshimiwa Lukuvi 10 tu, nchi hii ingekuwa mbali mno kimaendeleo. Watanzania wanaonewa mno, haki zao zinafinyangwa wanakosa pa kusemea. Rogers alinipiga, akanikondesha, lakini pigo alilopata leo, Mungu amemlipa hapa hapa duniani. Naomba Mungu ambariki sana Lukuvi aendelee na moyo huu wa kusaidia wananchi wanyonge.”

Kaijage alipata kufunga safari kwenda ofisini kwa Lukuvi Dar es Salaam kuwasilisha malalamiko ya Rogers kuvamia eneo la Nyamyalilo Nyanga, ambalo sasa limerejeshwa kwa wananchi na umiliki wao umeendelea kama ulivyokuwa kabla ya kuvamiwa na Rogers.

Sitanii, nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Lukuvi kwa jinsi alivyotatua mgogoro huu uliokuwa umeota mizizi na kuonekana kama jini kwenye chupa, lakini kwa uchunguzi alioufanya na busara za hali ya juu, amewezesha haki ya wananchi wanyonge kupatikana. Mheshimiwa Lukuvi asiishie Nyanga Bukoba tu, awasaidie Watanzania maeneo mbalimbali nchini kwani kuporwa ardhi ni kero kubwa kwa Tanzania.