Huu ni msimu wa tatu tangu Azam Media waanze kuidhamini Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Udhamini huo wa Azam Media Group umesaidia kunogesha msisimko wa michuano hiyo kwa kufanya timu nyingi kuwa katika mkao wa kiushindani, tofauti na misimu kadhaa iliyopita.
Klabu nyingi zimekuwa na uwezo wa kusajili na hata kuhudumia wachezaji kwa uhakika baada ya kuwa na udhamini wa Azam, ambao unawapa jeuri ya milioni 100 kila msimu. Azam Media Group sasa wameamua kuleta mapinduzi ya soka hapa Tanzania kwa kuifufua iliyokuwa michuano ya Chama cha Soka (FA) kwa kusaini mkataba na TFF wenye thamani ya bilioni 3.3.
Udhamini huo unaashiria kuongezeka kwa michuano mingine yenye ushindani mkubwa msimu huu na miaka mingine mitatu ijayo baada ya msimu huu. Udhamini huo ambao utatoa zawadi ya milioni 50 kwa mshindi wa Kombe hilo la Shirikisho ambao utashirikisha timu 64 katika mtindo wa mtoano utachangia sana kuibua vipaji vingi vya soka hapa Tanzania.
Mbali na kuibua vipaji, lakini itachangia kuboresha ushindani katika Ligi Luu ya Vodacom maana timu za Ligi Kuu zitakuwa zinapata changamoto ya kukutana katika mashindano na timu ambazo siyo za Ligi Kuu.
Katika hali yoyote timu hizo zisizoshiriki Ligi Kuu zitataka kuonesha kuwa hazipo Ligi Kuu, lakini zina uwezo mkubwa wa kutandaza soka la uhakika. Bila shaka wachezaji wake watataka kupambana kwa nguvu ili wapate fursa ya kusajiliwa na timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kombe la Shirikisho litasaidia kuibua hamasa ya soka mikoani maana hata mikoa ambayo haina timu zinazoshiriki Ligi Kuu itashuhudia timu za ligi hiyo zikitua huko na kutandaza soka la ushindani. Michuano ya Kombe la Shirikisho ambalo litashirikisha timu 64 na kucheza kwa mtindo wa mtoano nyumbani na ugenini, itatupa hata majibu ya zile hoja kwamba soka la kweli lenye ushindani lipo kwa timu zinazocheza Ligi Daraja la Kwanza.
Kwa namna moja au nyingine mashindano haya yatasaidia hata timu zinazoshiriki ligi kupata fursa ya kuona wachezaji wa kuwasajili kwa kipimo sahihi. Maana wapo wachezaji wanacheza soko la uhakika na la kiufundi sana wanapokuwa katika mashindano na timu walizonazo katika daraja moja, lakini wakisajiliwa Ligi Kuu wanapotea kwa “mchecheto” wa kukutana na majina makubwa lakini sasa watapimwa kwa kuonekana katika mashindano na timu za Ligi Kuu.
Mashindano hayo ambayo timu mwenyeji katika mechi atapewa milioni moja huku timu mgeni ikipewa milioni 3, ni sehemu muhimu ya kuziona timu nyingi ambazo zilishuka daraja na hazikuonekana tena Ligi Kuu na hapo tutapata fursa ya kujionea timu hizo kupitia runinga zetu.
Katika hili la kudhamini michuano ya shirikisho, Ligi ya Vodacom Tanzania Bara na kuleta timu yenye ushindani ya Azam FC, ni wazi kuwa Azam Media Group wanastahili shukrani za dhati kwa kuamua kuleta ushindani wa soka hapa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Nina imani kuwa Azam Media Group wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi ya hapa walipofika na ninauona huu kama mwanzo wa safari ya mapinduzi makubwa ya soka hapa Bongo. Udhamini wa Azam Media Group kwa timu yake ya Azam FC umechangia kuibua hamasa kwa wadhamini wengine kudhamini timu mbalimbali hapa nchini.
Kabla ya kuibuka kwa Azam, ilikuwa ni kawaida kusikia kila udhamini unatiririka Yanga na Simba lakini kwa sasa mambo yamebadilika na imejulikana wazi kuwa timu yoyote inaweza kudhaminiwa na kuwa bora kiwango cha kutangaza vyema bidhaa za mdhamini husika. Changamoto ya Azam FC kwa timu kongwe za Simba na Yanga imeziimarisha sana timu hizo kongwe kwa kuzifanya zifanye mambo yake kwa umakini hasa katika usajili maana wakileta dharau na wachezaji Azam wanawachukua mara moja na kuwapa heshima inayostahili.
Sanjari na Azam Media Group, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, anastahili kupongezwa kwa jambo hili na hata atakapoelekea kustaafu atapaswa kuwa na jambo la kutuambia tumkumbuke kwa hilo. Jambo la kumkumbuka Malinzi ni namna alivyomudu kufanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Azam Media Group ambao wameonesha wana dhamira ya kukuza soka hapa nchini.
Ukiacha uhondo huo wa Azam Media Group huku uwanjani kuna kijana Mbwana Samatta wa TP Mazembe ambaye analeta shauku nyingine ya soka kwa mashabiki, wachezaji na wadau wengine wa soka hapa nchini. Samatta anaonekana kuwa kijana aliyeamua kulibadili jina la Tanzania katika ramani ya soka duniani.
Mchezaji huyo wa Taifa Stars anaonesha kuwa ni mtu mwenye malengo na mtazamo wa mbele usioyumbishwa na matamanio ya muda mfupi ambayo yanapingana na malengo yake ya muda mrefu. Mchezaji huyo anaonesha dhamira ya kucheza soka huko Ulaya na si vinginevyo. Amekataa katakata kuendelea kubaki kucheza soka hapa Afrika na akili yake yote imehamia huko Ulaya na wala hataki kusikia cha kucheza klabu kubwa hapa Afrika wala usajili wa pesa nono ndani ya Afrika.
Samatta hajaonesha kukata tamaa hata baada ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka katika klabu ya CSKA Moscow ya Russia bila mafanikio. Samatta hakuanza kupiga kelele za kukataa timu za Afrika kabla hajacheza klabu kubwa hapa Afrika, lakini anasema hayo akiwa amechezea TP Mazembe kwa misimu ya kutosha, amecheza michuano ya Klabu Bingwa Afrika mara nyingi na amezitikisa nyavu katika michuano hiyo mara nyingi tu.
Hana hofu na beki yoyote hapa Afrika na amegundua kuwa uwezo wake unatosha kwenda kucheza soka Ulaya na sasa ameamua lazima akacheze soka Ulaya. Mbali na Samatta, kuna Mtanzania mwenzake pale TP Mazembe, Thomas Ulimwengu, ambaye naye anaonesha amedhamiria kwenda kucheza soka Ulaya.
Hivi karibuni amesikika akisema kuwa kuna timu kubwa inamuhitaji huko Ulaya ambayo hakuwa tayari kuitaja lakini ni wazi uwezo wake umewakuna Wazungu huko Ulaya. Hawa ni wachezaji wanaotakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa wachezaji wa Tanzania ambao wana malengo ya kufika mbali katika soka.
Wachezaji wetu wajifunze kutoka kwa Samatta na Ulimwengu katika uzalendo, kutobweteka na ujasiri. Kila mtu ni shahidi namna vijana hawa wanavyopambana wakiwa katika timu ya Taifa, wanavyojiamini na kujituma katika maisha yao ya soka. Katika ustawi wa soka letu ni lazima tuseme asante kwa Samatta, Ulimwengu na Azam Media Group.
Barua pepe: [email protected] Simu: 0715 36 60 10