Taarifa za karibuni zinaonesha kwamba watu 5,358 wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) waliokuwa kwenye matibabu, wameacha kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARVs), mkoani Dodoma.

Taarifa hizi zimekuja wakati wadau wa Ukimwi wakitafakari hatima ya uchunguzi wa sakata la kutengenezwa dawa bandia za ARV. Dawa hizo aina ya TT-VIR toleo namba (batch number oc.01.85) zilisambazwa katika mikoa ya Mara, Tanga na Dar es Salaam tangu Mei, 2011.

 

Kuwapo kwa ARV bandia na wanaoishi na virusi kuacha kutumia dawa, kunadhihirisha udhaifu uliopo ndani ya mifumo na mamlaka za serikali zilizopewa kusimamia ubora, uwepo na upatikanaji wa dawa.  Wadau kama Sikika wanaamini, pengine kuna uhusiano wa karibu kati ya uwepo wa dawa hizo bandia nchini na wanaoishi na virusi kuingiwa na hofu na kuacha kutumia dawa.


Tunaamini hayo kwa kuzingatia ukweli kwamba suala la mgonjwa kutumia dawa kwa kiasi kikubwa, linategemea imani na utayari wa mhusika. Uwepo wa dawa bandia au zisizo na ubora unapunguza imani na hivyo kusababisha mgonjwa kuacha kuzitumia na kuathirika zaidi.

 

Sakata la kuwapo kwa ARV bandia lililochukua takribani miezi minane sasa, limekuwa na sura tofauti hususan juu ya nani anahusika moja kwa moja baada ya kiwanda kinachodaiwa kutengeneza dawa hizo cha Tanzania Pharmaceuticals Industry (TPI) kukanusha kuhusika na utengenezaji, huku Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) wakisisitiza kuwa dawa hizo zimetoka kiwandani hapo.


Sikika kama mdau inathamini na kutambua juhudi za serikali za kutekeleza taratibu za kisheria ikiwamo ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara uliofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia TFDA.

Hatua nyingine iliyochukuliwa na serikali ni kukifungia kiwanda cha TPI kutokana na nyaraka zilizokutwa MSD kuonesha kuwa TPI iliiuzia MSD dawa hizo. Serikali pia iliwasimamisha kazi watendaji watatu wa MSD.

 

Usambazaji na matumizi ya dawa aina ya TT –VIR 30 toleo namba 0C .01.85 pia ulipigwa marufuku, na serikali ilizitaka mamlaka za serikali za mitaa kupitia waganga wakuu kukusanya dawa hizo bandia kutoka vituo vya huduma za afya na kwa wananchi,  na kisha kuzirudisha MSD.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na MSD, takribani makopo 8,000 ya toleo hilo kati ya zaidi makopo 12,000 yaliyosambazwa yalikusanywa. Hivyo, kwa hesabu rahisi, kuna takribani makopo 4,000 ambayo bado yapo kwenye mzunguko na ambayo hakuna taasisi yenye uhakika wa yalipo makopo hayo; kwenye vituo vya huduma ama kwa wananchi.

Serikali ililifikisha suala la ARV bandia kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) kwa uchunguzi na hatua zaidi za kisheria. Lakini, pamoja na juhudi hizo za serikali, wadau hawaridhishwi na kasi ndogo ya ufuatiliaji wa tatizo hilo hususan muda mrefu unaotumika kupeleleza.

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya DPP, jalada la kesi ya ARV bandia limepokewa na linashughulikiwa kupata mwelekeo wa nani ahusishwe na kwa kosa gani kabla ya kuachia mamlaka husika jukumu la uchunguzi wa kina.  Kwa maelezo ya ofisi hiyo, suala la ARV bandia limechukua muda mrefu (zaidi ya miezi miwili), tofauti na muda wa kawaida wa siku 14 unaotumiwa na ofisi ya DPP kushughulikia kesi mbalimbali zinazofikishwa hapo, kutokana na uzito/unyeti wa suala hilo.


Wakati taratibu hizo za kitaalamu na kisheria zikiendelea, tunaishauri serikali kutoa taarifa rasmi kwa wananchi juu ya dawa bandia (makopo 4,000) ambazo hazijakusanywa. Je, ziko vituoni au zilishatumiwa na wananchi? Kama zilishatumiwa, je, serikali ina taarifa zozote juu ya waliozitumia dawa hizo? Je, kuna madhara yoyote waliyopata kutokana na kuzitumia?


Kwa kutoa taarifa sahihi, serikali itasaidia kuwatoa mashaka wanaotumia ARV na kuwajengea imani waendelee kuzitumia bila kuathiri afya zao.  Wadau wanaamini kuwa kuwapo kwa dawa zenye ubora na uhakika kutaongeza imani kwa Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU) kuendelea kuzitumia na kuimarika afya zao.

Makala haya yameandikwa na Aisha Hamis, Afisa Programu, Idara ya VV na UKIMWI katika Shirika la Sikika