Vifo visivyotarajiwa vya wafanyabiashara maarufu wawili – Henry Nyiti na Nyaga Mawalla – vimeibua hisia tofauti miongoni mwa wakazi wa Arusha na mikoa ya kaskazini kwa jumla. Nyiti alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni iliyojihusisha na uchimbaji na uuzaji vifaa vya madini ya Interstate Mining and Mineral,s iliyokuwa na makazi yake mkoani Arusha.
Pia alikuwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Geothermal Power ambayo inajihusisha na utafiti wa uzalishaji umeme kwa kutumia nguvu za joto ardhini. Alifariki dunia wiki iliyopita mkoani Morogoro kutokana na kile kilichoelezwa kwamba ni kutokana na ugonjwa wa malaria. Kwa muda mrefu sasa, Nyiti amekuwa mkoani humo akijihusisha na uchimbaji madini ya vito, kazi aliyokuwa akiifanya pia Mererani mkoani Manyara.
Nyiti umaarufu wake ulivuka ngazi ya kawaida ya wananchi, na kujikuta akiwa mmoja wa watu wanaotambuliwa na viongozi wa ngazi za juu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali. Ni kwa sababu hiyo, imeelezwa kwamba maziko yake yaliahirishwa hadi leo ili kumpa nafasi Rais Jakaya Kikwete kuweza kushiriki.
Pamoja na Rais Kikwete, watu wengine maarufu wanaotarajiwa kushiriki maziko hayo yatakayofanyika Tengeru ni Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, ambaye anatajwa kuwa mmoja wa washirika wake wakuu. Wengine wanaotarajiwa kushiriki maziko hayo ni mawaziri akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
“Kifo cha Henry Nyiti ni pigo na athari kubwa kwa jamii yetu, kwani huyu bwana alitengeneza nafasi nyingi za ajira kwa watu mbalimbali bila kujali kabila, dini wala itikadi. Amesaidia sana katika kuchangia shuguli za kijamii kama ujenzi wa zahanati na makanisa, mfano Kanisa la Kabato Usa River…amekisaidia sana Chama Cha Mapinduzi hasa wakati wa kampeni…kila mara aliombwa msaada na kusaidia. Baba yake mzazi, Mzee Paniel Nyiti amekuwa Mwenyekiti wa CCM kwa muda mrefu katika Kata ya Tengeru,” amesema mmoja watu waliomfahamu.
Nyiti alikuwa mwanamichezo, hasa riadha na alitumia fedha zake kufadhili safari mbalimbali za wanariadha ndani na nje ya nchi. Mawalla alikuwa mmoja wa mawakili na wafanyabiashara maarufu, akiwa anajihusisha pia na masuala ya uwindaji wa kitalii na ujenzi. Anatajwa kuwa mmoja wa mabilionea vijana hapa nchini akiwa na ukwasi mkubwa uliotokana na taaluma yake ya kisheria.
Taarifa za awali zinasema alifariki dunia jijini Nairobi, Kenya, akikokwenda kwa matibabu kwa wiki kadhaa. Inasemekana Mawalla amekuwa na maradhi ya moyo na shinikizo la damu kwa kipindi kirefu cha maisha yake.
Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni bado chanzo hasa cha kifo chake kilikuwa hakijawekwa bayana na familia yake, ingawa kuna madai yasiyothibitishwa kwamba “alijiua” kwa kuruka kutoka katika ghorofa.
Vifo vya wafanyabiashara hao vijana,vimepokewa kwa hisia tofauti hasa kutoka kwa watu ambao waliweza kusaidiwa kwa namna moja au nyingine.