Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAKATI vitisho vya kimtandao vinaendelea kutajwa kuongezeka duniani, Tanzania inaendelea na juhudi za kulinda miundombinu yake ya kidijitali, kwa kuandaa kwa mara nyingine Kongamano kubwa la Usalama Mtandaoni.

Kongamano hilo linalotarajiwa kufanyika kwa siku mbili kuanzia Aprili 10 mwaka huu katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, linadhihirisha dhamira ya dhati ya nchi ya kuimarisha uimara wa mifumo ya kimtandao.

Kongamano hilo litakutanisha viongozi wa sekta, watunga sera, wataalamu wa TEHAMA, wabobezi wa usalama mtandaoni wa ndani na nje ya nchi na wadau mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, amesema Kongamano hilo litajadili changamoto na fursa katika kulinda mazingira ya kidijitali Tanzania na dunia kwa ujumla.

“Mabadiliko ya haraka ya kidijitali nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla yameleta fursa nyingi, lakini pia yamefungua mianya ya hatari za kisasa za kimtandao.

“Mkutano huu ni jukwaa muhimu la kushirikiana maarifa, kuimarisha uwezo, na kujenga ushirikiano ili kuhakikisha usalama wa mazingira ya kimtandao ndani na nje ya nchi yetu.” alisema.

Alisema kongamano hilo limeandaliwa kwa kushirikiana na wadau muhimu kutoka taasisi za serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa ya usalama mtandaoni.

Pia amesema kupitia kongamano hilo, wanalenga kuimarisha uimara wa mifumo dhidi ya hatari mbalimbali za kimtandao, kuongeza uelewa, na kuhimiza matumizi ya mbinu bora za usalama katika mazingira ya kidijitali.

Pia litagusia mwelekeo wa sasa katika masuala ya usalama mtandaoni, ikiwa ni pamoja na matumizi ya Akili Unde (AI), Ulinzi wa Taarifa, na matishio mapya dhidi ya biashara na watu binafsi.

Kadri uhalifu wa kimtandao unavyozidi kuongezeka, ni muhimu kwa biashara, taasisi za serikali, na watu binafsi kuchukua hatua za mapema za kujilinda dhidi ya vitisho hivyo na kulinda taarifa nyeti pamoja na miundombinu yake muhimu.

Kongamano hilo linaendana na Dira ya Tanzania ya kuwa na Uchumi wa Kidijitali ulio salama na wenye mafanikio.