Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda na Waziri wa Afya nchini Tanzania Jenista Mhagama, wamekubaliana kukutana Dodoma makao makuu ya wizara hiyo, kufanya mazungumzo ya pamoja ya kupanga utekelezaji wa ndoto na maono ya Makonda ya kuufanya Mkoa wa Arusha kuwa Kitovu cha Utalii wa Matibabu kwa Ukanda wa Afrika ya Mashariki.

Wakizungumza kwa pamoja mkoani Arusha Makonda amemueleza Waziri Mhagama kuwa mkoa unatekeleza kwa kasi agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kukuza utalii wa aina mbalimbali mkoani hapa.

Amesema kuwa, kupatikana kwa Hospitali itakayokuwa na huduma za kibingwa na kibobezi sambamba na madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi, kutasaidia kuwavuta watu wanaoizunguka Tanzania na raia wa kigeni kusafiri kufuata matibabu hayo mkoani Arusha na hivyo kukuza utalii na kusisimua pato la Mkoa wa Arusha.

Aidha Waziri Mhagama, amemshukuru na kumpongeza Makonda kwa kusimamia vyema utoaji huduma za kiafya mkoani Arusha ikiwemo Programu ya Kliniki yake ya afya iliyofanyika mwaka 2024, na amemuahidi kuwa atamuita jijini Dodoma, kujadiliana pamoja mkakati madhubuti wa kutekeleza maono ya kujenga hospitali mpya ya kibingwa ama kuiongezea uwezo Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ili kukidhi viwango .

Aidha kwa pamoja wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kutimiza dhamira ya Rais Samia katika kuwapatia wananchi huduma bora za kiafya.

Hata hivyo Waziri Mhagama amesema wizara yake pia ipo mbioni kuupatia Mkoa wa Arusha mashine mpya ya MRI kama sehemu ya maboresho ya utoaji wa huduma za kiafya mkoani hapa na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa mashine hiyo muhimu kwa matibabu mbalimbali.