Aliondoka kwenda masomoni baada ya kupata baraka zote za mwajiri wake. Alikuwa na lengo la kujiongezea elimu, ujuzi na maarifa na kuvitumia kulitumikia taifa lake kupitia taaluma yake ya uuguzi.
Lakini alipatwa na mshituka aliporejea kutoka masomoni akiwa amekwisha kuhitimu katika ngazi ya daktari wa falsafa lakini akaambiwa kuwa ajira yake ilikwisha kufutwa.
Kwa takriban miaka 16 sasa Dk. Mary Mulugu anahangaika kurejeshwa kazini lakini licha ya kupitia katika taasisi nyingi na viongozi wengi, wakiwamo viongozi wa dini na kisiasa, muuguzi huyo ameshindwa kupata ufumbuzi wa suala lake.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa huku akionyesha kukata tamaa, Dk. Mulugu anasema katika kuitafuta haki yake amekwisha kupita katika ofisi mbalimbali zikiwamo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Wizara ya Afya, Wizara ya Utumishi, Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam lakini huko kote amegonga mwamba kupata ufumbuzi wa ajira yake iliyofutwa akiwa masomoni nchini Canada.
Aidha, Dk. Mulugu anasema amekwisha kumuandikia barua Muhadhama Polycarp Kardinali Pengo akimuomba amsaidie kuonana na Rais Dk. John Magufuli ili amfikishie kilio chake hicho kwa sababu jitihada zake za kutaka kumuona kiongozi huyo mkuu wa nchi kupitia mifumo iliyowekwa zimeshindikana.
Kama hiyo haitoshi, Dk. Mulugu pia amelifikisha suala hilo kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ali, nako akiomba msaada ili arejeshwe kazini na kulipwa stahili zake zote kama mtumishi wa umma.
Katika barua ya Disemba 27, 2018, iliyosainiwa na Mathew Kiramia kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ilieleza kuwa waziri amewaagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kupitia upya suala hilo na kuwasilisha taarifa.
Hata hivyo, Dk. Mulugu anasema hadi hii leo bado mamlaka hizo mbili hazijatoa maelezo ya kuridhisha kuhusiana na ajira yake.
“Aidha, waziri ameagiza utoe maelezo ulibaki Canada na kuendelea kufanya kazi kwa kibali gani baada ya masomo yako kukamilika?” inasomeka sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Dk. Mulugu.
Katika majibu yake kupitia barua ya Machi 18, 2019, Dk. Mulugu anasema kuwa kwa kawaida mwanafunzi anayehitimu masomo katika ngazi ya Daktari wa Falsafa hupewa ruhusa na nchi anayosoma kufanya kazi kwa kipindi cha miaka miwili. Anabainisha kuwa kwa mujibu wa mlolongo wa masomo yake, baada ya kuhitimu mwaka 2003, alikuwa na miaka miwili ya kufanya kazi nchini Canada lakini aliamua kurejea nchini mwaka 2004.
Dk. Mulugu anasema aliporejea alipatwa na mshangao mkubwa alipoelezwa kuwa ajira yake ilikuwa imefutwa tangu mwaka 1991 na kibaya zaidi, hata faili lake la ajira lilikuwa halionekani.
Anasema awali ilikuwa shida kufuatilia suala hilo kwa sababu hakukuwa na nyaraka yoyote baada ya faili lake kupotea na ilibidi liandaliwe faili la muda ili kumwezesha kufuatilia suala hilo, jambo ambalo nalo liligeuka kikwazo, kwani mwajiri wake alidai kupatiwa faili kuu badala ya hilo la muda ili aweze kulishughulikia suala hilo.
“Niliamua kurejea ili nije kuitumia elimu na maarifa yangu kuisaidia nchi na wananchi wenzangu. Ninaumia sana kuona nikihangaika hivi wakati nilijitolea kwenda kusoma kuongeza ujuzi, maarifa na elimu ili nije kulisaidia taifa langu. Lakini kwa zaidi ya miaka 16 sasa nimekuwa nikihangaika bila kile nilichokipata kupitia masomo kutumika kama ambavyo nilikusudia kitumike,” anaeleza Dk. Mulugu alipozungumza na JAMHURI hivi karibuni.
Anasema katika mihangaiko hiyo yote, bado hajafanikiwa kuelezwa kinagaubaga kwa nini ajira yake ilifutwa na faili kupotea kabla yeye hajakamilisha masomo.
Katika barua aliyomwandikia Katibu Mkuu wa CCM Septemba 27, mwaka juzi, Dk. Mulugu anasema aliondoka nchini kwenda masomoni Canada mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya kupata ruhusa na kibali kutoka kwa mwajiri wake na serikalini kama ambavyo taratibu zinataka.
“Niliomba na kuruhusiwa kwenda masomoni katika ngazi za uzamili na uzamivu. Nilifuzu vizuri na kurudi Tanzania Machi 2014 nikiwa na shauku ya kulitumikia taifa langu Tanzania, hasa upande wa miradi na elimu kwa kina mama na watoto. Nilipojaribu kurudi kazini nilikutana na ugumu ambao kwa muda mrefu sikuuelewa mpaka mwaka 2014 nilipomwona aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Turuka,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Dk. Mulugu anasema chini ya maelekezo ya Dk. Turuka, mwajiri wake (City Council), alitakiwa kutoa msimamo wake kuhusiana na ajira yake na katika barua aliyoiandika kujibu hilo, City Council ilieleza kuwa bado inatambua ajira yake ingawa mwajiri huyo hakutaka kutambua maendeleo yake kitaaluma na alimtambulisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kama Muuguzi/Mkunga.
Kwa mujibu wa nyaraka kutoka kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, katika mgawanyo wa mali na watumishi baada ya kuvunjwa iliyokuwa Tume ya Jiji la Dar es Salaam na kuanzishwa kwa halmashauri ya jiji na manispaa tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke, Dk. Mulugu alipangiwa Manispaa ya Ilala kama kituo chake cha kazi na kutakiwa kuwasilisha nyaraka zake huko.
Lakini baada ya kufanya hivyo na kugonga mwamba, Dk. Mulugu alirudi tena halmashauri ya jiji ambayo kupitia barua yenye kumbukumbu namba DCC/1.9/36/84 ya Februari 23, 2015, Dk. Mulugu alielezwa kuwa halmashauri ya jiji ilimwandikia Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kupitia barua yenye kumbukumbu namba DCC/19/36/50 ya Julai 15, 2014 kuikumbusha ofisi hiyo kuhusu suala lake lakini katika majibu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala alieleza kuwa suala hilo halikutekelezwa kwa msingi kuwa kilichokabidhiwa kwake ni jalada la mtumishi badala ya mtumishi mwenyewe.
Ofisi ya Halmashauri ya Jiji iliendelea kufuatilia suala hilo kwa kumwandikia tena Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala barua yenye kumbukumbu namba DCC/19/36/74 ya Oktoba 20, 2014 ya kumuomba awasilishe jalada hilo ili halmashauri ya jiji ipate taarifa itakazozitumia kufanya uamuzi lakini jalada hilo halijawasilishwa hadi leo.
Usuli
Dk. Mulugu alihitimu kozi ya ukunga katika Chuo cha Uuguzi Sumve mwaka 1976. Kati ya mwaka 1988 na 1990 aliajiriwa na Halmashauri ya Dar es Salaam kama Msaidizi wa Ustawi wa Jamii ambako alifanya kazi ya kuwahudumia watu waliokuwa na matatizo ya kijamii.
Kati ya mwaka 1994 na 1988 alikwenda tena kuongeza elimu baada ya kufanya kazi kama Muuguzi Mkuu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 1984. Kati ya mwaka 1977 na 1982 alifanya kazi kama Muuguzi Mkuu katika kitengo cha Zimamoto na magari ya wagonjwa.