Baadhi ya wataalamu wa sekta ya nishati nchini, wamebainisha kuwa moja ya changamoto kuu zinazoikabili sekta hiyo hususan usalama wa nishati, ni upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uendelezaji wa miradi ya umeme.
Changamoto hiyo na nyingine kadhaa zilibainishwa hivi karibuni katika warsha ya mashauriano kuhusu uendelezaji wa sera ya usalama wa nishati kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, iliyofanyika Novemba 16, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Akifafanua kuhusu changamoto hiyo, mmoja wa washiriki wa warsha, Mhandisi Salum Inegeja kutoka Wizara ya Nishati na Madini, anasema katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati, hususan inayohusu njia za kusafirisha umeme, kunahitajika ardhi ya kutosha inayotakiwa kutengwa kwa mujibu wa sheria na hutofautiana kulingana na kiwango cha umeme unaokusudiwa kuzalishwa na mradi husika.
“Kwa mfano, mradi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 unahitaji ardhi yenye upana wa mita 90 kuanzia eneo mradi unapoanzia hadi pale unapoishia. Hali kadhalika, mradi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 220 unahitaji kutengewa ardhi yenye upana wa mita 60, wakati mradi wa aina hiyo wenye msongo wa kilovoti 132 unahitaji ardhi yenye upana wa mita 40 na ule wa msongo wa kilovoti 33 unahitaji ardhi yenye upana wa mita 30,” anafafanua Mhandisi Inegeja.
Anasema kwamba ni changamoto kubwa kupata maeneo kama hayo yasiyo chini ya umiliki wa watu binafsi, au taasisi kama msikiti, kanisa, shule na nyingine kama hizo.
Changamoto nyingine iliyotajwa kuwa inaukabili usalama wa nishati nchini, ni kiwango kikubwa cha mtaji unaotakiwa kwa uwekezaji katika ujenzi wa vituo vya umeme.
Akifafanua kuhusu changamoto hiyo, Mhandisi Inegeja anatoa mfano wa gharama za ujenzi wa mradi wa umeme wa Kinyerezi I wenye megawati 185 kuwa ni dola milioni 182 za Marekani, wakati mradi wa ujenzi wa megawati 200 za kituo cha umeme wa makaa ya mawe pamoja na ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme wa kilovoti 220 unagharimu dola milioni 460 za Marekani.
Pia, Mhandisi Inegeja alitoa mfano wa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi II wenye megawati 240 kuwa unagharimu jumla ya dola milioni 344 za Marekani, mradi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 (Gridi ya Kaskazini Magharibi kutoka Mbeya hadi Nyakanazi) unaogharimu dola milioni 663.92 za Marekani, mradi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 (Kaskazini Mashariki kutoka Dar es Salaam-Chalinze-Tanga-Arusha) wenye gharama ya dola milioni 693 za Marekani na upanuaji wa gridi kwa ajili ya mradi wa umeme vijijini, wenye msongo wa kilovoti 132 ambao unagharimu jumla ya dola milioni 805.25 za Marekani.
Aidha, changamoto nyingine zinazoainishwa ni pamoja na upungufu wa wataalamu wa ndani wanaohitajika katika kuendeleza baadhi ya miradi ya umeme, umbali mrefu kutoka katika vituo vya kuzalishia umeme mpaka kwenye vituo vya kuhifadhia umeme, ukame wa maji unaotokana na mabadiliko ya hali ya hewa katika mabwawa ya kuzalishia umeme, ambao huathiri uzalishaji wa umeme pamoja na wizi wa miundombinu ya kusafirishia na kusambazia umeme.
Awali, akitoa hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Mbadala, Mhandisi Leonard Ishengoma, alisema kuwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki zimedhamiria kuhakikisha kunakuwa na nishati ya uhakika, ya bei nafuu na ya kutosha kwa nchi hizo ili kuchagiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ukanda husika.
Anaongeza kwamba katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa, ni lazima kuwapo na sera thabiti inayosimamia pamoja na mambo mengine usalama wa nishati.
Uendelezaji wa Sera ya Mfumo wa Usalama wa Nishati imekuja kufuatia maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa 10 wa Sekta ya Nishati uliofanyika jijini Arusha Septemba 11, mwaka huu.
Sera ya Mfumo wa Usalama wa Nishati inaendelezwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya kiuchumi Afrika, ofisi ndogo ya eneo la Afrika Mashariki (UNECA) iliyopo Kigali.
Sera ya Mfumo wa Usalama wa Nishati inayopendekezwa inalenga kushughulikia changamoto zinazokabili usalama wa nishati kwa nchi washirika.