Chama cha kukopesha wanawake cha Muunganiko wa Wanawake Sekta Isiyo Rasmi Dar es Salaam (MUWASIDA) kwa kushirikiana na Kampuni ya udalali ya Namic Investment Ltd, wanatuhumiwa kuuza nyumba ya Mbegu Kangamika (72) kwa mizengwe.

Nyumba hiyo Na. 255 ipo Mtaa wa Bombani, Pugu katika Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Iliuzwa kwa mnada Machi 4, 2009 kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kufidia mkopo wa Sh 2,000,000 ambazo mke wa Kangamika, Rehema Hassan, alikopa mwaka 2007 katika SACCOS hiyo.

Kangamika anasema kuuzwa kwa nyumba yake kumetokana na Rehema Hassan (kwa sasa ni marehemu) kuomba mkopo na kuweka dhamana ya kiwanja ambacho kwa baadaye kilichukuliwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa dampo.

“Baada ya kununua hii nyumba mwaka 2006 nikiwa na mke wangu wa ndoa, Vumilia Salum, mwezi mmoja baadaye Rehema Hassan alinifuata huku Pugu na kunieleza kuwa mwanaye Abdallah naye anataka anunuliwe nyumba.

“Mimi nilikubali, nikawapa Sh 500,000 wakanunua kiwanja Pugu Kinyamwezi, eneo lile walitaka kuanzisha mashimo ya kuchimba mchanga wa kuuza,” anasema Kangamika.

Anasema uwanja huo ndio ulitumika kwenye dhamana ya mkopo wa Rehema na si nyumba yake kama inavyodaiwa.

 “Siku chache baada ya kununua kiwanja kile, aliyetuuzia alinifuata na kunieleza kuwa familia yake imekataa kuuza uwanja huo, hivyo anarudisha hela yetu.

“Alirudisha hela yote, lakini mke wangu (Rehema Hassan) alikuwa tayari amekopea Sh milioni 2 MUWASIDA,” anasema Kangamika.

Kutokana na hali hiyo, Rehema alishindwa kulipa mkopo, hivyo kusababisha MUWASIDA kumwandikia barua Kangamika ili alipe mkopo huo.

Anasema usumbufu huo ulimfanya aahidi kuwalipa MUWASIDA na kwa mara ya kwanza aliwalipa Sh 150,000 katika akaunti iliyoko Akiba Bank.

Akamtafuta na kumpeleka mkewe (Rehema Hassan) Kituo cha Polisi cha Ukonga Stakishari ili akalipe deni lililosalia.

Anasema alikosa ushirikiano kutoka MUWASIDA na kwamba baada ya kuwataka wamkamate Rehema ili alipe deni, walimjibu kuwa wanamtambua yeye, hivyo asipolipa deni hilo nyumba yake itauzwa.

Machi 4, 2009 Kampuni ya Namic Investment ilipewa kazi na MUWASIDA ya kuuza nyumba hiyo. Wakaiuza kwa Stanley Mwabulambo kwa Sh milioni 6.5.

Kangamika anasema aliinunua nyumba mwaka 2006 kwa Sh milioni 8.3. Katika moja ya vielelezo, Kangamika na mke wake wanakiri kuweka dhamana ya kiwanja ili wapate mkopo wa Sh milioni 2 kutoka MUWASIDA.

“Ofisi iliyokuwa ikitumika kwa kipindi kile ilikuwa ni ofisi ya Mtaa wa Bombani na Pugu, mimi nilikubali kwa sababu sikuwa na wasiwasi, nilijua kiwanja kipo,” anaeleza Kangamika.

Katika kesi na. 108 ya mwaka 2009 aliyofungua Mahakama ya Ardhi Ilala akipinga uuzwaji wa nyumba yake, anasema hukumu iliyotolewa haikumtendea haki kwani imempa ushindi mnunuzi.

 “Hawa watu hawana vielelezo vinavyoonyesha kama nyumba yangu iliwekwa dhamana ya mkopo, mahakama haijawahi kusikiliza upande wa mashahidi wangu wala kutaka kuona nyaraka za umiliki wa nyumba yangu,” anasema Kangamika.

Mtendaji wa SACCOS hiyo, Stewart Ishengoma, anasema walishamalizana na Kangamika.

“Huyu anasema dhamana iliyotolewa ni ya kiwanja na si nyumba, hivi kwa akili ya kawaida mtu akinunua ardhi hata vilivyoko juu ya ardhi hiyo si lazima atavimiliki?

“Sisi tunajua kiwanja alichowekea dhamana ya mkopo wa mke wake ni kile anachokaa hadi sasa, na wakati tunafanya makubaliano hayo eneo lile lilikuwa na nyumba na alikuwa anaishi ndani ya nyumba ile,” anasema Ishengoma.

Anaongeza kuwa kutokana na nyumba nyingi kutopimwa kwa kipindi hicho walishindwa kupata hati ya nyumba, hivyo kilichofanyika Kangamika na mkewe walipelekwa mahakamani kuapa.

Nyumba inayodaiwa kuuzwa ni nyumba ambayo imenunuliwa na Kangamika kwa kushirikiana na mke wake wa ndoa aitwaye Vumilia Shabani.

MUWASIDA wanaeleza kuwa hawatambui kama Kangamika alikuwa na wake wawili na kwamba wakati mke wake Rehema Hassan anafika kwenye ofisi zao kuomba mkopo hakuwaeleza hilo.

Wanasema nyumba hiyo wangekuwa wameshaikabidhi kwa mnunuzi, lakini kinachochelewesha ni kesi nyingine iliyofunguliwa na taasisi ya PRIDE ambako Rehema alikopa Sh milioni 5 na akashindwa kuzirejesha.

Kangamika alipoulizwa kama nyumba yake ina mkopo zaidi ya ule wa MUWASIDA, alisema anadaiwa na Tujijenge SACCOS Sh 400,000 yeye akiwa mmoja wa wadhamini watatu waliomdhamini mkewe. Anahoji kwanini wadhamini wengine hawafuatwi kama yeye.

Mnunuzi wa nyumba hiyo, Stanley Mwabulambo, anasema ameinunua kihalali, hivyo haoni sababu ya mzee huyo kuendelea kufungua kesi ambazo huishia kushindwa.

“Mimi nimenunua nyumba hii kihalali, walitangaza kwenye gazeti mimi nikaona, nikaenda kununua, nafikiri ni kwenye Gazeti la Daily News la Agosti 29, 2017, toleo namba 12,022,” anasema Mwabulambo.

John Shabani (75) anasema: “Inasikitisha kwa kweli siku hiyo mimi niliona watu wakiwa na fimbo huku wengine wakiwa na sime wakilazimisha mzee Kangamika atoke ndani ya nyumba hiyo kwani siyo yake.”

Jirani mwingine wa Kangamika, Morand Emmanuel (54), anasema anachofanyiwa mzee Kangamika ni dhuluma, kwani kiwanja hicho ni mali yake halali na kwamba mwanamke anayetajwa kuchukua mkopo kwa dhamana ya nyumba hiyo si mkewe wa ndoa.

JAMHURI limeambiwa kuwa sehemu ilipo nyumba ya Kangamika na kiwanja cha jirani, kuna mpango wa kujenga kituo cha mafuta. Mnunuzi anadaiwa kuahidi kutoa Sh milioni 240; na uwanja ilipo nyumba ya Kangamika ukikadiriwa kuuzwa kwa Sh milioni 170.

Vumilia Shabani (43) ambaye ni mke wa ndoa wa Kangamika, anasema amemfungulia mashtaka mumewe ya kuuza nyumba bila kumpa taarifa.