TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imemfikisha mahakamani Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, John Bogohe, kwa makosa matatu ikiwamo kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri.

Mhasibu huyo alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Devota Msofe na kusomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Suzan Kimaro.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mhasibu huyo anashtakiwa kwa makosa matatu; yakiwa ni kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri, kughushi nyaraka kinyume cha vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na ubadhirifu kinyume cha Kifungu cha 28 cha Sheria  ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.

Anadaiwa kughushi na kuwasilisha nyaraka za udanganyifu kwa kuwasilisha stakabadhi ya malipo yenye Na. 0064628 ya Julai 23, mwaka 2014 ikionyesha kiasi cha Sh milioni 10.8 alizipokea kutoka kwa Alphayo Shao, yakiwa ni malipo ya kandarasi ya ukusanyaji wa ushuru kutoka Soko la Kwasadala.

Hata hivyo, ilibainika kuwa kiasi hicho cha fedha hakikutokana na malipo ya ushuru, bali yalikuwa ni malipo yaliyolipwa na Kampuni ya Sigara kupitia Benki ya NMB, ikiwa ni malipo ya ushuru wa matangazo ya kampuni hiyo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Mbali na mhasibu huyo, pia TAKUKURU imemfikisha mhakamani hapo  mfanyabiasahara, Alphayo Shao, akishtakiwa kwa kosa la kumsaidia mhasibu huyo kutenda kosa la matumizi mabaya ya nyaraka kumdanganya mwajiri.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mfanyabiashara huyo anadaiwa kudanganya kuwa kiasi cha Sh 10,880,000 aliziwasilisha yeye na kukatiwa stakabadhi ya malipo Na. 0064628 ya Julai 24, mwaka 2014 zikiwa ni malipo ya zabuni ya kukusanya ushuru katika Soko la Kwasadala huku akifahamu kuwa haikuwa kweli.

Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Suzan Kimaro, alisema kitendo hicho ni kinyume cha Kifungu cha 30 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007. Washtakiwa wote walikana mashtaka na wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa mwezi ujao.

Kutokana na kufikishwa mahakamani kwa mhasibu huyo, TAKUKURU imetoa wito kwa wafanyabiashara kuacha kuwasaidia watumishi wa umma kughushi nyaraka kwa nia ya kufanya ubadhirifu wa mali za umma.

Kamanda wa TAKUKURU mkoani Kilimanjaro, Holle Makungu, amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa wanaofanya hivyo watambue kuwa wanapopatikana na hatia chini ya Sheria ya TAKUKURU, sheria imeelekeza kampuni ya aina hiyo kuondolewa kwenye orodha ya kampuni zinazostahili kupewa zabuni kwenye taasisi za umma.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU mkoani hapa imeendesha semina, mikutano ya hadhara na kufungua na kuimarisha klabu za wapinga rushwa 40 pamoja na kushiriki katika maonyesho saba, lengo likiwa ni mkakati wa taasisi hiyo kuelimisha umma kuhusu rushwa na madhara yake kwa wananchi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Matukio hayo yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa mujibu wa sheria, ambapo wanatakiwa kudhibiti mianya ya rushwa, kuelimisha umma, kuchunguza na kufungua mashtaka.

Kamanda Makungu amesema ni jukumu la wananchi kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa badala ya kuliacha jukumu hilo kwa taasisi hiyo pekee.