Na Tatu Saad, JAMHURI MEDIA
Mshtakiwa Abubakar Hassan (66) anayekabiliwa na mashitaka manne ikiwemo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na kughushi, amesomewa hoja ya awali katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu.
Mshitakiwa huyo amesomewa hoja za awali leo Machi 22, 2023 na wakili wa serikali Grace Mwanga mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Ferdnadri Kiwonde.
Mwanga amedai kuwa Mshitakiwa Abubakar Hassan (66), Muislam, mkazi wa Nyangao na mkulima anakabiliwa na shitaka la kughushi,kujifanya kama mtu mwingine na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.
Mwanga amedai kuwa Machi, mwaka 2014 mshitakiwa akiwa na watu wengine ambao hawapo mahakamani walijitambulisha kwa mtu anayefahamika kama Rajesh Agarway kwamba wanauza kiwanja kilichopo moshi mjini.
Amedai kuwa Rajesh alikubali kununua eneo hilo baada ya mshitakiwa na mtu mwingine ambaye hayupo mahakamani kujitambulisha kwake kama mume na mke Ebenezer mwasha.
Amedai kuwa Rajesh alikubali kwa kuingia mkataba wenye jina la Ebenezer Mwasha uliosainiwa Machi Mwaka 2014 na mshitakiwa pamoja na Rajesh Agarway. mshitakiwa alipokea cheki ya malipo ya sh. milioni 100 kama sehemu ya malipo na baadae Rajesh alilipa sh milioni 5,000,000.
Amedai kuwa wakati biashara hiyo inaendelea mshitakiwa akiwa eneo la azikiwe katika jengo la Benjamini Mkapa aliwasilisha hati feki ya kiwanja, kadi ya kupigia kura iliyoghushiwa pia alisema yeye ni mume wa Joyce Sengwaji.
Mwanga amedai kuwa wakiwa eneo hilohilo Rajesh aligundua kama hati hizo ni feki na zimeghushiwa na kutoa taarifa katika kituo cha polisi na mshitakiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani hapa Januari , mwaka huu 2023 kwaajili ya kuhojiwa.
Baada ya mshitakiwa kusomewa hoja hizo alikubali taarifa zake binafsi na kukataa mashitaka yanayomkabili.
Mwanga ameomba tarehe nyingine kwaajili ya kuanza kusikilizwa na alidai kuwa wanatarajia kuwa na mashahidi 9 pamoja na vielelezo 4.
Kesi hiyo imehairishwa hadi Aprili 6, mwaka huu kwaajili ya kuanza usikilizwaji.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka inadaiwa kuwa katika shitaka la kwanza, mnamo Machi 1, mwaka 2014 mtaa wa Azikiwe Ilala Dar es Salaam katika eneo la jengo la Benjamini Mkapa mshitakiwa akiwa na nia ovu alijipatia sh. milioni 105 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Rajesh Agarway akijifanya kuwa anamuuzi kiwanja kilichopo moshi mjini wakati akijua sio kweli.
Katika shitaka la pili inadaiwa kuwa kati ya tarehe na mahali pasipojulikana mshitakiwa alighushi hati na kujipatia hati ya kiwanja kilichopo eneo la Moshi mjini kuonesha kuwa hati hiyo imetolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mji wakati akijua sio kweli.
katika shitaka la tatu inadaiwa kuwa kati ya eneo na tarehe isiyofahamika mshitakiwa alitengeneza kadi ya kupigia kura ikionyesha kama halili imetolewa na tume ya taifa ya kupigia yenye jina la Ebenezer Shilekiromuu Mwasha wakati akijua sio kweli.
Katika shitaka nne inadaiwa kuwa Machi 1, mwaka 2014 mshitakiwa akiwa katika mtaa wa Azikiwe eneo la Jengo la Benjamini Mkapa, Ilala Dar es Salaam kwa nia ovu alijifanya kuwa mtu mingine kama Ebenezer Shilekiromuu Mwasha kwa lengo la kujipatia fedha.