Katika toleo la leo tumechapisha habari za mchakato wa kuandaa anwani za makazi (postal code) kukamilika. Mpango huu umeandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na muda si mrefu karibu kila nyumba hapa nchini itakuwa ikitambulika.
Utaratibu wa anwani hizi utaweza kumtambulisha mtu anaishi mkoa upi, wilaya ipi, kata ipi, kijiji au mtaa upi na nyumba namba ngapi. Mfumo huu wa anwani za makazi unakwenda sambamba na mchakato wa upatikanaji wa vitambulisho vya taifa.
Vitambulisho vya taifa vinalenga kumtambua kila Mtanzania na wageni kwamba wao ni kina nani, wanaishi wapi na wanafanya nini. Kwa pamoja miradi hii miwili inarahisisha utambuzi wa kila mtu anayeishi hapa nchini. Tumeshuhudia kwa wale waliopata leseni mpya za udereva kwa sasa wanatambulika ni kina nani, wako wapi na wanafanya nini.
Sambamba na leseni mpya za udereva, tutakumbuka kuwa miaka miwili iliyopita tulikuwa na kazi ya kusajili namba za simu. Kwa bahati mbaya wapo watu waliotoa majina bandia na kujisifu kuwa wao ni wababe wameweza kukwepa mfumo.
Usajili huu wa simu, vitambulisho vya taifa na anwani za makazi ni dhana za msingi katika maendeleo yetu. Sisi tunashauri kuwa Serikali sasa iwe wazi, iongeze na mradi wa upimaji viwanja hasa katika makazi mapya watu wasijenge holela. Upimaji viwanja nao ukikamilika nchi hii itakuwa imepiga hatua kubwa ajabu. Nchi zote zilizoendelea zimefanya haya.
Inaaminika kuwa Watanzania wapatao milioni 18 kati ya milioni 42 sasa wana uwezo wa kufanya kazi au wanafanya kazi. Ajabu, watu wanaolipa kodi idadi yao haifikii milioni moja. Hawa wengine wapatao milioni 17 wanafanya biashara zao kwa kuhifadhi fedha kwenye magunia au chini ya mito ya kulalia. Kwa kufanya hivyo, Serikali inapoteza kodi nyingi ajabu.
Kwa kuwa na mifumo hii yenye kututambua sisi ni kina nani na tunafanya nini, tuna uhakika kiwango cha kodi inayolipwa kitaongezeka zaidi ya mara 10. Kuna magunia ya fedha zinazobadilishana mikono bila kuandikiwa risiti. Wapo wafanyabiashara wengi ajabu wanaouza bidhaa bila kutoa risiti katika maeneo mbalimbali nchini.
Anwani za makazi zitaziwezesha hata benki kukopesha Watanzania kwa uhakika na kwa riba ndogo. Leo mtu anaweza akajitambulisha kama Deodatus katika benki hii, kesho akaenda benki nyingine akajitambulisha kama Hamisi na akaikimbia mikopo yote asilipe – kumbe jina lake halisi ni Mutalemwa.
Suala la usalama nalo litaimarika kwa kila mtu kutambulika anaishi wapi. Wageni wetu wakiwamo watalii wataacha kupotea njia. Teknolojia za kisasa kama satellite navigator zitatumika kumuongoza mtu kutoka popote alipo duniani hadi nyumbani kwa Mtanzania, anayemuhitaji bila kulazimika kuuliza au kuangalia mwembe mkubwa kama alama ya kufika nyumbani kwake.
Miradi hii ni muhimu. Tuwe tayari hata kuchangia gharama kwa kuiwezesha kwani inaanzishwa kwa faida yetu na kwa usalama wetu kama Watanzania. Hongera TCRA, hongera NIDA kwa hatua kubwa mliyoifikia.