Ni wazi sasa Waziri Mkuu wa zamani wa Ureno, Antonio Guterres, ndiye Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa. Anatarajiwa kuanza kazi rasmi  Januari 2017 Katibu Mkuu wa sasa, Ban Ki-moon atakapomaliza muda wake.

Kwa sasa, kiongozi huyo anasubiri kuthibitishwa rasmi na nchi wanachama wa Umoja huo, baada ya kupata uungwaji mkono wa asilimia 100 kutoka katika nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Guterres ameongoza Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Wakimbizi (UNHCR) kwa mwongo mmoja, alipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Usalama, ambapo nchi 13 kati ya 15 za Baraza hilo ziliunga mkono uteuzi wake katika kura ya siri.

Wakati wa mahojiano, wajumbe wengi wameonesha kuridhishwa na utendaji wake sambamba na kuungwa mkono na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kama vile Amnesty International na Human Rights Watch.

Guterres pia anaungwa mkono na nchi tano wanachama wa kudumu na wenye kura ya turufu kwenye Baraza la Usalama zilizompigia kura ya ndiyo katika uteuzi wake.

Aliyetangaza mwafaka wa nchi wanachama za Baraza la Usalama, alikuwa ni Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, ambaye aliambatana na wajumbe wengine 15 wa Baraza hilo, na kumtangaza Guterres kama mshindi.

“Tunamtakia ndugu Guterres kazi njema wakati atakapotekeleza majukumu yake mapya kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka mitano ijayo,” aliongeza Balozi Churkin.

Guterres alikuwa Waziri Mkuu wa Ureno kati ya mwaka 1995 na 2002, amewahi pia kushika nyadhifa kadhaa za juu, lakini kukubaliwa kwake bila kupingwa na nchi wanachama kumeonekana kuwashangaza wengi.

Atakuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Mataifa ambaye amekuwa kiongozi wa juu kwenye serikali ya nchi yake, nafasi ambayo mara nyingi ilikuwa inakaliwa na mawaziri wa mambo ya nje.

Katika kinyang’anyiro hicho, kulikuwa na wagombea 10 kuwania nafasi hiyo ya juu katika Umoja wa Mataifa, akiwamo Waziri wa Mipango wa Umoja wa Ulaya, Kristalina Georgieva, kutoka Bulgaria aliyeingia kwenye mbio za kutaka kupata nafasi hiyo bila mafanikio.

Makamu wa Rais wa zamani wa Benki ya Dunia, Georgieva, alishindwa kupata uungwaji mkono kutoka kwa nchi mbili wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, huku kukiwa na taarifa za ndani kuwa Urusi ilimpinga.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO, Irina Bokova, ambaye alitengwa na serikali ya Bulgaria, akitakiwa kumpisha Georgieva, alipata kura mbili hasi kutoka kwa nchi tano zenye kura za turufu ndani ya Umoja huo katika mkutano huo.

Maisha yake binafsi

Antonia Guterres, alizaliwa mwaka 1949 na kusomea somo la fizikia katika Chuo cha Superior nchini Ureno kabla ya kuwa profesa na kuanza kazi ya uhadhiri mwaka 1971.

Anasema kuwa imani ya Kikatoliki, hakujifunza vyuo vikuu kwa muda mrefu. Baada ya miaka miwili, alijitosa kwenye siasa, na kujiunga na Chama cha Socialist, mwaka 1974.

Mwaka 1992 alichaguliwa kama Katibu Mkuu wa chama hicho cha Socialist  na miaka mitatu baadaye akachaguliwa kama waziri mkuu wa Ureno. Alishika nafasi hiyo kwa miaka kumi (1995-2005).

Guterres anazungumza kwa ufasaha lugha nne – Kiingereza, Kireno, Kifaransa na Kispaniola. Alijitosa kwenye uwanja wa diplomasia na kuwa Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), wadhifa ambao aliushikilia kwa miaka kumi hadi mwaka 2015.

Uongozi wake katika shirika hilo umetajwa kuwa uongozi bora uliowezesha shirika hilo kufanya mambo makubwa na mengi hasa kipindi ambacho wakimbizi kutoka nchi za Syria, Yemen, Afghanistan, Somalia na Sudan Kusini walipozidi kuongezeka.

 

Wagombea wenza Marekani waendeleza malumbano

 

Wakati wananchi wa Marekani wanatarajiwa kupiga kura kumchagua Rais wa 45 wa taifa lao ifikapo Novemba 8, hali ya malumbano imeendelea kutawala katika kampeni hizo, na mara hii ilikuwa ni kati ya wagombea wenza.  

Mgombea urais mwenza wa chama cha Republican nchini Marekani, Mike Pence, na mwenzake wa Democratic, Tim Kaine, wamelumbana kuhusu taarifa za kodi za Donald Trump kwenye mdahalo wa runinga.

Pence, ambaye ni Gavana wa Indiana, anasema mgombea urais wa chama cha Republican, Trump, alitumia ‘werevu’ katika kutumia sheria za kodi kukwepa kulipa kodi na kuongeza kuwa Wamarekani watafanya makosa makubwa wakiamini propaganda hizo za kisiasa. 

Kwa upande wake Kaine, Seneta wa Virginia, ambaye ni mgombea mwenza wa Clinton, alipinga wazo hilo la ‘werevu’ akishangaa iwapo ilikuwa busara kukwepa kulipa kodi kwa mfanyabiashara huyo tajiri, Donald Trump.

Kaine (57), alianzisha mjadala huo wenye hisia kali katika Chuo Kikuu cha Longwood, Virginia kwa kushangaa ni vipi Pence anamtetea Donald Trump wakati ni mtu aliyehusika kuwapa mateso Wamarekani kwa kukwepa kodi ambayo ingesaidia maendeleo yao.

Lakini mpinzani wake wa Republican alimjibu kwa kumkosoa Hillary Clinton kwa kutumia barua pepe yake ya kibinafsi kwa shughuli rasmi pamoja na sera yake ya mambo ya nje ambayo alisema imesababisha vurugu katika baadhi ya maeneo duniani.

Pence anasema, “Marekani si salama sasa” kuliko ilivyokuwa Rais Obama alipochaguliwa, na akasema Clinton anafaa kulaumiwa kutokana na kuchipuka kwa kundi la Islamic State (IS) ambalo limekuwa janga kwa taifa la Marekani.

Taarifa za hivi karibuni zinamtaja Donald Trump kutolipa kodi kwa kipindi cha miaka 18. Taarifa hii iliyotolewa na gazeti la New York Times imesababisha utata nchini Marekani. Kulingana na waraka uliopeperushwa na gazeti hilo, Donald Trump amesema kuwa alipoteza dola milioni 916 kwa mwaka 1995.

Ripoti ya taarifa ya mapato ya mwaka 1995, iliyotumwa na mtu ambaye hakutajwa jina kwa gazeti la New York Times inaonesha kwamba baada ya vitegauchumi vyake kuanguka kiuchumi katika mji wa Atlantic City na kupoteza dola bilioni moja na kushindwa kulipa kodi kwa zaidi ya miaka 18.

Wakati hayo yakitokea, taarifa kutoka timu ya kampeni ya Clinton inasema kwamba hali hiyo haiwezi kufumbiwa macho na kuongeza kuwa lazima mamlaka husika zichukue hatua za kisheria dhidi ya mhusika na washirika wake wote.

Donald Trump ameahidi kulifungulia mashitaka gaezeti la New York Times kwa kumdhalilisha na kumchafulia jina hasa katika kipindi hiki ambacho Marekani inakabiliwa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Novemba 8.

 

Taarifa hii imeandaliwa na Michael Sarungi kwa misaada ya mitandao ya kimataifa.