Miaka 13 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, afariki dunia, waliokuwa wasaidizi wake wa karibu bado wana kumbukumbu ya mambo mazito kuhusiana na ugonjwa uliosababisha kifo chake. Si hilo tu, Serikali nayo imewasusa na wengi wanaishi maisha ya tabu haijapata kutokea. Yafuatayo ni mahojiano kati ya JAMHURI na Anna Mwansasu, aliyekuwa Katibu Muhutasi wa Mwalimu Nyerere…
Jamhuri: Uliajiriwa lini serikalini?
Anna: Mimi nilianza kazi serikalini rasmi mwaka 1969. Wakati huo nilikuwa nimeajiriwa ofisi ya Waziri Mkuu. Ilipofika mwaka 1973, nilihamishiwa Ofisi ya Rais Ikulu. Pale nilimkuta [Joseph] Butiku akiwa private secretary [Katibu Myeka] wa Mwalimu, akiwapo [Laurence] Batao akiwa Msaidizi wa Mwalimu, alikuwapo Waziri wa Nchi [Said] Natepe, [Benjamin] Mkapa akiwa Press Secretary, [Mizengo] Pinda akiwa Katibu Msaidizi, Joan Wicken na Arnar Cassum wote wakiwa Wasaidizi wa Mwalimu.
Jamhuri: Ulijisikiaje kuanza kufanya kazi na Mwalimu?
Anna: Kwanza niseme tangu mwaka 1973 hadi Mwalimu anastaafu [1985] sikupata kumfahamu vyema Mwalimu. Nilimfahamu vyema baada ya kustaafu. Siku alipostaafu, tulichaguliwa wafanyakazi kadhaa kwenda naye Butiama. Tulipofika, Mwalimu akasema hapa hakuna ofisi, twende shamba tukachimbe visiki. Tulikuwa group kubwa. Ninaposema kundi tulikuwa wengi kweli. Akina Tendewa, Mshama, Shayo, Batao na si sisi tu wafanyakazi, lakini ilikuwa ni group kubwa, watoto wake, watoto wa ndugu zake, akina Manyerere Jackton hawa, basi hapo ndipo nilipomfahamu Mwalimu.
Pale ndipo nilipojua Mwalimu ni mtu “simple” sana. Hakuwa na makuu na ni mtu aliye na upendo na hana makuu. Ilikuwa wanapakua chakula, tunakula wote, na Mwalimu alikuwa anapenda tule wote, lakini sisi tulikuwa tunaheshimu “privacy” yake. Alikuwa anataka tuwe wote muda wote lakini sisi tulikuwa na nyumba zetu na tulitaka awe huru. Alikuwa anajali watu, sana kupita kiasi. Pale nyumbani kwake, pale kwake, hayo mambo ya chakula ninayoyazungumza ilikuwa mtu yeyote anayekwenda kumtembelea Mwalimu ikiwa ni wakati wa chakula – awe ndugu yake, awe nani – atakwenda kula chakula na Mwalimu. Huo ndiyo uliokuwa utaratibu wake. Mama Maria tulikuwa karibu naye sana, na sote pale tulionekana kama wanafamilia.
Jamhuri: Mwalimu alikuwa anatumia kinywaji gani?
Anna: Mwalimu alikuwa anakunywa bia moja tu ya baridi jioni… siwezi kufahamu ni ipi ila wale waliokuwa wahudumu wake wanaweza kujua zaidi.
Jamhuri: Ni sifa ipi ulistahili kuwa nayo kufanya kazi na Mwalimu?
Anna: Sifa namba moja ilikuwa ni uadilifu. Mwalimu alikuwa mchapakazi mkubwa. Huwezi kuwa ofisini kwa Mwalimu ukawa mzembe mzembe. Wakubwa watakuondoa. Uadilifu ilikuwa sifa kuu ya Mwalimu. Alikuwa hajali nani anafanya kazi ofisini kwake [ukabila] kwani katika ofisi ya Mwalimu walikuwapo watu kutoka Iringa, Bukoba, Musoma, Kilosa, kila mtu alikuwa ndugu yake. Hakurundika watu kutoka mkoani kwake tu, ilimradi uwe ni Mtanzania ulipata sifa ya kufanya kazi ofisini kwake.
Jamhuri: Ilikuwaje kama mtu alitaka kumuona Mwalimu ofisini kwake?
Anna: Ilikuwa ukifika ofisini kwa makatibu, unataka kuonana na mkubwa, hakukuwapo tatizo. Mtu anakuja anataka kumuona Mwalimu, unachukua jina lake, namba yake ya simu kama anayo, unaipeleka kunakohusika. Private Secretary anamsikiliza mtu, anamruhusu kwenda kwa Mwalimu kama inahitajika hivyo. Ilikuwa hakuna ubabaishaji wa njoo kesho, njoo kesho kutwa. Ilikuwa ikibidi mnapiga simu kwenye ofisi inayohusika mnamwambia anayehusika amsaidie huyo mtu aliyetaka kumuona Mwalimu.
Mwalimu alikuwa anawasaidia watu. Hata pale Butiama, kuna watu walikuwa wanafika na shida, wanamweleza Mwalimu, na Mwalimu akimsikiliza anamwita Batao anamwambia Batao mpe kiasi kadhaa kutoka kwenye posho yake ya ustaafu. Tena wakati mwingine, inafika mahala anakuja mtu anasema ana njaa na kwa kuwa Mwalimu alikuwa na vihenge, anamwita mtu anayehusika anasema jamani ehee, mchotee mahindi huyu akale. Hayo ndiyo yaliyokuwa maisha ya Mwalimu.
Jamhuri: Ukiacha haya maisha ya nyumbani, siku hizi tunashuhudia makosa mengi kwenye miswada, hati za serikali na nyaraka nyingine. Enzi zenu ilikuwaje, hamkukosea kila mlipochapa hotuba au nyaraka za Serikali?
Anna: Enzi za Mwalimu hakukuwapo kitu kinachoitwa kukosea. Utakoseaje? Mwalimu alikuwa havumilii makosa. Ukikosea mara moja, anaita vyombo vya habari anatangaza kukuondoa kazini. Wala hakukuwapo nafasi ya kukosea, sasa ukicheka na wanaokosea, wataendelea kukosea.
Watu walikuwa wanafanya kazi kiadilifu. Hilo suala la miswada kukosewa, sijui nini kuandikwa kivingine hayo hayakuwapo kutokana na uadilifu wa Mwalimu na wote waliokuwa ofisini. Kama kuna mtu alitenda kinyume na taratibu, Mwalimu hakusita saa hiyo hiyo… atatafuta ukweli, kwani alikuwa na njia zake za kutafuta ukweli.
Alikuwa anapata taarifa kutoka kwa wasaidizi wake, alikuwa na wazee mbalimbali aliokuwa anawaamini wanafika pale wanampelekea taarifa, kwa hiyo Mwalimu alikuwa akithibitisha kuwa fulani kafanya kosa, alikuwa hasiti saa hiyo hiyo anatangaza kwenye vyombo vya habari kwamba huyu kazi hana. Na watu walikuwa wanasema, sijui kama kulikuwa na ukweli, hao viongozi wanasema Mwalimu akikuita Ikulu anakupa cheo, akikuita Msasani anakufukuza kazi. Kwa hiyo alikuwa ana msimamo tu, kwamba alikuwa hataki mchezo, alikuwa anachukua hatua hapo hapo. Kwa hiyo suala la mikataba kukosewa na nini, mimi sijawahi kusikia.
Jamhuri: Wanaokosea unashauri wafanyeje?
Anna: Kukosewa kwa mikataba kunachangiwa na tamaa ya kutaka utajiri wa haraka haraka. Mwalimu amestaafu mwaka 1985, watumishi wote wa Mwalimu waliofanya kazi enzi za Mwalimu na wakastaafu kabla ya Mkapa kurekebisha skimu ya pensheni, ni maskini wa kutupwa kwa sababu tu ya uadilifu wao. Walifanya kazi kwa uadilifu na wanaishi maisha ya dhiki ajabu. Kwa bahati mbaya hata baada ya Mkapa kubadili skimu, wale wote waliotumikia enzi za Mwalimu hawakufikiriwa. Na kama walifikiriwa waliongezwa kidogo mno. Ukilinganisha na hizi sasa wanazopata watu wengine ni kidogo mno.
Jamhuri: Mama, wewe wakati unastaafu ulipata pensheni kiasi gani na sasa unalipwa kiasi gani?
Anna: Wakati nastaafu mwaka 1997 nilipata pensheni ya shillingi milioni nne. Kilichonifanya nistaafu ni ile Mwalimu kuniambia Anna ujuzi wako ulionao ni bora ustaafu uende South Commission Geneva – kidogo hiyo ndiyo ilinipa nafuu, na kidogo hiyo ndiyo ilinifanya nijenge Kivule [Kitunda- Dar es Salaam], ambako nimejenga kanyumba kana vyumba viwili na hakajaisha. Wala hakana umeme.
Kwa mwezi napata laki moja naaaa, laki moja naaaa, kwa maana ndani ya miezi mitatu napata 350,000. Lakini tunashukuru ukipata hiyo, unakwenda kulipa madeni na kununua dawa. Kwa maana mimi natumia “pace maker” (vidonge vya kusaidia moyo) kwa siku nameza vidonge vinane. Na vidonge unakuta kidonge kimoja kingine 450, kingine 250 na kingine 300, unapata misaada kutoka kwa ndugu mwishowe na wengine wanakuchoka. Mpaka leo naombaomba namna hii, lakini si mimi peke yangu, tuko wengi wa aina hii tuliotumikia kwa uadilifu wakati wa uongozi wa Mwalimu… mimi naishi hapo Kivule, nikichoka nakuja kula hapa kwa Mwanangu [Mchezaji wa Yanga wa Zamani – John Mwansasu].
Jamhuri: Huko Kivule, kiwanja chako kina hati?
Anna: Wapi bwana. Hata wakisema nilipie hiyo hela yenyewe ya kulipia hati ninayo basi? Mimi nikipata ile pensheni nalipa madeni na sibaki na kitu. Lakini ukichukulia hili kundi la viongozi waliokuwa wasaidizi wa Mwalimu ndiyo hao wapo madarakani. Wakiamua watatukumbuka.
Jamhuri: Wewe ulikuwa unamwogopa Mwalimu kiasi gani?
Anna: Mwalimu ile tu alivyokuwa, alikuwa akijitahidi kuwafanya watu wawe karibu naye, kuwafanya watu wamzoee, lakini unakuta kuna kitu kinakwambia…, usiende sana. Nakumbuka tulikuwa tumesafiri, tulikuwa New York [Marekani]. Mara nikiwa chumbani, baada ya kuwa nimekwishatayarisha hotuba yake nimeiweka kwenye folder (jalada), Miss [Joan] Wicken hakuwapo alikuwa anaumwa, nikiwa chumbani kwangu nimetulia nikasikia mtu anagonga mlango. Nikabaini sauti kuwa alikuwa Mwalimu. Nikanyanyuka nikaenda mlangoni akaingia chumbani akaniambia ‘Nimefanya marekebisho kidogo kwenye hotuba yangu kama kurasa tatu hivi, naomba unifanyie masahihisho kwa kuichapa upya.’ Ilikuwa zimesalia kama dakika tano kabla ya muda wa kuondoka, nilipata hofu kubwa.
Mwalimu akiwa amenisimamia, nilichapa ile hotuba kwa kasi kubwa na nilipomaliza nikaisoma upya kuona kama sijakosea, akiwa amesimama akauliza, ‘Umemaliza mama?” nikamwambia ndiyo. Akasema ‘Umeisoma upya’ nikamwambia ndiyo. Akaichukua akasema ‘Anna asante sana.” Hili sijawahi kulisahau. Kuchapa hotuba ya Mwalimu akiwa amekusimamia, haikuwa kazi rahisi. Na mara zote Mwalimu alikuwa anasema ‘naomba’ unifanyie kazi hii, hakuwahi kusema ‘nataka’.
Jamhuri: Umesema muda mwingi Mwalimu alikuwa anafanyia kazi Msasani. Ikulu alikuwa anakuja wakati gani?
Anna: Ni kweli mara nyingi Msasani ndiko alikokuwa akifanyia kazi zake. Ikulu alikuwa anakuja kama kuna sherehe za kitaifa, kuna ugeni unaomtembelea kama mabalozi au nini, vinginevyo, Batao alikuwa anabeba mafaili asubuhi na kuyapeleka Msasani, kisha jioni anayarejesha Ikulu baada ya Mwalimu kuyapitia na kutoa maelekezo.
Jamhuri: Sasa mafaili ya kunyonga wahalifu waliohukumiwa kifo nayo alikuwa anayapitia Msasani?
Anna: Kuna baadhi ya mafaili sisi wadogo tulikuwa hatuyaoni. Mengine yalikuwa yanakwenda moja kwa moja kwa Private Secretary wake. Lakini Mwalimu alikuwa hafurahii kuua na nafahamu hakufanya hivyo isipokuwa yule Mwamwindi tu [aliyemuua Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dk. Kleruu].
Mafaili kama ya Usalama wa Taifa, Mambo ya Ndani, yalikuwa yanapelekwa moja kwa moja kwa Mwalimu au Private Secretary wake. Ingawa kwa kila hali usingeweza kutoa siri. Kulikuwapo na vetting ya hali ya juu kwamba mpaka unafikia ofisi ya Rais – unatosha. Lakini si kila siri ilikuwa inatufikia sisi ma-secretary, maana kuna baadhi ya mambo ni mazito unaweza kuyaona, ukajikuta unafika nyumbani unakereketwa kifuani ukamwambia mumeo na mambo yakaharibika.
Jamhuri: Kuna watu wanasema kifo cha Mwalimu kilikuwa ghafla mno. Je, hili lina ukweli kiasi gani?
Anna: Mwalimu alipoanza kuugua mimi nilikuwa Geneva. Ilikuwa tunajua kwamba anaumwa, lakini ile mara ya mwisho ya kuja Uingereza kule na kutokurudi hiyo ndiyo naikumbuka zaidi. Nakumbuka pale ofisini tulipata taarifa kuwa Mwalimu amekuja London kuja kutibiwa. Tukajua ni ile kawaida kwa vile alikuwa anapangiwa daktari anarudi, kwa hiyo tukajua kwamba ni mpangilio ule ule.
Basi, baada ya siku tatu nne hivi, tukapata taarifa kuwa Mwalimu hali yake siyo nzuri sana. Wakati huo Miss Wicken alikuwa ametoka huko kwake alikokuwa, akaja pale London akanipigia simu akaniambia, Anna, Mwalimu hali yake si nzuri. Basi na mimi ikanigusa, kwa hiyo nikatafuta nauli nikapanda ndege nikaja London. Nikaja London pale tukafika siku hiyo, nikaenda nyumbani kwa Mwalimu, alikuwa anakaa kwenye apartment (nyumba ya kupanga) alikuwa hataki kukaa hotelini kuepusha matumizi makubwa ya fedha.
Basi nikafikia pale, nikamkuta Ghati [mjukuu wa Mwalimu] pale, akasema njoo ulale chumbani kwangu. Baadaye tukaenda kumuona Mwalimu. Tukaingia pale chumbani kwa Mwalimu, nikamwamkia Mwalimu ‘Shikamoo’, ‘Marahaba’ tukaongea, nikamuuliza unaendeleaje akasema, ‘Mimi bwana sitaki kukaa sana hapa. Nina mkutano na Warundi wangu nataka nirejee Arusha kwenye mkutano. Kisha akasema ‘Bwana wameniambia, wanataka kunibadilishia damu, waniwekee damu nyingine. Waniongezee damu, waniwekee damu ya mtu mwingine. Sasa huku mswahili atatoka wapi, nitawekewa damu ya Mzungu. Nikishawekewa damu ya Mzungu nitakuwa Kambarage tena?’ Kwa hiyo alikuwa anatania hivyo.
Basi alikuwa katika hali ile ya kawaida tu. He was fine (alikuwa anaendelea vizuri). Tukaondoka tukawa tumelala. Kwa hiyo baadaye Ghati akawa amekwenda kule kwa babu yake, alivyorudi [usiku] akasema hali ya babu imebadilika. Akaniambia hivi; babu kazidiwa. Basi tukaenda kule. Kuangalia si yule Mwalimu niliyeongea naye kabla, hali imebadilika. Kuongea anaongea kwa tabu. Akasema nawasubiri waje wanipeleke hospitali. Ilibidi tusubiri, daktari wake aje, wafanye utaratibu aweze kwenda hospitali. Mwalimu ambaye alikuwa ananyanyuka anakwenda toilet (chooni), alichukuliwa na wheelchair. Akawa hawezi kabisa kutembea. Akaenda akalazwa hospitali, ikawa tunakwenda tunamwangalia tu kisha tunarudi, kesho yake tunakwenda, sikumbuki ilikuwa siku ngapi, lakini nakumbuka tulikaa kama siku tatu hivi alikuwa haongei.
Jumapili yake, baada ya hizo siku tatu, akaja Mkapa, akakuta Mwalimu yuko unconscious, wamemwekea mashine, halafu alikuwa hayapendi madude yale [mashine ya kupumulia], akawa ananyanyua mkono kuyaondoa. Kutokana na hali hiyo ikabidi mmoja akae huku, na mwingine akae kule [upandeni mwa kitanda] ili kuzuia asipeleke mkono puani.
Kwa hiyo kipindi hicho wakati Mama Mkapa anakuja, akainua mkono, nikamwambia Mama Mkapa, Mwalimu anataka kukusalimia, akampa mkono. Kumbe alikuwa anatambua watu. Sasa ilipofika Jumapili, wakaja Rose na Anna, walipofika kumwangalia Mwalimu, Mwalimu anageuka akawa anawambia Rose na Anna, “Nyie Waswahili mmekuja lini?” Kama miujiza vile, akaweza kuzungumza, akaongea nao pale, kesho yake haongei. Akahamishiwa huko ICU [Intensive Care Unit], ambako hakuna mtu aliyekuwa anaruhusiwa kuingia zaidi ya Mama Maria na familia yake. Kwa hiyo mimi siku zangu nilizokuwa nimeomba zikawa zimeisha nikarudi kazini [Geneva, Uswisi]. Lakini alivyokuwa tu alikuwa katika hali inayoeleweka kwamba anaweza akapona.
Jamhuri: Hadi anafariki walikuwa wameishambadilishia damu?
Anna: Sina uhakika.
Jamhuri: Ulipopata taarifa za kifo cha Mwalimu ulikuwa wapi na ulifanyaje?
Anna: Daaa! Naikumbuka siku hiyo. Nilikuwa ofisini, na nilipiga kelele hadi Wazungu wote wakaja kujua kulikoni. Unajua Wazungu kwa taratibu zao hawana utamaduni wa kupiga yowe ofisini, lakini mimi nilipiga kelele ajabu. Walikuja pale, wakanipa ruhusa niende nyumbani nikapumzike.
Nilipofika nyumbani nikarudi ofisini nikawaambia kwa tamaduni zetu lazima niende nyumbani Tanzania kumzika Mwalimu. Nikakusanya fedha kidogo nilizokuwa nazo nikakata tiketi na kufanikiwa kuja kumzika Mwalimu.
Jamhuri: Kwa muda uliofanya kazi na Mwalimu, ni vitu gani vitatu vilivyobaki kwenye kumbukumbu yako milele?
Anna: La kwanza ni elimu. Kama si sera ya Mwalimu ya kutoa elimu bure, basi nisingeweza kufikia hapo nilipofikia. La pili ni exposure (fursa ya kutembea). Wapo ma-secretary wengi hapa nchini, lakini Mwalimu alinipa fursa ya kutumikia hadi nje ya Afrika. Jambo la tatu ni Mwalimu kunipa fursa ya kuishi maisha ya kuwa sehemu ya familia yake.