Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Itilima
RUZUKU inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imemwezesha, Anna Ang’obo Ngasha (45), kujifunza ushonaji nguo, kununua cherehani, kazi ambayo inamwezesha kujiingizia kipato cha kuendesha maisha yake.
“Nimekuwa fundi mzuri hapa kwenye mtaa wetu wa Line B, ukiuliza mafundi maarufu watano hauwezi kunikosa na haya ni matunda ya fedha za TASAF” anasema.
Anna mkazi wa Kijiji cha Line B, Kata ya Sangata katika Halmashauri ya Wilaya Itilima, mkoani Simiyu, ametoa ushuhuda huo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ambayo amepata tangu alipojiunga na Mpango wa TASAF.
Akieleza magumu aliyopitia kabla ya kushikwa mkono na TASAF na hatua aliyopo sasa, Anna anasema alikuwa na maisha magumu, chakula nyumbani kwake hakikuwepo.
“Watoto wangu walikuwa wanaenda shuleni wamevaa nguo za nyumbani bila viatu.
Mimi mwenyewe hali ngumu, nilikuwa sina mavazi nilikuwa nasaidiwa na watu, wanasema mama chukua hii nguo ukajifunge. Nimefanya sana vibarua niliishia kupata chakula kidogo, nilikuwa naenda kuomba chakula,” anasema, Anna na kuongeza;
“Sasa hivi najitegemea kabisa, chakula ninacho cha kutosha nyumbani, nanunua nguo zangu za watoto wangu bila wasiwasi. Haya ni matunda ya kazi ya Mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) ndiye amefanya yote haya.” anasema.
Akieleza jinsi alivyofikia hatua aliyopo sasa, Bi. Anna anasema mwaka 2015 ndipo alipoandikishwa kwenye mpango wa TASAF na alipoanza kupokea ruzuku, kiasi kidogo cha fedha alizopewa alijiwekea akiba, na kingine alikitumia kwa ajili ya mahitaji ya wanafunzi.
Pia anasema alianzisha mradi wa kuuza dagaa na mahindi ya kuchoma, na faida aliyopata pamoja na kusomesha watoto na yeye alimtafuta mtu wa kumfundisha ufundi cherehani.
Kwa mujibu wa Anna, kadri alivyokuwa akipewa fedha za TASAF, aliendelea kuzitunza na zingine kuziweka kwenye biashara zake na alipofikisha sh. 150,000 alinunua cherehani.
Kwa mujibu wa Bi, Anna, alipofahamu kukanyaga cherahani, alianza kumpelekea nguo za kuziba viraka, wakati huo akiendelea kujifunza.
“Nilitengeneza kibubu, fedha nilizokuwa napata kwa kushona viraka nalizitunza humu niliendelea kuongeza juhudi, wateja walianza kunielewa,” anasema na kwamba aliendelea kuweka fedha kwenye kibubu hata pale alipopata ruzuku ya TASAF
Anasema kwa sasa ana mtaji wa kununua vitambaa vya kushona nguo za wateja zaidi ya sh. 300,000, lakini wakati anaanza kununua vitambaa alikuwa na mtaji wa sh. 50,000.
Anasema ufundi wa kushona nguo umemwezesha kupata kipato cha uhakika, kwani hata baada ya watoto wake wawili kuhitimu darasa la saba na kufaulu aliwapeleka sekondari bila wasiwasi wowote.
Anamshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuhakikisha TASAF inawezesha watu wenye maisha duni, kwani amerejesha furaha kwenye familia yake ambayo haikuwepo kwa sababu ya umaskini.
Kwa mujibu wa Anna, mbali kujifunza ufundi cherehani na kusomesha watoto, nyumbani kwake ana vitu vingi, ambavyo amefanya kupitia TASAF, ambavyo huko nyuma hakuwa navyo.
“Nimenunua mbuzi zikizaa nauza nanunua bati, nimefyatua tofali za block ninategemea kuanza ujenzi,” haya yote yananifanya niwe na furaha. Aidha, anasema anakodi mashamba analima mahindi.
“Namshukuru Rais Samia kwa mazuri ambayo ametufanyia wanawake wanufaika wa TASAF,” anasema.