NA MTANDAO

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amesema anakamilisha utaratibu wa kuangalia namna ya kuunda serikali ya mseto kwa kushirikiana na viongozi wa vyama vya Social Democratic na SPD.

Amesema wanatarajia kwenda mbele katika jitihada zao za kuunda serikali na ndiyo maana ana matumaini juu ya majadiliano yanayoendelea, huku akisema  anaamini hilo linaweza kufikiwa kwa wakati.

Amesema Wajerumani wanahitaji uwepo wa serikali imara itakayojali ustawi wa taifa la Ujerumani, na kuongeza kuwa wananchi wanapaswa kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki.

“Siku 14 zilizopita, tulikamilisha mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuunda serikali, ni vizuri kwamba leo tunaweza kuanza mazungumzo hayo, lazima tujadiliane wazi ni mambo gani mema yanafaa kwa Ujerumani ya siku za usoni,” amesema Merkel.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha Christian Social Union (CSU), Horst Seehofer, amesema chama chake kinaingia katika majadiliano kwa moyo mkunjufu lakini akasema huenda majadiliano hayo yasifanikiwe endapo matakwa yao hayatakubaliwa.

Vyama hivyo vitatu vya kihafidhina vya Christian Democratic Union (CDU), CSU na SPD katika taarifa yao ya pamoja vilisema vina nia ya kumaliza majadiliano hayo ndani ya wiki mbili.

Hata hivyo, Kansela huyo wa Ujerumani wa muda mrefu, alijaribu kuunda serikali na Chama Cha Walinzi wa Mazingira “die Grüne” na waliberali wanaowapendelea Chama cha  Free Democrats, jaribio ambalo lilishindwa mwaka uliopita.

Katika siku za hivi karibuni, pamekuwepo na hali ya sintofahamu ya lini viongozi hao watafikia mwafaka wa kuweza kuunda serikali ili kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea kama kawaida kama inavyotakiwa.

 Mwaka jana, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, aliibuka kidedea kwa ushindi katika uchaguzi mkuu nchini humo kuwa kiongozi wa nchi hiyo kwa  kipindi cha nne, lakini haukuwa ushindi wa kishindo.

Merkel, kupitia chama chake cha CDU, ameshinda kwa asilimia 32.9 huku wataalamu wengi wa masuala ya kisiasa wakidai kuwa chama chake kimekosa ushawishi ikilinganishwa na chama cha mlengo wa kulia cha AFD.