Kama angekuwa hai, tarehe 13, Aprili 2019 Mwalimu Nyerere angetimiza umri wa miaka 97.

Muda mfupi kabla ya hapo, nilifikiwa na ugeni wa mtu aliyejitambulisha kwanza kama ni jamaa yangu kwenye ukoo wetu lakini ambaye sijapata kuonana naye. Hilo si ajabu kwa sababu ya ukubwa wa ukoo wenyewe.

Aliniletea ujumbe kutoka kwa mtu mwingine kunijulisha kuwa Mwalimu Nyerere yuko hai, hajafariki dunia ila kuna sehemu amezuiliwa na nahitajika nipewe ufafanuzi wa wapi alipo na jinsi ya kuweza kumuibua huko aliko.

Nikafahamishwa hata Steven Kanumba, yule muigizaji mashuhuri ambaye tuliambiwa amefariki dunia mwaka 2012 naye yupo, pamoja na watu wengine kadhaa mashuhuri ambao sikumbuki majina yao.

Ningeambiwa maneno kama haya miaka 10 iliyopita ningecheka sana, tena kwa kushindwa kujizuia na mbele ya huyo huyo aliyetumwa kwangu. Lakini umri ni darasa linalozima mengi.

Umri unanikumbusha kuwa imani ni jambo la ajabu kidogo. Nazungumzia imani yoyote ambayo umeisikia: ya dini, ya kishirikina, ya uwezo wa binadamu pekee bila kutegemea msaada wa dini wala ushirikina, ya uwezo wa sayansi. Kwa kifupi, imani yoyote ambayo inakuamsha kitandani kila siku na kukupa uhakika mkubwa kuwa leo ni siku nzuri ya mafanikio kwenye safari ya maisha yako.

Kwamba hata kama kuna tatizo, imani yako inakutuliza kuwa tatizo hilo halitadumu na maisha yako yataendelea kupata mafanikio.

Kuna ushindani katika imani mbalimbali kiasi kwamba baadhi ya waumini wanajipa hadhi kubwa zaidi na imani zao dhidi ya imani nyingine. Mfano, kukataa kuwa nguvu ile ile inayomsukuma muumini wa ushirikina kuamini masuala ya ajabu inaweza kuwa na matokeo yale yale kwa mtu ambaye yeye anaapa kwa jina la sayansi.

Nitatoa mfano mmoja ambao unadhihirisha uwezo mkubwa wa imani yoyote. Ni mfano ninaopenda kuurudia kwa sababu ya nguvu ya hoja yenyewe. Matabibu wa taaluma inayojulikana kama tiba ya Magharibi hutumia dawa bandia inayojulikana kama placebo kutibu watu ambao wanaamini wanakabiliwa na ugonjwa lakini ambao sayansi imethibitishwa kuwa hawana maradhi yoyote.

Anayeamini kuwa ni mgonjwa anapewa kidonge ambacho kinaweza kuwa unga wa muhogo, lakini kwa sababu anaamini anaumwa na kuamini anapewa tiba, ule unga wa muhogo utamponya ugonjwa ambao ni wa kufikirika tu. Hii ni sayansi lakini inatumia imani tu kumaliza tatizo la kisaikolojia la mgonjwa feki.

Ndiyo sababu nasema sikucheka kusikia zile taarifa za kurudishwa Mwalimu Nyerere kwa sababu sina uhakika ni zipi faida kwa binadamu anayefikia uamuzi kuwa yupo binadamu mwenzake mwenye uwezo wa kuwarudisha watu ambao tuna hakika walifariki dunia na tuliwazika miaka mingi iliyopita.

Lakini kusema sikucheka si kusema kuwa nayaamini hayo. Sina shaka pia zipo hasara za imani kama hizi kwa sababu maisha yanapaswa kuhusishwa zaidi na yale yanayojiri kwa sisi ambao tupo badala ya kuturudisha kwenye imani kuwa wale ambao hawapo wanaweza kurudi.

Kwa hali ya kawaida, binadamu hawezi kuwa na amani kuanza kuishi tena na mwanafamilia ambaye alishiriki kumzika. Lakini binadamu wote hatuko sawa, kwa maana ya kukubali yaliyopita yabaki huko huko, na ndiyo maana hatuachi kusikia simulizi za watu kurudishiwa uhai au za watu kusema wana uwezo wa kufanya hivyo.

Natafakari mazingira ambapo ni jambo la kawaida tu mtu kurudishiwa uhai, mazingira ambayo yangenifanya nimkubalie jamaa yangu tukamuibue Mwalimu Nyerere huko aliko.

Nahisi kama swali la kwanza ambalo angeniuliza mimi baada ya kukubali wazo la kumrudisha ni: “Nani kakwambia nilitaka kurudi huku?”

Uongozi hauachi ombwe hata kidogo kwa hiyo nafasi aliyokuwa nayo Mwalimu imeshajazwa siku nyingi zilizopita. Tunaweza kuandaa makongamano mengi kujadili imejazwa na nani na kwa njia ipi au iwapo imejazwa kweli, lakini ukweli ni kuwa nafasi ile aliyoiacha haipo tena.

Kwa hali hii humtakii mema kuombea arudi. Marcus Aurelius, mtawala wa Warumi kati ya mwaka 161 na mwaka 180, aliugua akiwa vitani wakati wa utawala wake na habari zikaenea kuwa amekufa. Mmoja wa majemedari wake, Avidius Cassius alijitangaza kuwa mtawala wa Roma na kuchukua nafasi ya Aurelius.

Taarifa kuwa Aurelius alikuwa bado hai zilizua vita kali kati yake na majeshi ya Cassius na hatimaye Cassius aliuawa, ingawa haikuwa kwenye uwanja wa mapambano bali kwa kuchomwa kisu na mtu ambaye yawezekana alikuwa mfuasi wa Aurelius.

Ni historia inayodhihirisha suala moja muhimu. Nafasi zinazoachwa wazi na kuzoeleka na wale waliyozishika haziachwi kirahisi. Au zinaweza kuachwa tu kwa kutumia nguvu ya ziada. Hapa sizungumzii uongozi rasmi alioshikilia Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake. Nazungumzia nafasi aliyokuwa nayo kama mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya jamii.

Sina shaka ipo sababu ya msingi kabisa kwamba baadhi ya dini zetu zinatufundisha kuwa yapo maisha ya duniani ambayo huisha na kuna uwepo wa roho ahera baada ya hapo. Ni hatua ambazo hazipaswi kuingiliana, na hatua moja hufuata nyingine. Na ndiyo maana watu wakiondoka kwa mtindo huu hawarudi.

Ni imani zinazotusaidia kusonga mbele na maisha. Ni imani zinazotukumbusha wajibu wetu wa kukabiliana na maisha yetu ya sasa.

Maoni: [email protected]