Mwanamke mmoja amefariki akipiga picha aina ya Selfie na rafikiye katika barabara ya treni nchini Thailand.

Rafikiye alisema kuwa walikuwa wamekunywa pombe na kuamua kujipiga picha hiyo na treni lakini hawakuona treni nyengine iliokuwa ikija kutoka barabara nyengine ya treni, kwa mujibu wa polisi.

Miguu yake ilikatika na kufariki hospitalini ambako alikuwa amepelekwa kwa matibabu zaidi.

Rafikiye wa kiume alipata majeraha mabaya.

Idadi ya watu wanaofariki wakipiga selfie katika maeneo hatari inaongezeka.

Kisa hicho kilitokea siku ya Alhamisi asubuhi katika kituo cha treni cha Samsen mjini Bangkok, kulingana na maafisa wa polisi wa Wissanusak Seub akiongezea kwamba maafisa walikuwa wakichunguza kilichotokea.

Kuchukua video huku umesimama mbele ya treni imeonekana kuwa swala hatari, hususan nchini India.

Mnamo mwezi Januari , mtu mmoja aliyekuwa akijichukua kanda ya video akisubiri treni iliokuwa ikikaribia aligongwa na treni hiyo mjini Hyderabad nchini India.

Mnamo mwezi Oktoba 2017, vijana watatu waligongwa na treni walipokuwa wakijaribu kuchukua picha ya selfie katika jimbo la Karnataka, huku vijana wengine wawili wakifariki wakati walipokuwa akipiga picha katika barabara ya reli mjini Delhi.