Lugha yetu ya Kiswahili haina uchache wa maneno katika matumizi ya kila siku kiasi cha kumfanya mtumiaji wa lugha hii kupata shida na kuchanganya maneno mawili au zaidi kukusudia kuelezea jambo moja; na kuleta mgongano wa mawazo kwa msikilizaji au msemaji wa habari fulani.
Si mara moja wala mbili, nimepata kusoma au kusikia habari fulani na kukuta mtoa habari akitumia maneno yenye maana tofauti lakini anakusudia kuelezea jambo moja. Matokeo ni msikilizaji au msomaji wa habari kujichanganya na kujiuliza mzungumzaji anakusudia jambo gani?
Mathalani, wiki iliyopita, Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Casmir Mabina, amenukuliwa na gazeti mojawapo litolewalo kila siku akiwa ofisini kwake, Dar es Salaam akisema, “Tunamshauri Rais Magufuli aache kutawala nchi kwa woga na ubabe…afuate misingi ya Katiba na sheria, na kuwaongoza Watanzania badala ya kuwatawala” mwisho wa kunukuu.
Kauli hiyo ni nzito kwa wanasiasa na hata kwa wananchi katika medani za kisiasa, utawala na uongozi. Naamini wapo watu wanaomudu kujibu na kuweka wazi mapigo hayo. Sikusudii kwenda huko. Nakusudia kuzungumza maana na matumizi ya maneno mawili ‘woga na ubabe’ ambayo yamebeba ujumbe mzima.
Neno woga linakuja katika hali ya kuwa na hofu ya kufikwa na jambo la kutisha au la taabu. Hali ya kutoweza kustahamili vitisho. Hali ya kuwa na kitete, hofu. Ukweli, mtu anapokuwa na woga hushindwa kufanya jambo. Anaogopa na hana ushujaa wa kufanya jambo.
Mbabe mtu mkubwa mwenye nguvu, yaani ‘mtemi’. Mtu mwenye nguvu na hodari kwa kupiga wenzake (mbabe). Ukiangalia sifa ya mtu mwoga na sifa ya mtu mbabe si moja ni tofauti. Kinachonishangaza mimi inakuwaje mtu anakuwa mwoga na muda huo huo anakuwa mbabe!
Nadhani mtu kama huyo ana uamuzi wa aina mbili. Ima aendelee kuwa mwoga katika kauli na matendo yake daima au aamue kutoka katika hali ya uwoga na kuingia katika hali ya ubabe, baada ya kujikomboa kifikira na kujenga moyo wa kujiamini na kuwa jasiri katika kauli na vitendo vyake.
Kama hivyo ndivyo, je, maelezo hayo yanamweka Rais Magufuli katika sifa ipi kwa wakati huu ya ubabe au ya woga; kwa sababu zipi? Au zote hazimuhusu? Natambua yapo makundi yanayomtambua Rais Magufuli ni mchapakazi na mtetezi wa wanyonge. Ni moto mkali kwa makundi yanayopenda kuvunja Katiba ya nchi kwa makusudi kwa kisingizio cha demokrasia na huku wakilia na kulalama kwa wananchi ili wawaonee huruma.
Yapo makundi yanayomtafsiri Rais Magufuli ni mwovu, hashauriki na wala hasikilizi vilio vya wanasiasa wenzake. Ni ngangari katika utumbuaji majipu na hatoi afueni katika kukata mirija au kufunga njia za mafisadi, walarushwa na wahujumu uchumi katika kupata na kujilimbikizia mali isiyo halali. Makundi hayo hayapendi kuumbuliwa mbinu zao za udhulumati.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli anasema kuwa vya moto anavipata. Ni kweli anavipata vya moto kwa sababu si chaguo lao. Makundi hayo hayajapendezwa na hayatapendezwa kwa sababu waliyemtaka hakuwa. Si chaguo lao. Ni kama vile simulizi ya mama mkwe kumkataa mke wa mwana wake wa kiume na kumtia kila aina ya kasoro hata kama hana kasoro.
Namalizia makala yangu kwa kusema machache kuhusu vyama vya siasa. Tangu ujio wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, na utekelezaji wake wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, umma wa Watanzania ulianza kushuhudia kuona vitimbi na kusikia kauli za kejeli, chuki, fitina, dharau hata wakati mwingine kupokea matusi ya rejereja baina yao wanasiasa.
Chama cha siasa kilichoshinda kilikuwa adui mbele ya vyama vilivyoshindwa. Vyama vilivyoshindwa vilionesha wazi kutoridhika na matokeo ya upigaji na uhesabuji wa kura za wagombea na hasa hasa nafasi ya urais. Misamiati ya wizi wa kura na utoaji hongo ili kupata uongozi ilianzishwa na kulelewa katika njia haramu ya rushwa.
Tangu wakati huo hadi leo, vyama vyote vipya kama vile NCCR-Mageuzi, TLP, CUF n.k. na chama kikongwe CCM, vimejikuta katika siasa za matukio badala ya kuimarisha siasa za masuala (itikadi). Matokeo yake tumezalisha wanachama na viongozi wa kushughulikia siasa za matukio na kusahau siasa za masuala ya chama.
Leo unaposikia maneno ya kejeli, mipasho au uchochezi n.k. ni matokeo ya kukosa itikadi na mwongozo wa chama cha siasa. Vyama vimetengeneza wanachama na viongozi uchwara ambao wanadhani siasa maana yake ni kupinga kila jambo – liwe limetoka upinzani au madarakani (serikalini).
Suala la siasa ya matukio na itikadi nitalizungumza wiki ijao penye majaaliwa. Usikose nakala yako. Leo nakuaga nikisema wanamuziki wa iliyokuwa bendi ya taarab ya Egyptian Musical Club, Dar es Salaam walipata kuimba wimbo ambao baadhi ya maneno yake yanasema: “Anaye mpenda baba, sisi tumfanye mama, Tumuwekee mahaba, kwa usiku na mchana.”
Kwa ushairi huo hekima inatufanya kutambua kuwa ‘wanayempenda wananchi, sisi tumfanye Rais wetu, tumuwekee mahaba kwa usiku na mchana.’