Mengi yanazungumzwa. Yanailenga Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk. John Magufuli. Mengine yanalilenga Bunge na hapa anaguswa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

Haya si mambo ya kuachwa au kupuuzwa. Kuna majibu yanahitajika. Majibu yanaweza yakawa ya faragha, au ya kwenye hadhara.

Baadhi ya wakosoaji wanamwona Rais Magufuli ni aina ya dikteta. Wanajadili kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa kana kwamba ndiye wa kwanza kufanya hivyo. 

Leo wapo wanaosema wanamkumbuka Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Wanasahau ni katika kipindi chao watu walipigwa risasi wakafa. Morogoro waliuawa. Iringa mwandishi aliuawa. Magufuli hakuwa hapo alipo sasa. Wanasahau polisi walioua wafuasi wa chama cha siasa Pemba. Matumizi ya gesi ya machozi yapo miongo mingi tu. Hili si jambo la fahari, lakini ni kujaribu tu kuonesha kuwa Mungu alifanya jambo la maana sana kwa binadamu – kumpa usahaulifu. 

Wanalalamikia kunyimwa fursa ya kuendesha mikutano ya hadhara, na hata ile ya ndani.

Wabunge wa Kambi ya Upinzani wanalalamikia kinachoendelea bungeni. Dk. Tulia amekuwa mwiba mchungu kwao. Wanasema amekosa uvumilivu, na kwa maana hiyo anachojua ni timua-timua na fungia-fungia ya wabunge.

Huku mitaani kuna malalamiko ya kwamba wapinzani wanaminywa kufanya mikutano halali, lakini wapenzi na wafuasi wa CCM wanaachwa watambe. Wanatoa mifano ya namna CCM walivyoachwa watambe jijini Mwanza na mjini Iringa, lakini wakati huo huo wapinzani wakibanwa Kahama, Dar es Salaam na katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Wanahoji hiyo intelejensia ya Jeshi la Polisi; iweje darubini yake ya kubaini uvunjifu wa amani iwe inatoa majibu chanya kwa wapinzani pekee, na si kwa CCM? Haya yanahojiwa mitaani.

Kuyajadili haya hakuhitaji hamaki, jazba wala mihemko. Mambo yanayoihusu nchi si ya kujadiliwa kwa wepesi au kupewa majibu mepesi ya aina ya kuchangamsha baraza, au ya funika kombe mwanaharamu apite.

Kwa mujibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuongoza nchi ni jambo zito mno. Ukiyasikiliza na kuyatafakari maneno ya Mwalimu, unaweza kujua hali aliyonayo Rais John Magufuli.

Sidhani, lakini inawezekana kabisa wakati sisi huku mitaani tukilia kufanya mikutano ya hadhara na makongamano katika ofisi na hoteli za kileo, Rais Magufuli yeye anawaza ni kwa namna gani atakidhi kiu ya Watanzania ya kuiona Tanzania mpya kiuchumi.

Wakati sisi tukiona kukosa kuandamana ni jambo la kutufanya tulie machozi, inawezekana Rais Magufuli na wasaidizi wake wanakesha wakisaka mbinu za kukabiliana na vitisho vya maadui wa ndani na nje ya nchi. 

Ni kama mtoto aliyetopea kwenye kelele za ushabiki kwa kutazama picha ya maigizo kwenye runinga. Wakati mtoto akipaza sauti pengine kwa kutaka mzazi wake awe pamoja naye katika kuiangalia picha inayooneshwa, mzazi akili yake inakuwa mbali akiwaza mlo, ada na maisha ya baadaye ya mtoto wake huyo. Kwa hiyo, wakati wapinzani wao wakililia kuandamana, inawezekana Rais Magufuli yeye anatafuta mambo mengine makubwa zaidi kwa ustawi wa nchi yetu.

Hapa ni vema tukatambua kuwa kazi moja kubwa waliyonayo ndugu zetu wa vyama vya upinzani ni kuona wanaiondoa Serikali iliyoko madarakani. Kazi hiyo wanaifanya kwa kipindi chote cha miaka mitano. Hawana muda wa kupumzika. Kwao, kuwaambia wasiendeshe siasa ili kuipa nafasi CCM itekeleze ahadi zake, ni sawa na kuwaambia kuwa mwaka una vipindi vya majira mbalimbali! Wapinzani hawajui kama mwaka una vuli, masika au kipupwe! Kwao kila baada ya uchaguzi, unaanza uchaguzi mwingine. 

Najaribu kutumia akili ya kawaida kupata jawabu kwa swali hili la kupigwa marufuku kwa mikutano ya hadhara na ya ndani – mingi ikiwa ni ya vyama vya upinzani.

Kwa namna yoyote iwavyo, Rais Magufuli sidhani kama ni dikteta wa kufikia kiwango cha kuliagiza Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya vyama vya siasa bila kuwa na sababu. Sidhani.

Nashawishika kuamini kwamba huenda kuna sababu za msingi za kuwapo kwa agizo hilo ambazo kwa wale wataalamu na wabobezi wa masuala ya mustakabali wa nchi, haziwezi kutangazwa kwenye televisheni, redio, magazeti au kupitia mikutano ya hadhara. 

Inawezekana kukawapo jambo nyeti kitaifa linalomfanya yeye na Serikali yake wachukue hatua hiyo, na wazibe masikio kwa lawama zozote zinazoelekezwa kwao.

Uongozi wa nchi unakuwa mgumu pale kiongozi mkuu anapotaka kumfurahisha kila mtu. Kiongozi wa nchi wakati mwingine yampasa asimamie anachoamini hasa akijua kina manufaa mapana kwa jamii pana.

Pamoja na nia nzuri ya Serikali ambayo pengine imefichika, bado kuna sababu kwa viongozi wetu kutokuwa waoga kujibu hoja hadi zikaweza kueleweka kwa wananchi.

Kama lipo suala la usalama wa nchi linalosababisha Serikali ichukue hatua za kuzuia mikutano, ni wajibu wa wahusika kulieleza jambo hilo kwa wadau. Kwa mfano, sioni ni kwanini viongozi wenye dhamana wasiwaite viongozi wakuu wa vyama vya siasa wakaketi faragha, wakaelezana ukweli. Kama viongozi wetu wa vyama vya siasa ni wazalendo, bila shaka baada ya mazungumzo wanaweza kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuendesha siasa zao. Kutoka hapo wanaweza kuwa na maelezo mazuri kwa wafuasi wao. Si kila jambo lazima lizungumzwe majukwaani, hasa kama jambo lenyewe ni lenye maslahi kwa nchi.

Kuna mifano mingi mizuri ya wanasiasa mahasimu katika mataifa kadhaa ambao huunganishwa na jambo lolote linalohusu maslahi ya nchi. Sidhani kama kuna viongozi wa Chadema, CUF, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, UDP au chama kingine cha siasa wanaoweza kupinga hoja njema zinazotolewa na viongozi wa Serikali kwa jambo linalohusu usalama wa nchi yetu.

Hili naliunganisha na kile kinachoendelea bungeni. Inawezekana Rais Magufuli na wasaidizi wake wakawa na hoja njema ya kwamba baada ya Uchaguzi Mkuu, sasa ni kipindi cha wao kuachwa wakatekeleza kile walichowaahidi Watanzania. Hiyo ni hoja nzuri yenye kuweza kuelezwa na kueleweka kwa upande wa CCM na wafuasi wake.

Lakini linalopokuja suala la dhima kuu ya chama cha siasa kushika dola, maelezo na msimamo huo wa CCM na Serikali yake hauwezi kukubalika kwa wapinzani. Matokeo yake ndiyo haya ya Serikali kupewa majina mengi. Hili si jambo la ajabu katika mfumo wa siasa ya vyama vingi.

Hata hivyo, ni ukweli ulio wazi kwamba haiwezekani Tanzania ikabaki kuwa nchi ya malumbano ya kisiasa tu. Hata kuzuiwa kuoneshwa ‘live’ kwa Bunge, ingawa wapo wanaokosoa uamuzi huo, lakini kwa upande mwingine kuna mantiki. Hii ‘live’ imewafanya wawepo watu ambao kutwa nzima wapo mbele ya runinga tu! Bunge likianza saa 3, nao wanaketi. Likiahirishwa saa 7 mchana nao wanakwenda kula. Likirejea saa 11 jioni tayari wanakuwa kwenye nafasi zao. Likiahirishwa saa 2 usiku, nao wanaahirisha hadi kesho! 

Hatuwezi kuwa na nchi ya aina hiyo ambayo kuna watu wanawasindikiza watu wengine kufanya kazi zao! Hata kama tunalalamika kuwa ni kuminya haki za msingi za kupata habari, bado tunapaswa kukubaliana na faida za uamuzi huu.

Bunge ni mahali pa siasa. Bungeni hoja hujibiwa kwa hoja. Kanuni zinazuia matusi na mambo mengine yasiyo ya staha, lakini hazimzuii mbunge kuzungumza maneno yasiyopendwa na mpinzani wake.

Wajibu wa Serikali ni kuwa na majibu, tena majibu yaliyojitosheleza kwa zile hoja zinazoelekezwa kwake. Hali ilivyo sasa ni kama kuna ombwe la viongozi kujibu hoja za wapinzani na matokeo yake Naibu Spika ameamua kufanya kazi zilizopaswa kufanywa na Serikali.

Woga na kutojiamini ni silaha dhaifu kwenye ulingo unaoshirikisha vyama vingi vya siasa. Aliyekuwa Mbunge wa Bunda, Mzee Steven Wasira, anaweza kuwa na udhaifu wake, lakini kwenye suala la kujibu hoja, alikuwa mahiri. Hoja ilipotolewa, ikaonekana ngumu, kwa Wasira ililainishwa kwa majibu ya kujiamini. Alifanya hivyo ndani na nje ya Bunge.

Bungeni ni kama kwenye uwanja wa mpira. Timu inapaswa kuwa na beki ambaye mshambuliaji sharti ajiulize mara kadhaa namna ya kumpita. Washambuliaji wakishajua hakuna beki wala kiungo mkabaji, wataongeza mashambulizi. Timu isiyokuwa na wakabaji husubiri huruma ya refa isifungwe. Sasa inaelekea refa wa Serikali bungeni ni Naibu Spika. Pamoja na kuwapo lugha zisizo za staha, bado Naibu Spika anapaswa awe mvumilivu. Kufuata kanuni pekee hakuwezi kumsaidia. Bunge, pamoja na kutumia sheria na kanuni, pia linatumia desturi. Asiwe defensive kupindukia! 

Mwisho, niseme maneno mawili. Mosi, Rais Magufuli, namuomba amsamehe yule kijana aliyemtolea lugha isiyofaa kupitia Facebook hata akafungwa miaka mitatu au kulipa faini ya Sh milioni saba. Wakristo na Waislamu wameaminishwa kwenye kusamehe. Amsamehe halafu amkaribishe – ampe fursa ya kukutana naye kijana amweleze kilichomsumbua hata afikie hatua ya kutenda vile. Amkaribishe chakula na baada ya hapo wapige picha! Kwa kumsikiliza, Rais atakuwa ameambua jambo fulani lenye manufaa kwa uongozi wake.

Naamini baada ya tukio la aina hiyo idadi ya matusi itapungua. Watabaki vichwa ngumu tu. Sioni mbinu ya kuwafunga au kuwapiga faini watu wa aina hii kama itakuwa na tija.

Pili, Jeshi la Polisi litumie busara ya kawaida kukabiliana na upinzani na wapinzani. Wajue kila wanachofanya, hata kama ni kwa utashi wao, wananchi wanajua aliyewatuma ni Rais Magufuli.

Naamini viongozi wa Serikali, wale wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa vyama vya siasa na wadau wengine wanapaswa kuketi faragha kupeana ukweli juu ya hatua hizi za kuzuia mikutano na mambo mengine. Penye wengi hapaharibiki jambo. 

Sidhani kama Rais Magufuli kaamua tu kwa roho mbaya kuona Serikali yake ikichukua hatua hizi inazochukua. Bila shaka kuna jambo. Tatizo, wadau hawajawekwa faragha wakaelezwa hilo jambo. Kuwaacha wananchi waendelee kuishi kwa hisia kutawajaza hasira na chuki dhidi ya Serikali yao. Viongozi wetu wawe na ujasiri wa kueleza au kujibu hoja kinagaubaga bila woga.